Utashi wa Mungu na Upendo wa Mungu
21 subscribers
29 photos
26 files
13 links
Maelezo ya Kiswahili
Download Telegram
to view and join the conversation
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 56
Kwa Bw. Vincenzo Messina, Mfungwa katika Gereza la Favignana, Trapani

Fiat

Mpendwa sana Ndugu yangu katika Yesu Kristu,

Nimefurahishwa sana na ombi lako la kupata Kitabu cha Malkia wa Mbingu. Nimekuwa nawaza kwamba Mama wa mbinguni anakuja hata katika gereza kufanya ziara yake ya kuwatembelea kama Mama, kama Mwalimu, na kama Mfariji na pia kwa ajili ya kuwasindikizeni na kukesha pamoja nanyi na hata kwa ajili ya kuwafundisheni namna ya kuishi Utashi wa Mungu na namna ya kuujenga Ufalme wa Utashi wa Mungu hata hapo gerezani.

Kwa hiyo ndugu yangu, jipe moyo, uwe na imani na matumaini, kwani unaye Mama wa mbinguni ambaye anakupenda mno, ambaye hatakuacha kamwe peke, na kama utamsikiliza, atageuza hiyo gereza kuwa kikanisa cha hija takatifu. Na kama udhaifu wa kibinadamu umekupeleka gerezani, yule Malkia Mwenye mamlaka anakuja kwa nguvu ya Utashi wa Mungu ili akutoe na kukuongoza kwenda mbinguni na kufanya siku zako ziwe na maumivu yaliyopunguka. Yaani, maumivu yako, kuachika kwako, kukosa mahitaji, upweke wako, yeye Mama atavibadilisha viwe ni hati za uhuru na ushindi wa milele. Atakusaidia uonje amani ambayo huwa huwezi kuipata na kuifaidi hata unapokuwa duniani. Utashi wa Mungu utakubadili wewe na utaanza kuonja uhai mpya ambao atakuletea yule Mama wa mbinguni.

Ni vema pia ujue kuwa hata mimi hapa ni dada yako mfungwa wa gerezani. Tangu zaidi ya miaka hamsini FIAT Kuu imenifunga mimi hapa ndani ya kitanda. Hata hivyo ninaridhika na ninafurahi. Lakini je ni nani anayenifanya nifurahi? Ni Utashi wa Mungu ambao najitahidi kuutekeleza daima. Hata wewe unaweza ukawa na furaha endapo utatekeleza Utashi wa Mungu. Oh, ni jinsi gani utakavyobadilika huo uchungu wako! Utaanza kuonja nguvu ya kweli ya kimungu, ambayo itarahisisha sana hali yako hiyo ya mateso.
Kamwe usiache kusali Rosari kwa Mama wa mbinguni, na kama utaweza, basi uwe wewe ndio mmisionari hapo gerezani kwa kujitahidi kuwafahamisha wenzako kwamba Malkia wa mbinguni anataka kuwatembelea ninyi wafungwa wote ili awapatieni ninyi nyote zawadi ya Utashi wa Mungu. Endapo mngehitaji nakala nyingine ya Kitabu, na iwapo ninyi hamtaweza kulipa fedha yake, mimi nipo tayari kuwatumia nakala hizo bila kudai malipo yeyote.

Nakukabidhi ndani ya bushuti la Mama yetu wa mbinguni ili uwe unasikiliza mafundisho yake ya Mbingu.

Na kwa salamu elfu na elfu nasema ni mimi dada yako mpendwa kabisa,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 03
Kwa Mama Mkubwa, Sr Maddalena del Moro, wa Santa Chiara, Ravello
20 Novemba, 1917

Y.M.Y.

Utashi wa Mungu uwafunge sana sana hata msiwe na muda wa kuwaza juu yenu ninyi wenyewe.

