Utashi wa Mungu na Upendo wa Mungu - Luisa Piccarreta
39 subscribers
256 photos
50 files
514 links
Fahamu kuhusu kutimia kwa Sala ya Baba Yetu kupitia Maandishi ya Mtumishi wa Mungu Luisa Piccarreta, Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - Kuishi Utashi wa Mungu
Download Telegram
Ah, ndiyo, Ewe Uhai wa Moyo Wangu, mimi ninalia pamoja nawe. Maneno yako hayo ya ‘Lazaro, amka uje nje!’, mimi ninataka niyajaze na ‘Ninakupenda’, na ‘Ninakuabudu’, ili kauli hiyo ikushawishi uwe unayarudia rudia juu ya kila moyo. Huku ukiwa unayamwaga machozi yako kama umande uletao baraka, uwe unarudia kusema: “Toka nje ya kaburi hilo la utashi wa kibinadamu, na ebu uingie tena katika uhai wa Utashi wa Mungu”. Kwa minajili hiyo, watakapokuwa wakisikia uamrisho wa sauti Yako, wote waamke na kuuunda Ufalme wa ‘FIAT’ Yako.

Ewe Yesu Wangu Mpendwa, mimi sitakuacha peke yako kamwe. Ingawa kama sijui ni kitu gani cha kukuambia, lakini, angalau ninajua kukuambia ‘Ninakupenda, Ninakupenda’. Ninataka, matendo yako yote, hatua zako, maneno yako, na hata machozi yako yote, niyasuke pamoja na ‘Ninakupenda’ yangu ndogo, na mwishowe nataka nikuombe utupatie FIAT Yako yenye kutawala, na yenye kuamrisha. Kwa sababu hiyo mimi ninakufuata pamoja na wanafunzi wako. Wakati unapolala usingizi pale ndani ya mashuha, ikiwa ni ishara ya pumziko unalotaka kumpatia mtu yule atakayeishi katika Utashi Wako wa Kimungu, dhoruba kali inawatia hofu Mitume, hali inayowafanya wapige kelele wakilia: “Mwalimu, Utuokoe, vinginevyo tutateketea!”. Yesu Wangu, hicho siyo kitu kingine isipokuwa ni dhoruba itokanayo na utashi wa kibinadamu ambao, unapovumisha mawimbi yake ya kutisha na makali katika bahari ya maisha, huwa inatutishia kutuzamisha. Ewe Yesu Wangu Mleta amani, pamoja na Mitume, na kupitia ‘Ninakupenda’ yangu, ninapiga nami kelele kwa nguvu nikisema: “Mwalimu, utuokoe, vinginevyo tutateketea!”. Tafadhali, amrisha hii dhoruba ya utashi wa kibinadamu na uifanye itulie. Kwa nguvu ya amri ile ile uliyoitoa juu ya ile dhoruba iliyowakabili Mitume, sasa upatanishe utashi wa kibinadamu na Utashi wa Kimungu, ili utuwezeshe tupumzike katika mikono ya uhakika ya ‘FIAT’ Yako ya Juu kabisa.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA KUMI NA TISA

Tumfuate Yesu katika tendo lake la kuingia Yerusalemu na tumwombe atupatie ushindi wa Utashi wa Mungu dhidi ya utashi wa kibinadamu. Kishapo tumfuate katika tendo lake la kuweka Sakramenti mbalimbali.

Ewe Chema Changu Mpendwa, ninakuona unageuka na kuelekea Yerusalemu tena. Mimi nanakusindikiza kwa kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’. Lakini, ni uchungu upi ambao Moyo Wako unakosa kuukabili dakika hii? Unapoingia hapa Hekaluni unaona ni jinsi gani watu wanavyoikufuru? Je imekuwa sasa ni soko badala ya kuwa ni nyumba ya Baba Yako? Hapo Wewe unatwaa mijeledi ya kamba kamba, na kwa taratibu na kwa amri ya kimungu unaanza kupita kulia na kushoto, ukipindua juu na chini mambo yao yote, huku ukiwafukuzia nje wote wale wanaolikufuru Hekalu. Kutokana na nguvu ya kitendo Chako cha kuamrisha, hamna hata mmoja anayethubutu kukupinga, bali wote wanakukimbia. Ewe Yesu Wangu, Mtawala wa Kimungu, ‘Ninakupenda’ yangu inaingia na kuzifunika zile kamba za mijeledi ili uzichukue tena kamba hizo kwa ajili ya kuuchapa na kuufukuzia mbali utashi wetu wa kibinadamu, ambao umelikufuru sana Hekalu lako hai, yaani roho zetu. Lo, hebu uuchape mijeledi kabisa, kiasi kwamba usithubutu tena kutawala bali utoe kabisa nafasi na kiti chake cha mamlaka kwa Utashi wa Mungu.

Ewe Mchumba Wangu wa Mbinguni, ‘Ninakupenda’ yangu inakufuata katika tukio lile la kuingia Kwako kwa shangwe katika mji wa Yerusalemu. Mimi ninagonga mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu juu ya yale matawi waliyoshika makundi ya watu, naugonga juu ya nguo zile wanazotandika njiani mbele ya miguu yako, ninaugonga katika zile kelele na mashangilio ya ‘hosana, hosana’ wanayokuimbia hao makundi ya watu. Ninagonga muhuri huo kwa ajili ya kukuomba ulete ushindi wa Utashi Wako. Ewe Mfalme Wangu Mtukufu, hilo Umbo Lako la Mtekaji, la Mshindaji, linaelekea kuniletea habari njema ya furaha. Lo, hebu unifurahishe! Kwa Binti Mdogo wa Utashi Wako, hebu sema hivi: “Utafika Ufalme wa MAPENZI YAKO YATIMIE hapa duniani kama vile kule Mbinguni” . Mimi sitakuacha kamwe bali nitaendelea kukuchosha kwa ‘Ninakupenda’ zangu hadi pale nitakapokuwa nimekushinda na wewe utakapofikia kuniambia: “Binti Yangu, Wewe umeshinda. Ninakuahidia kwamba Ufalme Wake utashuka hapa duniani. Wewe sasa na unifuate Mimi. Pendo Langu lina linaonja hamu ya kusindikizwa nawe. Maadui zangu wametafsiri vibaya hayo makelele ya makundi ya watu wanapoimba ‘hosana, hosana’ na kwa sababu hiyo wanatafuta namna ya kuondoa uhai wangu. Mimi lakini, kabla sijakufa, ninapenda niweke Sakramenti mbalimbali kama kumbukumbu ya mwisho ya Pendo Langu la kina, kwa ajili ya wana Wangu, na kwa ajili ya uhai wa kudumu kati yao. Na wewe utaendelea kuniomba daima hiyo ‘FIAT’ yangu ya Kimungu, katika kila Sakramenti, ili kusudi watu wawe wanajipatia Ufalme Wake”.