Dada yangu katika Yesu Kristo,

Kwa mistari hii michache napenda kujibu barua yako. Mimi naamini kuwa kinachosababisha yote hayo unayonielezea ni kukosekana kwa muungano na Yesu katika mambo yako yote. Adui anakukuta ukiwa peke bila Yesu, na ndipo anatenda kazi yake chafu, anakusumbua, anakuondolea amani ya moyoni ambayo ni ya lazima kwa ajili ya kumpumzisha Yesu Mteseka. Huyu adui angekukuta upo daima na Yesu, hakika angetoroka na kukimbia ili asiteseke na ule uwepo mwabudiwa wa Yesu. Hiyo ndiyo tiba dhidi ya maovu yote: Kaa na Yesu ndani yako daima, iwe katika mambo ya kiroho, kama vile pia katika mambo ya kimwili. Na Yesu atachukua jukumu la kukuletea amani na kukusaidia kutekeleza wajibu zako. Yaani Yesu ndiye atatenda ndani yako. Kila jambo linalokutesa ulitolee kwa Yesu ili aliinue na alilipie fidia. Tolea kwa Yesu hata ubaridi unaoupata. Kwa namna hiyo utakuwa na wasaa zaidi wa kuambatana na Yesu Mteswa. Kama utakuwa na Yesu, utajisahau wewe mwenyewe na utakuwa unamkumbuka daima Yesu tu. Naye Yesu atashughulikia matatizo yako yote........ Ah, ndiyo kweli, umpende zaidi na zaidi. Ni muungano na Yesu peke yake, ndio utafanya ijitokeze chemchemi mpya ya pendo linalokua na kuongezeka; kwani wakati unapokuwa na Yesu, utakuwa unampenda, na vinginevyo utakuwa unajipenda wewe mwenyewe na maovu yako tu. Ikiwa hivyo, ni picha mbaya gani utakayoleta mbele ya Yesu? Si kweli hivyo?

Nenda umwambie Mkubwa wako mwema kuwa utakuwa unatii katika mambo yote kwani yule anayetii hakosi, na Yesu Mbarikiwa atajaziliza kile kinachokosekana katika mahitaji yako. Na halafu ujue, pale Yesu anapoona anapendwa, huwa anasahau makosa yetu, na sisi tusingependa kupoteza akili yetu kwa kumkumbusha tena. Yesu anataka pawepo mapatano na maelewano kati yenu ili Yeye aendelee kuwa kati yenu.
Ninakuomba sana sala zako.

Binti mdogo wa Utashi wa Mungu

Corato, 20 Novemba 20, 1917
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 64
Kwa Bi. Mazari, wa Bari – 3 Decemba, 1937

In Voluntate Dei !

Binti yangu mwema katika Utashi wa Mungu,

Napenda kukushukuru kwa upenzi wako mkubwa kwangu na kwa kunihangaikia mie nisiyestahili. Mbingu, Mpendwa Yesu, Mama na Malkia, wao hao wakulipe kwa yote hayo. Yaani, na mimi kwa upande wangu, nitasali ili wao wakupe na kukuvalisha lile vazi la kifalme la Utashi wa Mungu na wakufunike na kukupasha joto kwa bushuti la upendo. Hata hivyo, wewe ni budi ufike na ujilete ili upate kulipokea na kulivaa vazi hilo la kifalme. Vazi hilo litakutofautisha na wengine na litakufanya utambulikane kama binti anayependelewa na Utashi wa Mungu; na Yesu pamoja na Mama, kwa mikono yao ya kimungu, watakufunika wenyewe kwa lile bushuti angavu la upendo. Wala usidhani kuwa ni vigumu sana kupata bahati kubwa hiyo. Kwa kweli ni rahisi kabisa, ili mradi tu wewe utapenda na kuazimia kwa dhati kabisa kuishi katika Utashi wa Mungu na kugeuza kila kitu utendacho kiwe ni Utashi wa Mungu. Huyu Yesu mpenzi na Mama Malkia Mtakatifu sana, wao watakuwa tayari kukusaidia. Watakuja na kuwa daima ndani na nje yako ili wakuongoze, ili wawe nuru yako na nguvu yako. Na endapo wataona udhaifu fulani ndani yako, na siyo udhaifu wa utashi, ni wao watakuongezea nguvu za ziada pale ambapo wewe unashindwa kufanikisha. Je unataka kufahamu zaidi juu ya hilo? Kwa ajili ya mtu yeyote yule anayetaka kuishi katika Utashi wa Mungu, Mama Malkia amekwisha kukubaliana na Mwanaye wa kimungu kuwa atamsaidia mtu huyo na kumwendeleza na kumkuza kwa pendo lile alilotumia kumsaidia kumlea, kumwendeleza na kumkuza Mwanae Yesu.. Kwa minajili hiyo kinachotakiwa ni uamuzi na azimio lako. Mambo mengine yatakuja yenyewe......