Ewe Pendo Langu, naendelea kukusogea na kujibana kwako. Na pindi unapoweka Sakramenti mbalimbali, mimi ninaingiza ‘Ninakupenda’ yangu katika kila ubatizo, ili kwa nguvu ya kauli hiyo, nikuombe ‘MAPENZI YAKO YATIMIZWE’ kwa ajili ya kila mmoja aliyebatizwa. Hiyo ‘Ninakupenda’ yangu ninairudia tena katika Sakramenti ya Kipaimara, ili kukuomba ushindi wa Utashi wako wa Kimungu ndani ya kila mwana-Kipaimara. ‘Ninakupenda’ yangu inakuwa ni muhuri wa Sakramenti ya Mpako Mtakatifu ili kusudi nikuombe, kitendo cha mwisho cha uhai wa kila aliye kufani, na kiwe katika Utashi Wako wa Kimungu. Ewe Yesu Wangu, hiyo ‘Ninakupenda’ yangu, ninaitia katika Sakramenti ya Daraja Takatifu ili nikuombe tupate Mapadre wa Utashi Wako na wa Ufalme wake ndani yao. ‘Ninakupenda’ yangu inaenea hadi ndani ya Sakramenti ya Ndoa Takatifu ili kukuomba Wewe utujalie familia zilizoundwa na kujengwa katika ‘FIAT’ yako ya Kimungu. Hiyo ‘Ninakupenda’ yangu, inapanda hadi ndani ya Sakramenti ya Kitubio ili kukuomba Wewe kwamba kila Kitubio wanachofanya na kiwe ni kifo cha dhambi na uwe ni uhai wa Utashi Wako wa Kimungu ndani yao.
Ewe Yesu, Uhai Wangu, hiyo ‘Ninakupenda’ yangu haitakuacha kamwe kwani itakuwa na Wewe kwa umilele. Kwa sababu hiyo, ninaiweka kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’ ndani ya kila Hostia ya Sakramenti, katika kila chozi la siri unalolidondosha ndani ya kila Hostia iliyogeuzwa, katika kila tusi na uovu unaotendewa, katika kila fidia unayotoa. Ninaiweka hapo ili, pamoja Nawe, niweze kukuomba kuwa: Ufike Ufalme wa Utashi Wako, hapa duniani kama kule Mbinguni. Ewe, Mpiga-mishale Wangu wa Mbinguni, kutoka katika kila Tabernakulo, uzijeruhi tashi za kibinadamu, eneza minyororo Yako ya Pendo, utumie mbinu zako zote za upenzi ili uweze kuzishinda tashi zote za kibinadamu. Badala yake tunaomba utujalie Utashi Wako, ili kusudi huu utashi wetu ufikie kuwa kitu kimoja na Utashi Wako, na iwe hivyo hapa duniani kama vile kule Mbinguni.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA ISHIRINI

Tumfuate Yesu katika Bustani ya Getsemani na katika maumivu ya Mateso Yake
.

Ewe Yesu Wangu Mteseka, baada ya Wewe kujiweka na kubaki katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, unasambaza uhai Wako katika kila Hostia ili kusudi uweze kushuka na kuingia katika kila moyo, na ili kusudi uwe daima tayari kuwafikia wanadamu mbalimbali wanaokuhitaji. Hilo umelitenda ili kutuambia kwamba: “Mimi sitawaacha bali ninabaki pamoja nanyi nyote, ili kusudi niweze kujenga Ufalme wa Utashi Wangu wa Kimungu kati ya watoto Wangu”. Pendo lako sasa limeridhika. Halafu unaingia katika bahari ya Mateso yako. Hatua za miguu yako zinaelekea kwenye Bustani ya Getsemani. Ninakuona ukianguka kifudifudi ardhini ukisali. Lakini pindi ukisali, unaingia katika mahangaiko na fadhaa, unahema, unaingiwa na maumivu makali sana, na unatoka jasho la damu. Mambo yote yote yanakuja mbele yako. Maumivu yote na dhambi zote, zote zikiwa ni matokeo ya silaha chafu za mauaji zilizopo katika utashi wa kibinadamu ambao unapiga vita dhidi ya Mungu. Ah, ni kweli, utashi wa kibinadamu, kwa kutumia silaha zake, huleta maumivu makali kwa Utashi wa Mungu. Kwa karne nyingi sana utashi huo wa kibinadamu umekuwa ukiuzuia Utashi wa Mungu, na bado unaendelea hata leo kuuzuia. Ewe Yesu Wangu unayekabiliwa na maumivu makali kabisa, huu moyo wangu duni unashindwa kuvumilia unapokuona Wewe umeanguka ardhini na unaogelea na kulowana katika Damu Yako Mwenyewwe. Ni hasa kwa ajili ya hoja hiyo, mimi ninakuomba utupatie Ufalme wa Utashi Wako wa Kimungu hapa duniani, ili kusudi, kwa nguvu ya silaha zake za Kimungu, uweze kuzishinda silaha za utashi wa kibinadamu, uweze kuutesa na kuuingiza katika maumivu makali, hata kuweza, kwa haki kabisa, kulipa kisasi kwa maumivu marefu ya karne nyingi sana, yaliyosababishwa nao huo utashi wa binadamu. Na bila kuupatia tena mwanya wa uhai, Utashi wa Mungu ushike uwanja wake wa uhai katika kila moyo. Na mimi, Ewe Yesu Wangu, ninapokuchukua na kukushika sasa kwa mikono yangu, ninapenda nikutulize kwa kutiririsha kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu’. Ninaitiririsha katika kila tone la Damu uliyomwaga, katika kila umivu, na katika kila hangaiko na kuhema kwako. Katika kila dhambi unayoiona, ninapenda nitengeneze mawingu ya ‘Ninakupenda’, ili kusudi jicho lako lisiweze kuangalia kitu kingine chochote isipokuwa hiyo ‘Ninakupenda’ yangu. Napenda pia kuwa kila picha chafu na ovyo ya madhambi mengi ifukuziwe mbali kutoka kwako. Naiweka hiyo ‘Ninakupenda’ yangu ili kukuomba kwamba Utashi Wako wa Kimungu utawale hapa duniani.

Ewe Yesu, hebu unisikilize: Kama Utashi Wako ungetawala, Wewe usingejikuta katika maumivu mengi na wala usingepata mateso makali yanayokumaliza namna hii. Kwa sababu hiyo, kabla ya kuondoka toka hapa Bustanini, tafadhali unipe kauli yako, umfurahishe huyu Binti Yako Mdogo na uniambie kwamba ushindi wa Utashi Wako wa Kimungu unafika.
Yesu Wangu Mteseka, maadui zako tayari wamekwisha kuingia hapa Bustanini. Wanakushika na kukufunga kwa kamba na minyororo, wanakukanyaga kwa miguu yao, wanakuburuza, wanakupeleka toka baraza moja la mahakama hadi baraza lingine. Ewe Pendo Langu, mimi ninakufuata hatua kwa hatua, ili juu ya maumivu yako yote nikaweke alama ya ‘Ninakupenda’ yangu na ndivyo niweze kukuomba kwamba, kwa kamba zako na minyororo yako, uufunge utashi wetu wa uasi, ili usithubutu tena kuupinga Utashi Wako wa Kimungu, bali badala yake uuache huru kabisa na kuuruhusu uwe unatawala. Ewe Yesu Wangu, maadui zako wala hawatulii, wanakujaza maumivu makali, wanakutemea mate hata kuziba uso wote. Wanakushitaki kama mhalifu wa jinai, na wanakuhukumu kufa na wanakufunga katika mahabusu. Ewe Mfungwa Wangu Yesu, mimi sitakuacha. ‘Ninakupenda’ yangu inafunika yale mate yote waliyokutemea ili kusudi Wewe usiwe unapata harufu ya mate hayo, bali upate harufu ya ‘Ninakupenda’ yangu. Nataka nikufunike mwili mzima na hiyo ‘Ninakupenda’ yangu ili kusudi katika maumivu yako yote, na katika matusi wanayokutukana, ‘Ninakupenda’ yangu iwe inakutetea na kukulinda, iwe inakunogesha, na iwe ni silaha itakayowafukuza na kuwakimbiza maadui zako na kuwaongoa wote kwa ajili Yako. Na hapo ndani ya gereza hilo jeusi kabisa wanamokufungia, ‘Ninakupenda’ yangu iwe ndiyo mwanga wako na msindikizaji wako anayekuomba utufungulie kutoka gereza la utashi wetu na utufanye sisi kuwa wana huru wa FIAT Yako ya Kimungu.

Ewe Yesu Wangu unayepigwa mijeledi, kwa muda fulani wanakutoa nje ya gereza ili muda huo wao waweze kubadilisha na kukuandalia mateso makali zaidi na ili wafanikishe kutekeleza nia yao ya kikatili ya kukuua. Wanakuburuza na kukupeleka kwenye mabaraza mengine ya mahakama, yaani kwa Pilato na kwa Herode. Huyu Herode ndiye anakudhihaki na kukuchezea hata akakuvalisha kitambaa cha watu vichaa. Tendo hili lilikuletea uchungu mkali usiowahi kusikika. Ewe Pendo Langu, Unapata mateso yalioje! Kwa njia ya ‘Ninakupenda’ yangu, ninataka nikushonee vazi lililoandikwa ‘Ninakupenda’ yangu ya mwanga, ili iwatie kiza hao adui zako, hata wasiweze kukutesa zaidi. Badala yake wawe wanakutambua Wewe na wawe wanakuomba ili utuondolee huu ukichaa wetu ambamo utashi wa kibinadamu umetutumbukiza. Na kwa kutufanya kuwa vichaa, unatufanya tupoteze akili yetu ya kutambua kitu kilicho chema na cha kweli, yaani kutekeleza Utashi Wako wa Kimungu.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA ISHIRINI NA MOJA

Tunaendelea kumfuata Yesu katika maumivu ya Mateso yake.

Ewe Yesu Wangu unayeumizwa sana, sasa wanakupeleka kwa Pilato tena na kule yanakusubiri mateso mengine mapya. Wanatoa hukumu ya kukupiga mijeledi. Wanakuvua nguo zako, wanakufunga kwenye nguzo ili waweze kukupiga mijeledi kwa ukatili wote. Mimi ninashika na kukumbatia nyayo zako za Kimungu ili niweze kutia alama ya ‘Ninakupenda’ yangu juu ya kila pigo unalolipata, juu ya kila kipande cha nyama zinazoraruliwa toka mwilini mwako, na juu ya kila jeraha wanalokusababishia mwilini mwako. Ninataka kupiga kelele na kulia ‘Ninakupenda’, na ninakuomba utuvue sisi lile vazi la utashi wa kibinadamu na utuvalishe lile vazi la Utashi Wako, ili kusudi tusiwe tunaonja wala kuona kitu kingine isipokuwa FIAT Yako ya Juu. Yesu Wangu uliyepigwa mijeledi, adui zako bado hawajaridhika. Kutokana na majeraha mengi hutambulikani tena. Moyo wangu unashindwa kuvumilia. Ningependa nikuokoe kwa njia ya kauli zangu za ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’ na ninapenda kukuomba utupatie FIAT Yako itakayotawala hapa duniani, ikiwa ndiyo nguvu pekee itakayositisha maumivu yako. Vinginevyo hayataweza kabisa kukoma, na mimi nitaendelea kuwa na uchungu ninapokuona Wewe unavyoteseka. Kishapo, wanakutia taji la miiba. Wanakuvalisha kipande cha kiraka cha nguo ya kifalme, wanaweka kipande cha mwanzi mkononi mwako, na ndivyo wanakutendea kama kinyago cha dhihaka. Ewe Yesu Wangu, Uhai Wangu, ninapenda hii ‘Ninakupenda’ yangu ipambe na kuremba kila mwiba unaotoboa Kichwa Chako, na ninakuomba utuondolee mbali hili taji la dhihaka, ambalo tumevalishwa na utashi wetu wa kibinadamu, utuvue na kiraka cha kitambaa cha kifalme cha utashi huo wetu, unyang’anye hiyo fimbo ya mwanzi toka mikononi mwetu, fimbo iliyo ni ishara ya matendo mengi yaliyo tupu na bila thamani yoyote, fimbo inayotupatia amri na maagizo ya kuchekesha na ya dhihaka tu. Badala yake, Ewe Yesu, utuvalishe taji la Utashi Wako wa Kimungu, utuvalishe kitambaa safi cha kifalme kitakachotutambulisha sisi kuwa watoto wake wa kweli. Utupatie mkononi mwetu fimbo ya kweli ya utawala na ya mamlaka ya FIAT Yako tunayotaka itawale na kuamrisha roho zetu.

Ewe Yesu, Mfalme Wangu, ‘Ninakupenda’ yangu inaendelea kulifuata Pendo Lako. Katika kukutana na kuunganika kuwa kitu kimoja, huunda pendo moja tu, kiasi kwamba mimi nafikia kuwa na pendo kubwa sana chini ya mamlaka yangu, hata linakufanya Wewe uwe unalisikia pendo langu wakati ule unapokuwa unasikia ile kauli ya kukuhukumu ufe, yaani pale walipopiga ile kelele ya ‘msulibishe, msulibishe’. Kwa upande wangu, mimi ninayageuza makelele hayo ya ‘msulibishe!’ na badala yake nitapiga makelele ya ‘Ninakupenda’ yangu ndani ya kila sauti, na juu ya kila mdomo. Nitasema: “Usulibiwe utashi wa kibinadamu ili Utashi Wako upate kutawala!”. Na kwa maumivu uliyokuwa unayapata wakati ule unapohukumiwa kifo, tunakuomba utuokoe kutoka kile kifo tunachosababisha juu ya FIAT Yako katika roho zetu, na fanyiza kwamba utashi wetu ufe na badala yake Utashi Wako wa Kimungu ufufuke, uamrishe, na ujenge Ufalme Wake katika matendo yetu yote.

Ewe Pendo Langu, moyo wangu unaelemewa na uchungu ninapokuona ukiupokea na kuubeba Msalaba. Wewe unaukumbatia na unauweka juu ya Mabega yako. Oh, ni jinsi gani ningependelea kuufunika Msalaba mzima kwa kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu’. Halafu ni jinsi gani ningependa nikuombe kuwa, kwa nguvu ya Msalaba Wako, machungu yale yote, ambayo Pendo Lako linayapeleka kwa wanadamu, yaweze kuleta nguvu ya FIAT Yako, itakayowaandaa wanadamu kuweza kuipokea himaya yake. Oh, ni jinsi gani ningependa nipige kelele katika kila umivu unalolipata, na katika kila tone la Damu Yako. Napenda niseme: FIAT Yako ifike!. Katika kila anguko, katika kila moja ya nywele zako zilizolowa kwa Damu Yako, katika kila kitendo cha kusukumwa ovyo ulichokipata ninasema: Ninakupenda, Ufike na Ufalme wa Utashi Wako!.
Yesu Wangu unayehema, unayekanyagwa kwa miguu, unayeburuzwa ardhini, sasa unawasili juu ya kilima cha Kalvario. Wanakuvua nguo zako, wanakulaza juu ya mti wa Msalaba, na kwa ukatili usiosemekana wanakupigilia Msalabani. Ninapenda kutiririsha ‘Ninakupenda’ yangu juu ya viungo vyote vya mwili wako vilivyoumizwa na kujeruhiwa, juu ya mifupa yako iliyotetereshwa na kulegezwa, juu ya matobo yote uliyopata wakati misumari ilipopigiliwa. Katika maumivu yako yote, ninapenda nitie kwanza kabisa mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu, na papo hapo napenda nikuombe utuvue sisi mambo yale yote yanayozuia Utashi Wako wa Kimungu usifufuke ndani ya mioyo yote na kuweza kueneza Ufalme Wake katika dunia yote.