Haya basi, ebu kazana. Usikate tamaa kutokana na matatizo mbalimbali na mazingira ya maisha. Hayo yote ni hatua za kupitia tunapozidi kupanda kwenda juu zaidi katika Utashi wa Mungu. Na kwa namna ya pekee, katika mazingira ya mateso, Mpenzi wetu Yesu huwa anakuja kutusaidia ili tupande juu zaidi, na ili kutuwezesha tujipatie ushindi mzuri zaidi ambao siyo wa kibinadamu, bali ni ushindi wa kimungu ulio na thamani isiyo na mipaka. Oh, ningependa jinsi gani kusikia kuwa unadumu daima katika Utashi wa Mungu!

(.......) Nimekuwa ninasali daima kwa ajili ya nia na shida zako, kama vile kwa ajili ya Carmella mwema. Kwani tunajua ni mabusu na makumbatio mangapi atakayoyatoa Bwana kwa yeye mgonjwa anayeteseka na kwako wewe unayemwangalia mgonjwa akiteseka. Unajua mara nyingi ni afadhali mtu kuteseka mwenyewe kuliko kumwangalia mtu mwingine akiteswa. Kwa hiyo basi hebu badilishaneni kupeana hayo makumbatio na mabusu ya Yesu na yale ya kwenu na mwambieni Yesu hivi: “Yesu, ebu chukua utashi wetu na wewe utupatie Utashi wa kwako”. Yeye anapenda kuutoa Uhai wake na anapenda uwe unatafutwa na kutamaniwa (.......)

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu

Corato, 3 Decemba, 1937
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n 20.
Kwa Wakuu Wa Mashirika Mapadre Rogazionisti Na Masista Figlie del Divino Zelo
24 Februari, 1932

Fiat

Waheshimiwa Baba Mkuu na Mama Mkuu,

Mfariji wa kimungu, Yesu, awatulizeni na awapake mafuta ya uponyaji juu ya jeraha kubwa na la kina lililotoboka katika mioyo yenu kutokana na kifo cha mpendwa wetu M. Gesuina. Lakini, si kweli kwamba mmempoteza. Yeye ameaga akienda mbinguni. Ninyi mmejipatia sasa yule atakayekuwa mlinzi na mpatanishi wenu mbele ya Mungu kama alivyokuwa hapa duniani. Kule mbele ya safari ataendelea kutenda ile kazi ya upatanishi, hasa kwa vile ameondoka katika kipindi ambapo ninyi wapendwa viongozi pamoja na jamii nzima ya watawa mpo katika majonzi, kwani mnapenda kupata ile amani mnayoitamani sana. Roho yake nzuri, yenye utulivu, upole na amani, baada ya kuwa imekamilisha safari yake, haikuwa tena na kitu cha kufanya kwa ajili ya dunia. Mbingu ikawa inamwita kurudi kwake ilipotambua kuwa safari yake kama kiumbe imekamilika na kwa hiyo haikuwa na muda tena wa kumwacha asubiri mbali.

Kwa sababu hiyo, kwa upande wetu hakuna neno lingine la kusema isipokuwa “Asante kwa Mungu” kwa ajili ya M. Gesuina ambaye amebahatika na kusema FIAT kwa ajili yetu sisi wenyewe ambao tumempoteza. Na hiyo FIAT ndiyo itaturudishia kila kitu. Basi, uchungu na pengo tulilopata visitukatishe tamaa. Hivyo vyote ni pepo zinazoashira ujio wa neema mbalimbali, ujio wa mwanga, ujio wa misaada itakayotushangaza zaidi. Hapa pamoja nasi, tunao Utashi wa Mungu wenye maweza yote. Kwa hiyo, hamna kitu cha kuogopa hapa. Huo Utashi wa Mungu ndio utabadili mioyo na kutengeneza watu wanaotupenda. Yesu Mbarikiwa na Mama yetu wa mbinguni watakuwa pamoja nanyi ili kuwaongozeni na kuwasaidieni mambo yote yaende kadiri ya Utashi Wao mwabudiwa.

Mama yangu mpendwa na Mheshimiwa Padre, mimi nawaoneeni huruma sana. Najua kuwa msiba huu umeleta ufa katika moyo wenu wa kimama na wa kibaba. Kwa hiyo, ninamwomba Yesu awajalieni nguvu, Yeye aje na ajiweke Yeye badala ya moyo wenu, ili uchungu wenu upunguke kabisa na Yeye asimamie na kuongoza mambo yenu yote.

Nawaombeni sala zenu. Na sasa ninapowaageni katika amani ya Utashi Mkuu napenda kubusu mkono wako Mama. Nabusu na mkono wako Padre huku nikikuomba na Baraka yako ya kibaba.

Ni mimi mtumishi wenu,

Luisa Piccarreta

Corato, 24 Februari, 1932
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 77
Kwa Mkuu Wa Ngome (Duchess) Bi. M. Pignatelli, wa Pisa
25 Aprili, 1939

In Voluntate Dei!

Mheshimiwa sana katika Utashi wa Mungu,

Asante sana kwa barua yako iliyo muhimu sana na asante kwa makala ya Mama Mkubwa Sr. Landa ambayo umenitumia. Mbingu ikulipe katika Utashi wa Mungu, ili maisha yako yote yasiwe kitu tofauti sipokuwa yawe ni tendo moja endelevu la Utashi wa Mungu. Mpendwa Mama Mtawala Ngome, moyoni mwetu sisi, ni neno muhimu sana kuweza kuishi Utashi wa Mungu. Mambo mengine yote, hata yakiwa ni makubwa jinsi gani, yanabaki kuwa ni mithili ya vitone vingi vya maji mbele ya bahari. Zaidi zaidi ni kuwa, sisi tunapoishi katika Utashi Wake, Yesu mpenzi wetu ataweza kuziona hatua zake za kimungu ndani yetu, ataona ujimudu wake, ataona Pendo lake na ataona nafsi yetu yote imeongoka na kugeuka kuwa ni kitu cha kimungu, ambacho Yeye Yesu Mtamu, anaweza akakitumia kwa ajili ya kutengenezea Uhai Wake na pia akakitumia kwa ajili ya kukuzia na kuulisha huo Uhai Wake ndani yetu.

Vitu vingine vyote, hata vikiwa ni vizuri na vya kupendeza kiasi gani, huweza vikatumika kwa ajili ya kutengenezea kazi zake, lakini ni peke yake tu maisha ndani ya Utashi wa Mungu, ndiyo yanaweza kutengeneza Uhai Wake. Ona tofauti iliyopo kati ya kazi zake na Uhai Wake! Mara tu tunapoamua kutekeleza kitendo chetu katika Utashi Wake, Mbingu huteremkia juu ya kichwa chetu, Pendo la kimungu huchukua na kushika mara kiti chake cha kwanza ndani yetu. Na hapo sisi hatuwi tena ni sisi wenye kupenda au wenye kutenda kitu, bali sasa huwa ni Pendo tu la kimungu ndilo linalopenda na linalotenda chochote ndani yetu.

Kwa minajili hiyo, sisi tunakuwa sasa ni wabeba-FIAT, ambayo ndiyo inaanza kutenda mambo yake makuu ndani yetu, mambo ambayo yanawastaajabisha hata wenyewe Malaika. Kwa hiyo, hata wewe uitolee hiyo ngome yako na kuiweka katika Utashi wa Mungu, ili huo Utashi wa Mungu uweze kuingia na kutawala ndani ya watu wote watakaojitokeza na kuingia hapo.