Ewe Yesu Msulibiwa, pale Msalabani juu, unahema na na unateseka vibaya sana. ‘Ninakupenda’ yangu igonge mhuri wa kusitisha mihemuko yako, mhuri wa kusitisha maumivu makali na ya mateso ya Moyo Wako, na usitishe miali ya moto inayouunguza huo Moyo. ‘Ninakupenda’ yangu na iwe ni kiyoyozi chako, na izime kiu chako cha moto. Kwa mhuri huo wa ‘Ninakupenda’ ninagonga alama juu ya kila neno ulilowahi kutamka pale Msalabani. Katika hiyo ‘Ninakupenda’ yangu, ninapokea pumzi yako ya mwisho ili nikuombe, kwa ajili ya maumivu yale makali uliyoyapata pale Msalabani, utujalie sisi neema ya kuungua kwa kiu cha kuishi katika Utashi Wako wa Kimungu. Utashi Wako uliokuwa umeshuhudia mahututi yako katika utashi wetu, sasa ushuhudie kifo cha utashi wetu na FIAT Yako ifufuke katika mioyo yote, ipate ushindi na iweze kujieneza katika kizazi chote cha binadamu na itawale hapa duniani kama vile kule Mbinguni.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA ISHIRINI NA MBILI

Ndani ya ‘Ninakupenda’ yetu tunafungilia Ubinadamu Mtukufu wa Yesu, uliokufa. Pamoja Naye tunateremka kwenda Limbo. Na pale, tukiwa pamoja na Malkia wa Mateso, na pamoja na roho takatifu zile zote, kwa pamoja tunamwomba kuwa Utashi Wake wa Kimungu upate ushindi kati ya wanadamu.

Ewe Pendo Lako, ninakuona umekwisha kuzimia. Oh, ni jinsi gani ningependelea niweze kuzimia pamoja Nawe, lakini sikubahatika kujaliwa hilo! FIAT, FIAT!..... Ninapenda nikupokee mikononi mwangu ili kusudi niweze kufungilia huo Ubinadamu Wako Mtukufu ndani ya ‘Ninakupenda’ yangu. Kwa njia hiyo, katika kila kitu utakachokuwa unaona, uwe unaiona ‘Ninakupenda’ yangu, katika kila unachokisikia uwe unaisikia ‘Ninakupenda’ yangu, uwe unaigusa ‘Ninakupenda’ yangu. Hii ‘Ninakupenda’ yangu haitakuacha kamwe: Utashi Wako wenyewe ndiyo uhai wa ‘Ninakupenda’ yangu. Lakini je unajua ni nini anachotamani huyu msichana mdogo? Anataka kwamba, Ule Utashi wa Mungu ambao Wewe uliupenda na uliutekeleza katika maisha yako yote ya hapa duniani, huo sasa uufanye ujulikane kwa wanadamu wote, ili kusudi wote wapende na watekeleze Utashi Wako hapa duniani kama vile kule Mbinguni. Huyu msichana mdogo anataka akushinde na kukuteka katika pendo ili kusudi Wewe utoe Utashi Wako wa Kimungu kwa wanadamu wote. Lo, Ewe Chema Changu, ebu ukafurahishe haka kasichana kadogo duni, ambako hakatafuti kitu kingine, isipokuwa kile unachokitaka Wewe, yaani, kwamba Utashi Wako ujulikane na utawale hapa duniani pote.

Ewe Yesu uliyekufa, wakati ninapokuwa nimeufungilia Ubinadamu Wako katika kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’, nimekutengenezea namna ya mazishi katika ‘Ninakupenda’ yangu. Ninakuomba na Wewe uuzike utashi wa kibinadamu ili usirudie kuishi tena. Mimi pamoja na Mama Yako Mteseka, aliye pia ni Mama Yangu, ninapenda kuambatana nawe kwenda Limbo. Ninakusindikiza katika ‘Ninakupenda’ yangu. Pale nashuhudia tukio na hali ya kustaajabisha sana: Hapa mahali patakatifu, namwona Baba yangu Adamu, namwona Abrahamu, Mababu na Manabii wote, na hata Mpendwa Mtakatifu Yosefu na watu wote wema wa Agano la Kale. Oh, ni jinsi gani wanavyofurahia kukuona! Halafu, huku wakianguka kifudifudi penye miguuni Yako mitakatifu, wanakuabudu, wanakupenda, na wanakushukuru. Lakini inaelekea kuwa sherehe yao haijakamilika bado. Basi wote kama kwaya ya pamoja, na kwa sauti moja, kuanzia na yule Baba wa kwanza Adamu, wanakuambia: “Tunakushukuru kwa yale yote uliyotenda na kuteseka kwa ajili yetu sisi sote. Maadam umekwishatekeleza na kutimiza ile sehemu ya kwanza, yaani sehemu ya kutukomboa, sasa tunakuomba umalizie na kukamilisha ile sehemu ya pili, yaani, ufanye Utashi Wako wa Kimungu utawale hapa duniani kama kule Mbinguni”.

Ewe Pendo Langu, je husikii hizo sauti nyingi za wapenzi wako? Hata mwenyewe Malkia wa mateso anakusihi, na mimi nikiwa pamoja naye tunasema: Ufike, ufike hapa duniani Ufalme wa Utashi Wako. Fanyiza kuwa watu wote waujue Utashi Wako Mwabudiwa. Leo, siku hii ya kifo chako, ndiyo siku ya ushindi Wako mbalimbali, ndiyo siku ya sherehe yako ya ushindi. Je inawezekana kweli kwamba hupendi kunijalia sherehe ya ushindi wa Utashi Wako wa Kimungu dhidi ya utashi wa kibinadamu? Basi sasa, hebu nisikie sauti Yako tamu mno kabla hujatoka hapa Limbo. Unijalie kwamba Utashi Wako utawale na ushike himaya yake hapa duniani kama kule Mbinguni.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA ISHIRINI NA TATU

Katika ‘Ninakupenda’ yetu, hebu tuambatane na lile tendo la Ufufuko Mtukufu wa Ubinadamu Mtukufu wa Yesu. Tufuatilie pale ambapo Mfufuka atakuwa anamtokea Mama Yake na atakapowatokea Wanafunzi. Pale tutamwomba kwamba Utashi Wake wa Kimungu ujulikane kwa mapadre wa Kanisa Lake.