Mpendwa wangu Mama Mtawala wa Ngome, kwa bahati mbaya, ni ukweli kwamba tumeadhibiwa kutokana na kitendo chetu cha kuwafahamisha watu, ili angalau wapate vitone tu vya ufahamu juu ya kuishi katika Utashi wa Mungu. Tumeadhibiwa na kupigwa bila kusamehewa, tumeadhibiwa kwa maumivu na mateso makali mno kiasi kwamba, isingekuwa ni kwa msaada wa FIAT, ingetakiwa tuwe tayari tumekufa kutokana na maumivu hayo makubwa yanayotutesa sana. Kitulizo pekee tunachopata ni hiki kwamba, hawawezi wakafikia kutuondolea Utashi wa Mungu. Basi nawe usali ili angalau watuache katika amani, na ili mateso hayo yote yajae na kufurika kwa ajili ya kuleta ushindi wa Utashi wa Mungu. Utashi wa Mungu peke yake uwe ndilo kimbilio letu, uwe ndiyo mafuta ya kuponyesha maumivu yetu, uwe ndiyo maficho yetu wakati wanapotudhulumu, ili wasiweze kutuona.

Padre Benedetto anakubariki, na mimi ninakukabidhi ndani na katikati ya Utashi wa Mungu nikisema, ni mimi,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu

Corato, 25 Aprili, 1939
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 132
Kwa Federico Abresch
15 Januari, 1945


Mwanangu katika Utashi Wa Mungu,

Napenda leo kujibu barua yako ya upendo sana, na ninamwomba Yesu azidi kukujalia neema zaidi na nuru zaidi ili uwasaidie watu wote waelewe namna ya kuishi katika Utashi wa Mungu. Oh, ni jinsi gani Yesu anavyotamani, hata kufikia kutoa machozi, kwa vile anapenda sana sisi tuufahamu Utashi Mtakatifu wa Mungu na kwa vile anataka Utashi huo wa Mungu utawale na utamalaki duniani pote! Ni kwa vile ni kauli ya Utatu Mtakatifu Mtukufu kwamba Utashi wa Mungu ufanyike duniani kama vile mbinguni. Kama vile kauli ya Mungu ilivyotolewa juu ya uumbwa na juu ya ukombozi, kadhalika kauli imetolewa juu ya Ufalme wa Utashi wa Mungu juu ya dunia. Na kwa hiyo Utatu utatumia mbinu zote, utamchukua mwanadamu toka pande zote za dunia: Kwa kutumia mapigo makali na hata kwa kutumia miujiza ya kutisha, hadi hilo lipate kutimia. Hilo litafikia ile hatua kwamba atakayekuwa ni sadaka ya kwanza atakuwa ni Yesu: Yeye atajiweka kuwa kichwa na utangulizi wa matendo yetu yote ili kusudi watu wote wakimbilie katika bahari ya Utashi wa Mungu..........

Na kama Yesu anatuadhibu, ni tu kwa hoja hii kwamba wanadamu, mathalan watu wa maisha ya wakfu, badala ya kumsikiliza na kumfuata Yesu kwa kuvutwa na upendo kama Yeye alivyotamani, wao lakini wameamua kumjia na kumfuata kwa njia ya adhabu...... Masikini Yesu! Ni jinsi gani anavyoteseka! Ni kwa jinsi gani anavyotamani na anavyolia! Ni vile wanadamu hawamwombi wala hawamsihii kamwe awapatie zawadi ile ya kuishi katika Utashi wa Mungu. Na pale anapofanikiwa, anamchukua mkononi mwake, anasherehekea na anajiona kuwa ni mfalme mshindi ambaye, baada ya miaka zaidi ya elfu sita ya kupambana, kupata majeraha na kufanikiwa kupata ushindi wa kwanza, na anaufurahia ushindi huo kwa kualika Mbingu yote ije kusherehekea huo ushindi wake wa kwanza. Pindi anaposherehekea anatoa na kumwachia mwanadamu Utakatifu wake, Pendo lake, Mwanga wake, na neema zake na anampatia pia na haki juu ya Makao yake ya mbinguni........ Kwa hoja hiyo, mwanadamu huyo, hata pindi yupo bado duniani yeye atakuwa tayari ni mmiliki wa Makao ya mbinguni na ataweza kujisemea hivi moyoni mwake: “Kile kinachotendeka mbinguni, ndicho na mimi nakitenda hapa duniani. Yaani, Utatu unafurahia na kujiburudisha, na mimi hapa duniani naendelea kuvuna watu zaidi na kupata ushindi mpya unaozidi kuleta furaha zaidi kule mbinguni.

Basi, uwaeleze wote kwamba, hakuna jambo kuu zaidi na hakuna tukio la kushangiliwa kwa shamrashamra zaidi, kuliko hili la kuishi katika Utashi wa Mungu: Sisi tunajitoa na tunajiweka kabisa mikononi mwa Mungu na Mungu anajiweka kuwa tayari kwa ajili yetu kiasi kwamba anatuwezesha kuwatengeneza ma-Yesu wengi kulingana na idadi ya vitendo tunavyotekeleza katika Utashi Wake Mtakatifu. Mabahari ya Utashi wa kimungu hayajafahamika bado. Kama wanadamu wangefikia kuyafahamu mabahari hayo, hakika wangejitosa na kujitumbukiza katika bahari ya Utashi wa Mungu ili tokea hapo wajipatie uhai usioweza kukoma. Kwa hiyo tuombe na tusubiri: Yesu anashikilia karne zote katika mamlaka yake. Kile ambacho hatekelezi leo hii, atakuja kukitekeleza kesho, kwa vile kwa leo hii akili za watu zimepofuka bado. Kesho kutapatikana macho yatakayokuwa na uwezo na nguvu ya kuweza kuhimili ule mwanga wa Utashi wa Mungu na Yesu atatekeleza kile ambacho hajafaulu kutekeleza bado leo hii.

Ninawasalimuni na ninawakabidhi ninyi nyote katika bahari kuu ya Utashi wa Mungu.

Binti mdogo wa Utashi wa Mungu.

Corato, 15 Januari, 1945
Luisa akiwa pamoja na Masista wa Shirika la Figlie del Divino Zelo
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 92
Kwa Bi Maria De Regibus, wa Torino

Fiat

Binti yangu Mpenzi katika Utashi wa Mungu,

Asante sana kwa matashi yako mema katika Utashi wa Mungu. Ukimya wako wa muda mrefu haukunishangaza kwa lolote kwani tunajua kuwa tunapokuwa tumekabiliwa na hali ngumu ya kunyanyaswa, kuhinishwa na kunyenyekeshwa, watu wote wanatutoroka na wengine hata wanajutia kwa nini walifahamiana na sisi. Hilo lilikwisha kutokea hata kwa Yesu. Hata hivyo, Mapenzi ya Mungu yafanyike daima. Ni Utashi wa Mungu tu ndio ulio mwaminifu, yaani unatufungulia na kutupanulia mikono yake ili kutupatia mahali hakika na salama pa kukimbilia, na ili ukatulishe kwa Pendo lake na ili Mungu Baba atuambie kila mmoja wetu: “Binti yangu, usiogope. Ebu unipe matendo yako yote kwa ajili ya kuweza kukuzia na kulishia Uhai Wangu ndani yako. Na sasa ujue kwamba, kwa mshangao na fadhaa ya wale ambao walichukia kuujua Utashi Wangu, huo Utashi wa Mungu utatawala na utajenga Ufalme wake hapa duniani. Mimi ni Mungu Mwenye enzi na nitatumia kila njia ili kumpata binadamu na kumwezesha afufuke ndani ya Utashi Wangu”.

Binti mpendwa, mimi ninasikitika juu ya Padre Beda. Ni kwa nini makala nilizoandika hazikuweza kufika kule Roma? Ni nani aliyezizuia? Wakati mimi ninapofahamu kutokana na taarifa za kuaminika kwamba kule katika Ofisi Takatifu ya Kitume kuliwafikia maombi ya watu wa sehemu zote kutaka makala hizo nilizoandika zitolewe hadharani kwa umma........Mwishowe lakini unaona kwamba Bwana anataka atende kila kitu Yeye, kama siyo leo hii, basi atatenda hivyo kesho. Kwa hiyo basi, nakushauri sana wewe usitoke kamwe nje ya FIAT kama unapenda kuwa mmoja wa wale watu walioitwa kuishi ndani ya Utashi wa Mungu na kama unataka kuendelea kushikilia kile kiti chako cha heshima. Sasa ninakuagiza ushauri wangu wa kujitahidi kumfanya Mtoto Yesu aliye Kichanga rohoni mwako, aendelee kukua, nakutakia uishi pamoja Naye, uwe unamtunza daima na kumlinda ndani yako, ukimwangalia daima ili uweze kutekeleza kile anachotaka Yeye. Uwe ukimwambia: “Nataka kuwa nakala yako Wewe”.