Ewe Yesu Wangu Mshindi, ninakuona unapotoka kule Limbo, ukiwa umetangulizana na lile jeshi lote la roho zile za watu wenye haki. Unaelekea na kurejea kaburini ili kusudi upate kushinda mauti na ili ukaufufue Ubinadamu Wako Mtukufu. Ni dakika tukufu ilioje! Kwa sababu hiyo ninataka niweke ‘Ninakupenda’ yangu juu ya kaburi wakati wa tendo lako la kufufuka, niiweke juu ya ule mwanga, na juu ya ule utukufu unaokuzunguka. Nataka nikuombe ufufuko wa Utashi Wako wa Kimungu ndani ya utashi wa binadamu. Sisi sote tufufuke ndani yako. Je Wewe hutaki kunipatia kile kilichobebwa ndani Yako? Basi mimi ninakuomba, kwa nguvu ya Ufufuko Wako, uvuvie juu ya kila mwanadamu, na kwa pumzi yako yenye maweza yote, uteremshe utashi wa kibinadamu, ili kusudi Utashi Wako ufufuke katika utukufu na katika hali ya ushindi. Ewe Yesu Wangu Mfufuka, pindi ulipofufuka hukutoka na kwenda Mbinguni. Tendo hilo linanithibitishia kwamba, siku zile 40 za ufufuko, ulizokaa bado kati ya wanadamu, ni uthibitisho wa Ufalme wa Utashi Wako kati ya wanadamu. Basi mimi sikuachi kamwe. Katika ‘Ninakupenda’ yangu, ninakufuata hatua kwa hatua katika kitendo chako cha kujitokeza kama Mfufuka kwa Mama Yako. Na kwa ile furaha mliyoipata na kuifurahia ninyi wawili, mimi pamoja na Malkia mwenye mamlaka, tunakuomba FIAT Yako. ‘Ninakupenda’ yangu inakusindikiza katika lile tendo lako la kujitokeza kwa Magdalena na kwa Mitume. Ninakufuata ili kukuomba kwamba Utashi Wako wa Kimungu ujulikane kwa mapadre ambao ndio Mitume wapya. Nao hao waufanye ujulikane kwa dunia nzima.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA ISHIRINI NA NNE

Hebu tuziite Mbingu na dunia ziambatane na Yesu katika tendo Lake la Kupaa Mbinguni. Tendo hilo tunaliunganisha kwa pete ya ‘Ninakupenda’ yetu huku tukiomba kwamba Utashi wa Mungu utawale katika dunia nzima.

Mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu unaendelea kukufuata katika matendo yote yale uliyoyafanya kama Mfufuka kati ya Wafuasi Wako.

Tunaziita Mbingu na dunia zikusindikize katika tendo Lako la Kupaa Mbinguni, na katika tendo Lako la kufungua milango ya Mbingu ambayo, kwa muda wa karne nyingi sana, ilikuwa imefungwa kwa ubinadamu ulio duni.

Na juu ya ile milango ya milele, mimi ninapenda kuweka pale mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu, na ninakuomba ile Baraka uliyokuwa umetoa kwa Wafuasi Wako wote waliokuwepo katika ile sherehe ya Kupaa kwako Mbinguni, na pia ninakuomba ubariki tashi zote za kibinadamu, ili kusudi ziweze kutambua manufaa makuu ya kuishi katika Utashi Wako.

Na kwa lile Pendo ambalo kwalo ulitufungulia milango ya Mbinguni, utujalie kwamba Utashi Wako wa Kimungu ushuke kutoka milango hiyo hiyo.

Ushuke na kuja kutawala hapa duniani kama vile unavyotawala kule Mbinguni.

Ewe Pendo Langu, Wewe sasa umekwisha kuwa Mbinguni. Endapo mimi sitaona kwamba ‘Ninakupenda’ yangu ndogo imeweza kukusadikisha Wewe kuuleta duniani Utashi Wako Mwabudiwa, basi mimi sitafanya kitu kingine, isipokuwa nitakutengenezea minyororo ya ‘Ninakupenda’ kati ya Mbingu na dunia.

Kwa minajili hiyo, Wewe uniachie milango ikiwa wazi daima, ili kusudi niwe na uhuru wa kuja na kuingia hadi miguuni pako na hadi mikononi mwako, kwa lengo la kukushonelea kwa pete za mnyororo wa ‘Ninakupenda’ yangu.

Nina uhakika kwamba mwishowe ni mimi nitakushinda Wewe na hatimaye Wewe utanipatia kile ambacho na Wewe unakitaka, yaani, kwamba Utashi Wako wa Kimungu utawale katika dunia nzima.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
Mtumishi wa Mungu
Luisa Piccarreta
inti Mdogo wa Utashi wa Mungu

“Ee Yesu, miguuni pako nakuletea uabudu na utiifu wa familia yote ya wanadamu. Ninaweka ndani ya Moyo Wako ile kauli ya ‘Nakupenda’ kutoka kwa watu wote. Juu ya Midomo Yako nakupigia busu langu, ili kukubandikia mhuri wa busu la watu wa vizazi vyote. Kwa mikono yangu nakukumbatia, ili kukubana kwa kumbatio la mikono ya watu wote, kwa ajili ya kukufikishia utukufu wa matendo yote ya wanadamu”

(Kutoka: KITABU CHA MBINGU, Juzuu Na. 12 - Mei 22, 1919)
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 28
Kwa Mheshimiwa Padre Msaidizi

Fiat

Mheshimiwa sana Padre Msaidizi,

Kutoka kwa Mwalimu mwema Angela La Stella nilipata karatasi lako lililokuwa na ombi lako la kutaka nikusaidie kidogo kwa sala zangu, na kwa Komunyo yangu Takatifu nk. kwa ajili ya kazi zako za kipadre.

Basi, tangia tarehe 20 Oktoba hadi leo hii, katika kila kitu nilichoweza kutekeleza katika umasikini wangu, nimekuwa ninaweka nia ya kutenda kwa ajili yako, yaani Misa Takatifu zote, Komunyo Takatifu zote na mengineyo.

Na ili nia yangu hiyo iweze kuwa na thamani zaidi, na ili iweze kukuletea wewe matunda ya utakatifu wa kweli, matunda ya neema za kushangaza na usizotegemea, nilimwomba Yesu awe anatenda kila kitu pamoja nami ili pamoja na zawadi za kwangu, niweze kukutolea zawadi za Yesu Mbarikiwa.

Nilifanya hivyo kusudi Upadre wako ujaliwe neema hizo zaidi na zaidi.

Kutokana na hilo, ninapenda kutumia nafasi hii kukutumia Heri nyingi sana kwa Sikukuu ya Somo wako na ninamwomba mpenzi Yesu abebe na kukuletea Yeye Mwenyewe zawadi hizo.

Zawadi anazokuletea kama Heri zangu ni hizi: ‘FIAT’ ndani ya moyo wako, ‘FIAT’ katika maneno yako, na ‘FIAT’ katika akili yako, ili hatimaye hiyo FIAT iiongoe nafsi yako yote na kuiumba upya nafsi hiyo hata iwe ni kitendo kimoja tu cha Utashi wa Mungu.

Na kutokea hapo wewe uwe ni mtu unayebeba Utashi wa Mungu na kuupeleka kwa watu wote.

Ni Utashi huo ndio unaoweza kuingiza amani, umoja, na utakatifu ndani ya watu wote.

Tunaonja sana hitaji kali kabisa la kupata utakatifu wa kweli, hasa hasa ndani ya Padre.

Na ni ‘FIAT’ ya Mungu peke yake ndiyo yenye kuweza yote, kwa vile ndiyo inayomiliki maweza yote.

Maweza hayo yapo katika nguvu yake na uwezo wake wa uumbaji.

Ndiyo inayoweza hatimaye kuleta na kuingiza ndani yetu ngazi na daraja la kweli la utakatifu.
Nakuomba na ninajikabidhi katika sala zako takatifu.

Na sasa, kwa heshima, nikibusu shavu lako la kulia, na nikipiga magoti mbele yako ninakuomba sana baraka yako ya kibaba. Ndimi,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 67.
Kwa Federico Abresch, wa Bologna

Fiat! – In Voluntate Dei!

Mpendwa Mwanangu katika Utashi wa Mungu,

Kwa Mama yeyote, aliye na watoto wake wanaokaa mbali, faraja pekee anayoonja ni pale anapofahamu kwamba watoto hao wanapenda kuishi katika Utashi wa Mungu.