Nakuletea salamu na matashi mema toka kwa dada. Nikikuaga, napenda kusema ni mimi,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu.
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 31
Kwa Bi. Mazari, wa Bari

In Voluntate Dei !

Binti yangu mwema katika Utashi wa Mungu,

Mbingu ikulipe wewe kwa sadaka unazotoa katika kueneza na kuelezea kile kitabu cha Malkia wa Mbingu. Nafikiri kuwa Mama wa Mbinguni hatakoma kukuambia ‘asante, asante, binti yangu’, na anaendelea kukuandalia neema nyingine nyingi kama vile ile neema kubwa ya kukuwezesha wewe uwe daima mbadala wa Mwanae Mpenzi ili kusudi wewe uwe ni mchukuaji na mpelekaji wa neema mbalimbali, uwe mleta umoja katika familia na uwe mletaji wa misaada ya mahitaji mbalimbali.

Binti yangu, tunapotekeleza Utashi wa Mungu sisi tunapata kuwa ni watoto wa kweli wa Mama Mkuu na tunageuzwa kuwa tabernakuli ambamo Yesu hujenga makao yake. Na kwa hiyo kila kitu tunachotenda hugeuka kuwa kitakatifu, kila tufanyacho hugeuka kuwa ni sala; hata mambo yale ambayo kwa yenyewe hayana lengo hilo kabisa. Hata mambo yale ya kawaida kabisa na ya kimaumbile tu, ambayo ni mahitaji ya maisha; pale tunapotekeleza Utashi wa Mungu hayo hugeuka kuwa sala, hugeuka kuwa ni uabudu, na ni upendo kwa Yesu wetu Mtamu. Ni kwa hoja kwamba, tunapotekeleza Utashi Wake, kila kitu tutendacho kinakuwa ni kitakatifu, na kila kitu ni pendo, hata nafsi yetu nzima huwa ni takatifu.

Sasa, kuhusu yale yote mnayonieleza juu ya mtoto wenu, nionavyo mimi katika akili yangu dhaifu, inaelekea kuwa yupo bado mdogo mno. Mwacheni akomae kwanza ili ajipatie mang’amuzi zaidi ya maisha. Ndoa ni msalaba, na kumwingiza katika msalaba wakati ni mdogo vile, nionavyo mimi, siyo jambo jema. Mnajua fika kuwa kila kitu kimeandikwa kule mbinguni. Kwa hiyo, endapo jambo hilo limepangwa na Mungu, Bwana Wetu kwa kipindi kifaacho na anachoona Yeye, atamtunza na kumhifadhi huyo msichana kwa ajili ya mtoto wenu mvulana. Halafu, jambo la kuzingatia zaidi ni kuwa familia ziwe tulivu na zenye amani, kwani ni amani ndiyo iletayo furaha katika familia na wala siyo fedha. Kuna matajiri wangapi ambao wanakosa furaha kwa sababu amani haitawali katika familia zao. Basi na ninyi zingatieni sana hilo. Tena, kama mwanamke anatukuka zaidi ya mume wake, atakuwa anapenda kumtawala huyo mume na kumfanya mtumwa wake duni..........Na mambo mengine jaribuni kuyapangilia vizuri.

Napenda kukuhakikishia kuwa namwombea mama yako mpenzi ambaye ni shahidi wa kweli. Huenda Bwana atamsaidia atimize siku zake za tohorani pindi yupo bado katika maisha yake haya. Oh, je isingewezekana wewe mwenyewe kumchukua akae nawe? Ni baraka kubwa ilioje ungeipata? Ebu uwafahamishe na kuwaonyesha hao kuwa kuna mikosi anayoleta Bwana juu ya wale wasiowaheshimu na wasiowapenda wazazi wao.