Ninawaza ni jinsi gani Yesu Mpendwa anavyotamani jambo hilo, na ninafikiri pia kuwa msumari unaomchoma na unaomtoboa Yesu zaidi, ni pale watoto wake wanapokosa kuishi katika Utashi Wake.

Na lakini, yule Malkia wa Mbinguni angefanya nini kama angetuona sisi tukiishi pamoja Nao ndani ya utashi ule ule mmoja?

Ni hakika kabisa wangetuletea sisi uhai ili uwe mali yetu na ili tuufaidi. Hivyo ndivyo kuishi hasa katika Utashi wa Mungu.

Mungu Mwenyewe huchukua mambo yetu yote na kuyaweka moyoni mwake, na badala yake anatupatia utakatifu wake ili tupate kuufaidi, anatupatia Pendo lake, anatupatia Nafsi yake, ili mradi afurahie kutuona sisi tukiishi ndani ya ule Utashi Wake ambao ndio unaotuletea mema yake yote.

Mpendwa katika Utashi wa Mungu, kuishi katika Utashi wa Mungu haimananishi kubadili vitendo vyetu bali ni kubadili utashi tu: badala ya kuacha utashi wetu ushike hatamu katika vitendo vyetu, yatakiwa tuache Utashi wa Mungu ushike hatamu katika kila kitu tutendacho.

Na je wewe unataka kufahamu ni nini kinachotokea katika kila kitendo chetu?

Pendo la Mungu ni kubwa hivi na pia Wema wake ni mwingi hivi kiasi kwamba kila tunapoanza sisi kutekeleza tendo lolote huku tukihusisha Utashi wa Mungu, hapo hapo Uhai wa kimungu huanza kutengenezwa ndani ya hilo tendo letu.

Na uzima huo wa Mungu hurudia kutengenezwa katika matendo yetu, mara zote tunapotekeleza tendo letu lolote lile.

Je unadhani ni neno dogo nikikuambia kuwa, ili mradi nikiruhusu Utashi Wake ushike hatamu, Mungu huwa ananipa uwezo na nguvu ya kutengeneza Uhai mwingi wa kimungu katika matendo yale yote ninayofanya?

Muujiza huo mkubwa hutokea kila mara, iwe katika vitendo vya kimaumbile na vya kawaida au katika vitendo vidogo vidogo, ili mradi tu pawepo na Utashi Wake.

Na mintarafu udhaifu wetu, mahangaiko yetu na mengineyo, usijali sana. Bora tu pasiwepo utashi wetu sisi kwa vile ndio huo unaotuharibia mambo yetu.

Matatizo na shida zetu hizo zote vinaweza kutumika na Mungu kama kikanyagio au kikalio ambapo Utashi wa Mungu hutengenezea kiti chake cha mamlaka na cha utawala juu yetu sisi wenyewe.

Au ni kama vile kokoto na vifusi vya vipandevipande vya mabomoko ya jengo vinavyoweza kutumika na mtu anayeanza kujenga nyumba yake.

Au pia ni kama udongo ulio mkiononi mwa Mungu aliye ni Mkulima wa mbinguni, ambaye bila utashi wetu sisi, anatumia shida na matatizo yetu na kuyafanya yachanue maua mazuri ya kupendeza kwa ajili ya usitawi wa Ufalme Wake. Katika mikono ya kimungu ya FIAT, kila kitu kinatumika kwa ajili ya utukufu wake Mungu na kwa ajili ya manufaa yetu sisi.

Hata hivyo, ninakushauri usiwe unawaza mno juu ya matatizo, shida na mapungufu yako. Kwa jinsi unavyozidi kuyafikiria hayo, ndivyo yatazidi kukuelemea na kukukandamiza moyoni.

Kumbe lakini, kwa jinsi unavyoacha kuyawazia, ndivyo yatazidi kufifia na hivyo yataacha kukutesa.

Zaidi ya hilo, elewa kwamba Yesu Mtamu huwa hatazami na kupima kile tunachoonja bali anapima zaidi kile tunachopenda.

Yaani, mara nyingi anatuonea huruma na anatuongezea Neema yake na nguvu yake hata kuyafanya matatizo na shida zetu zigeuke kuwa neema na nguvu yetu.

Na hatimaye, Yesu Mpenzi, kwa vile anapenda sisi tuishi katika Utashi Wake, huwa hapendi kujihusisha na wale waliokufa, bali anajihusisha na wale walio hai.

Kwa sababu hiyo, matatizo na shida zetu ni ishara tu kwamba tupo bado hai na wala hatujakufa bado.

Na Yeye, kwa vile anataka ajitokeze kama Mshindi, anayashinda matatizo hayo na anayageuza kuwa mapambo mazuri kabisa ya Ufalme Wake.
Kwa hiyo basi, jipe shime, uwe na ujasiri na uwe na imani.

Hizo ndizo silaha zinazomshinda hata Mungu.

Endapo hatutatekeleza hatua za awali, hatutaweza kufanya hatua ya pili, na ya tatu, na nyingine nyinginezo zinazofuata.......

Kama hatutajitumbukiza baharini, basi hatutaweza kuoga wala kuogelea ndani yake.

Basi, lililo muhimu ni sisi kuanza kwa dhati; mengineyo yatafuata yenyewe. Najikaabidhi sasa katika sala zako.

Umwambie na huyo mtoto mdogo Pio kwamba katika kila kitu atendancho awe anasema hivi: “Yesu, utwae utashi wangu na unipe Utashi Wako”.

Umsaidie na kumlea awe mtakatifu ili awe kweli kweli mtoto wa Utashi wa Mungu.

Ninaikabidhi familia yote katika Utashi wa Mungu.

Kwa njia hiyo utajipatia wewe mwenyewe ile neema ya kuujua zaidi huo Utashi wa Mungu.

Nawatakieni ninyi nyote salamu za FIAT.

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 23
Kwa Mama Cecilia
25 Februari, 1933

Y.M.Y.A. – Fiat
I.V.D. D.G.

Mheshimiwa Mama yangu Mpendwa,
Unisamehe kwa kutokukuandikia barua, lakini uwe na uhakika kuwa mimi huwa sikusahau mbele ya Bwana Wetu ili akupe daima nguvu na neema unazohitaji katika majukumu muhimu na magumu kabisa aliyokukabidhi.

Mimi ninatarajia kuwa kazi yako ya kwanza kabisa ni kuwalisha mdomoni manovisi wako kwa mkate wa Utashi wa Mungu.

Lakini, ndani ya mkate huo unaowalisha, ni budi uwe unatia dosi kali za viungo vya upendo. Uwe ni upendo wa kimbingu kabisa.

Utie pia dosi za viungo vya utamu wa Yesu toka mdomoni pako ili hata manovisi wawe wanapata na wanaonja ladha ya utamu huo.

Kwa nguvu ya dosi hizo, maneno machache wanayopata manovisi toka kwako yawe yanawatosheleza kwa ajili ya kuwafanya wawe watakatifu.

Ikiwa hivyo, hawatakuwa wanakwenda kutafuta semina ndefu ndefu ambazo, ingawa kama huwa zinavutia masikioni, lakini huwa mara nyingine zinaacha roho za wasikilizaji katika hali ya njaa na kiu.

Mama mpendwa sana, kwa niaba yangu uwaeleze manovisi kwamba wasiwe wanatafuta na kuokota vijiti vidogovidogo na nyasi nyasi kavu, bali wawe wakitafuta ule mkate wa mbingu ambao Yeye Yesu Mtamu hupenda kuwapatia kwa njia ya wewe, yaani ule mkate wa FIAT Kuu.

Na wala Yesu hatawauliza jambo lingine isipokuwa jambo hili, yaani: Je, katika kila tendo Mapenzi ya Mungu yalitimizwa?

Mama mpendwa, kama wewe unavyofahamu vema kuliko mimi, neno muhimu kupita yote ni kutokugomea chochote mbele ya Utashi wa Mungu.

Kugomea gomea jambo fulani, kukataa kutawaliwa na Utashi wa Mungu ina maana ya kubomoana na kuvunjavunja utakatifu; ni sawa na kufanya utakatifu uwe vipande vipande kiasi kwamba sisi wenyewe tusiweze tena kuelewa namna ya kupata utakatifu.

Tutageuka kuwa ni mwili ambamo viungo vyake vya mikono na miguu yake na hata moyo wake vimeng’olewa.

Oh, utakatifu gani duni wa jinsi gani huo ambamo hakuna uhai kamili wa Utashi wa Mungu?

Kwa hiyo, Mama yangu, ebu tuwe tunaupenda sana sana Utashi wa Mungu, tuwe tunautekeleza daima.

Hata kama itagharimu uhai wetu, mbona tutarudishiwa uhai ulio bora na mzuri zaidi?

Ebu tujitahidi kushughulika ili kuufanya Utashi huo wa Mungu ujulikane na kupendwa na watu wengine.

Hebu sasa turejee kwenye jambo letu linalotuhusu.

Mimi sisadiki kwamba kumetokea na wala kwamba kutatokea namna yeyote ile ya kivuli cha kugombana au kuchukiana.....
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 90
Kwa Sista Remigia

Fiat

Binti yangu mpenzi Sista Remigia,

Ninakuomba usiwe unapoteza muda. Oh, ni jinsi gani ningependelea kusikia ukisema: “Mimi siwazii iwapo nipo mzuri au kama napendeza au iwapo sipendezi. Wala siwazii iwapo naona ubaridi au naonja joto. Wazo langu ni moja tu, yaani ni kwa namna gani ninavyoweza kutiririsha matendo yangu yote na hata nafsi yangu mwenyewe ndani ya Utashi wa Mungu”. Ikiwa hivyo basi ni Yesu Mwenyewe atafikiria namna ya kukufanya wewe kuwa mtakatifu na ni Yeye atakayekufanya uwe na utulivu endelevu katika mambo yako, atakufanya uwe mwema kadiri anavyotaka wewe uwe. Kwa mara zote unapojifikiria juu yako wewe mwenyewe, hata ikiwa ni katika mambo mema, Yesu hatathubutu kukufunga kamba au hatamu, na kukuongoza kwa lazima, ili akufanye uwe Yesu wa pili atakayekuwa ni mrudufu wa uhai wake. Umwachie kazi hiyo aifanye Yesu Mwenyewe, na upesi sana wewe utajionea mwenyewe, jinsi unavyobadilika kuwa mtu mwingine kabisa, tofauti kuliko ulivyo sasa hivi. Yesu anajua namna ya kufanikisha zaidi jambo hilo kuliko tunavyoweza kufanya sisi wenyewe. Kwa hiyo, umwachie tu atekeleze Yeye.

Ninapenda kukutumia matashi yangu na ushauri wangu. Lakini je unajua ni matashi gani hayo? Ni matashi na ushauri wangu kwamba sasa usiwe kamwe unajifikiria wewe mwenyewe ndani yako, bali sasa ujifikirie daima ndani ya Yesu. Oh, ni jinsi gani Yesu atakavyokupenda! Atakubeba mikononi mwake, na atakupatia kiti cha kukaa ndani ya Moyo wake mdogo. Uwe makini na endelea kuishi ukiwa umejikabidhi nafsi yako kikamilifu kabisa ndani ya Yesu.

Ninakuaga, ni mimi,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 125
Kwa Monsignor
10 Januari, 1944

Mheshimiwa sana Monsinyore,

Mimi sielewi bado namna ya kukushukuru kwa heshima yako ya kunijali hata ukaweza kunikumbuka mimi mtumishi mdogo sana wa Yesu.

Sielewi namna ya kukulipa kwa hilo. Kitu kimoja tu ninaweza kufanya, nacho ni kusali nikimwomba Yesu Mpenzi akusaidie uweze kuishi katika Utashi wa Mungu, kwani ni huu Utashi wa Mungu peke yake ndio unaoweza kutufanya tuwe na furaha na pia ndio unaweza kutufanya tuwe watakatifu kwa nguvu ya utakatifu wake wenyewe.

Zaidi ya hilo, ni kwamba tamanio moja tu la Yesu ni hili kuwa sisi tuishi katika Utashi Wake kwa vile, kama tunaishi ndani ya Utashi Wake, Yeye ataweza kutupatia kitu kile anachopenda kukitoa kwetu.

Yesu anapenda kututengeneza na kutufinyanga upya katika Pendo lake, lakini kwa bahati mbaya utashi wetu wa kibinadamu ni mdogo mno hata hauna nafasi na mahali pa kumweka. Yesu anataka atupatie neema lukuki, lakini utashi wetu hauna uwezo wala nguvu za kuzipokea neema hizo.

Kwa hoja hiyo, Yesu, anatamani kuuona Utashi Wake Mtakatifu ndani yetu, siyo tu kwa lengo la Yeye kuweza kutupatia sisi kile atakacho, bali ni kwa lengo la kutufanya sisi kuwa kivuli halisia au nakala halisia ya Yeye mwenyewe.

Ni kwa sababu hiyo, anapotuona tukiwa tayari katika Utashi Wake, Yeye husherehekea na kusema: “ Hatimaye nimeweza kupata mahali pa kuweka nafsi yangu. Utashi Wangu hapa utaweza kuhifadhi vizuri neema zangu, Pendo langu, na hata Utakatifu Wangu”.

Basi, Padre mwema, ebu kwa moyo wetu wote tupende kuishi katika Utashi wa Mungu.

Utashi huu utakuwa unatuhifadhi sisi daima, utakuwa unatukinga na hatari zote, na utakuwa unatuweka huru dhidi ya mabaya yote.

Oh, laiti watu wote wangalijua nini maana halisi ya kuishi katika Utashi wa Mungu!

Wote wangekuwa wanapania kuupata na kuishi ndani yake na hapo mabaya yote yangekoma mara moja na pale pale!

Hayo ndiyo matashi yangu mema ya Mwaka mpya kwako. Ya kwamba uweze kuishi daima katika Utashi wa Mungu na kwamba Yesu akufanye wewe uwe mmisionari wa Utashi wa Mungu.

Uniwie radhi kwa maneno yangu hayo, ambayo labda huenda nikawa nimekosea katika kukueleza. Kwa mara nyingine napenda sana nirudie shukrani zangu.

Na sasa napenda nikuage nikikukabidhi ndani ya bahari ya Utashi wa kimungu, katika mikono ya Yesu, na ndani ya bushuti la Mama Malkia wa mbinguni.

Ninabusu shavu lako la kulia, na nikipiga magoti, nakuomba baraka yako ya kibaba. Ndimi.

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu.

Corato, 10 Januari, 1944
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 57
Kwa Mama Cecilia, wa Oria

In Voluntate Dei! [Katika Utashi wa Mungu!]

Mama yangu mwema na Mheshimiwa sana Mama,

Hapa napenda kujibu barua yako ya upendo sana. Ni mshangao na furaha ilioje kwangu kukusikia ukinieleza kuwa katika jamii sasa kunatawala amani na utiifu! Kama kuna amani, maana yake kuna Mungu! Watoto wake ni kama sasa wameokwa katika amani. Kwa hiyo hao wote ni vyombo vya amani, yaani ni watu wa kueneza amani kwa wengine. Maneno yao na namna ya mwenendo wao havitaleta kadhia, maudhi na uchukivu, bali huwa ni maneno na matendo yaliyopakwa mafuta ya uponyaji yenye kuleta amani, yenye kunogesha mioyo ya wale walioelemewa na uchungu zaidi. Katika jamii kama hiyo wale wanaokuwa wachokozi na wakorofi watajionja mara wamepoteza mapembe yao na wanapumbazwa mbele ya mtu yule aliye mtulivu na mwenye roho ya amani. Na unajua Mama yangu, kuwa amani, ni ishara tosha kuwa mahali hapo ni Utashi wa Mungu ndio unatawala, au kama uhai, au walau kama fadhila na nguvu. Wakati Utashi wa Mungu unakwenda kutawala ndani ya mtu fulani, kwanza kabisa hutuma ujumbe wake wa amani. Maana yake, mara nyingi huanza kwa tendo la kufumbia macho mambo ya vineno vineno, magomvigomvi, uvivuuvivu na vimakosamakosa ili kusudi tusipoteze amani wala muda. Na hivyo FIAT ya Kimungu hupata wasaa wa kutengeneza njia ndani ya roho yetu na huanza kujenga pale kiti chake cha ikulu na uhai wake, na hatimaye hueneza hapo himaya yake. Oh, ni jinsi gani ningependelea kama wewe mama yangu uliye mbali unifurahishe kwa jambo hili, yaani, wewe uwe ni tendo moja tu la Utashi wa Mungu na uwe ni chombo cha kupeleka huo Utashi wa Mungu kwa watoto wako wote........ Hapo sadaka yangu ya kumwacha mama abaki mbali nami, na sadaka ya kumkosa hapa, itapunguza machungu yake, kwani nitakuwa nikifikiria kuwa mama yangu yupo katika utume maalum wa kuwasaidia watu waujue Utashi wa Mungu. Na mimi, toka hapa nilipo, nitakuwa nasali, nitakuwa namsindikiza, na nitakuwa ninasimama dirishani kuchungulia ili niyaone matunda ya utume huo wa mbinguni. Kwa sababu hiyo, wakati barua zako zinapoigusa tu FIAT kwa ajili yangu mimi, mimi hapo hapo najisikia kushituka kwa furaha katika moyo wangu, na hapo ninasema: “Nitamwacha Mama abaki bado mbali nami, kwani ananifaa walau kwa ajili ya Utashi wa Mungu”.

Ebu sasa tuzungumzie mambo yetu. Nilikuwa nimekutumia zile anuani 23. Nasadiki ulizipata na utakuwa umewaandikia na kuwatumia tayari. Nilikuwa nimekutumia pia maandishi mengine kwa ajili ya matangazo ya usambazaji. Kama utakuwa unahitaji bado matangazo mengine, nieleze nami nitakutumia.

Ebu sikiliza mama yangu, ninataka nikufundishe ukorofi mtakatifu: Kwa kila ‘Ilani ya Malkia wa Mbingu’ na kwa kila Kitabu utakachokituma kwa mtu, uwe unamwambia huyu Bibi wa mbinguni kuwa unamtuma na kumwagiza akuletee zawadi ile kuu ya Utashi wa Mungu. Kwa njia hiyo, kila ‘Ilani’, kila Kitabu, vitakuwa ni rehani ya ziada utakayokuwa unaikabidhi katika mikono yake ya kimama, siyo kwa ajili ya wewe mwenyewe tu, bali hata kwa yeye yule uliyempelekea Kitabu na hiyo Ilani. Na yeye Malkia Mwenye Mamlaka, atakapokuwa anatazama na kuona rehani nyingi vile mikononi mwake, atajionja amefungwa na anadaiwa kwa lazima. Basi atakupatia kile ambacho Yeye mwenyewe hupenda kukupatia, yaani atakupatia Utashi wa Mungu kama uhai.

(.....) Jamii yangu yote ya hapa inakusalimu, Padre Benedetto anakubariki kwa moyo wote na mimi, nikikuacha umechukuliwa na Utashi wa Mungu, ninakubusu kwa shavu la kulia na ninasema,

Ni wako katika upendo kabisa,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 79
Kwa Padre Ludwig Beda, O.S.B.,
Kloster Andesch, Germany
30 Aprili, 1939

In Voluntate Dei

Mheshimiwa sana Padre,

Yesu anakuambia ‘Asante sana’ kwa ukarimu wako katika kuniandikia barua. Ni faraja ilioje uliyoleta katika roho yangu duni na kwa Padre wangu mwungamishi Don Benedetto! Sisi sote tumekuwa katika kipindi kigumu sana. Yesu Mwenyewe alilia kwa uchungu na ndani yangu moyo unapasuka ninapomwangalia akilia. Ilikuwa ni alama kubwa ya upendo kutufunulia kile ambacho Mama Malkia wa mbinguni alikuwa akianza kutuletea ili kutuonyesha jinsi anavyotupenda na jinsi alivyotamani kabisa moyoni mwake kutufundisha sisi namna ya kuishi katika Utashi wa Mungu, pia kutufundisha namna ya kukua na kukomaa ndani yake, na jinsi alivyokuwa anataka kutulisha kwa chakula cha FIAT ya kimungu.

Hapa Italia, wakati kilipotoka kitabu kile ‘Malkia wa Mbingu Katika Ufalme wa Utashi wa Mungu’, ndipo huyu Mama mwema alipochukua hatua ya kwanza ya kutuwezesha kufahamu jinsi anavyotupenda, kiasi cha kutuingiza na kutuchukua sisi tumboni mwake, ili toka pale atupatie kile kitu cha manufaa ambacho yeye ndiye anayekibeba. Kwa bahati mbaya lakini, njama za maadui wa kitabu chake hicho walizuia hatua hiyo isiendelee kutekelezwa. Yeye mwenyewe akarudishwa na kupelekwa tena katika pande zile za juu mbinguni. Toka pale juu, kwa subira isiyoshindikana, yupo anangojea kwanza yafike mabadiliko ya nyakati, mabadiliko ya watu na mabadiliko ya mazingira, ili hatimaye mambo yake yaweze kuchukua mkondo wake na ili aweze kutoa na kutupatia kitu kile ambacho hata sasa kinadharauliwa na watu.

Mheshimiwa Padre, ni mapenzi na uamuzi wa Mungu kwamba Ufalme wake ufike hapa duniani; kwa hiyo ni uhakika kabisa kwamba utafika, iwe kwa njia ya upendo au kwa njia ya adhabu. Vinginevyo, uumbwa utakuwa ni kazi itakayokuwa imekosa kupata taji lake. Mbele ya viumbe vingine vyenye nguvu ya kujiongeza na kujizidisha, Mungu angeonekana kana kwamba hana uwezo wowote kama Utashi Wake wa kimungu ungeshindwa tu kuzindua Uhai wake Mwenyewe ndani ya roho zetu sisi. Hapana. Hilo haliwezekani kamwe. Tuna uhakika kwamba Ufalme wa Utashi Wake utafika kwa vyovyote...
Bikira Maria Katika Ufalme Wa Utashi Mungu ⬇️⬇️⬇️ - A5 format

Imetolewa katika Sikukuu ya Huruma ya Mungu, Jumapili tarehe 11 Aprili 2021

SALAMU MARIA!