Mimi ninaomba sana sala zako; nami kwa upande wangu nitakuwa nakuombea kwa moyo wote. Sitasahau kamwe juu ya mambo yale yote unayofanya kwa ajili ya Mama mpendwa wa mbinguni. Na sasa ninakukabidhi katika Utashi wa Mungu ili Mungu akulinde, akusaidie na kukutegemeza.

Ninakusalimu sana, ni mimi,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
🕊"The Divine Will: on earth as it is in Heaven"🕊

Don Pierpaolo Maria Cilla

The Url to access directly to Radio Maria Italy on air👇

https://dreamsiteradioplayer.it/plit/radiomariait/

Below the link to listen the previous episodes (in Italian) by Father Pierpaolo Cilla "The Divine Will: on earth as it is in Heaven"👇

https://radiomaria.it/trasmissioni/la-divina-volonta-come-in-cielo-cosi-in-terra/
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 41
Kwa Federico Abresch wa Bologna

In Voluntate Dei! - Fiat

Mheshimiwa sana katika Bwana,

Huwezi ukaelewa furaha na raha ninayoonja ninaposikia mtu anataka kuishi katika Utashi wa Mungu, kwani huo ni ushindi anaopata Yesu. Na pindi Yeye anaposhinda utashi wetu, sisi nasi tunashinda Utashi wake. Katika Ufalme wa Utashi wa Mungu, hakuna anayeshindwa, bali tunakuwa ni washindi wote, yaani Mungu na mwanadamu.

Mashaka yenu yananishangaza. Inakuwaje hamfahamu kuwa Ukombozi ni maandalizi kwa Ufalme wa Utashi wa Mungu? Na Moyo Mtakatifu wa Yesu si kitu kingine tofauti na Ufalme Mkuu wa Utashi wake? Siyo Moyo ndio unaotawala, bali ni Utashi wa Mungu ndio unatawala Moyo wake wa kimungu.

Masikini Moyo, kama usingekuwa na Utashi unaoutawala, usingeweza kuwa mwema kwa lolote. Endapo utashi ni mwema, basi na moyo unakuwa mwema. Kama utashi ni mtakatifu na moyo unakuwa mtakatifu. Kama utashi wetu unaupisha na kutoa nafasi kwa Utashi wa Mungu na kuruhusu usimike kiti chake cha utawala ndani ya utashi wetu, basi moyo, kwa neema, unajipatia maweza na sifa za kimungu. Kwa hiyo basi, iwe katika mpangilio wa kimungu, iwe katika ule wa kibinadamu, huwa daima ni utashi ambao unashika nafasi ya kwanza, huwa ndio hushika kitendo cha kwanza kabisa na huwa ndio unaoshika utawala wake. Moyo na vitu vingine vinavyobaki huwa vinawekwa katika mpangilio wa pili unaofuata.

Kwa hiyo ni upuuzi kusema kuwa Moyo unatawala kama Utashi wa Mungu hautawali. Hizo zaweza kuitwa ni ibada na mazoezi ya uchaji......kama Utashi wa Mungu hautawali, basi hapo hamna Ufalme wowote. Ufalme utakuwa upo mbinguni lakini utakuwa bado haujapata nafasi yoyote duniani. Hata hivyo Kanisa, iliyo ni chombo cha FIAT Kuu na msemaji wake rasmi, huwa anaomba na kusihi Ufalme wa Utashi wa Mungu kupitia Moyo Mtakatifu wa Yesu na kupitia kwa Mama wa mbinguni. Kanisa haliombi hilo kwa maneno tu, bali kwa matendo. Utashi wa Mungu ndiye Mfalme. Moyo wake, majeraha yake, Damu yake azizi, Msalaba wake, Malkia wake Mtamu, hawa wote wanakuwa ndio wahudumu wanaomzunguka Mfalme wakiomba Ufalme wa Utashi wa Mungu ufike ndani ya watu kupitia wao.

Sasa tunapataje kufahamu hilo? Mambo yote ya lazima ni Utashi wa Mungu kwa ajili yetu, yaani mazingira mbalimbali tunamoweza kujikuta. Endapo tunakuwa tumeamua kwa dhati kabisa kuishi katika Utashi wa Mungu, hilo ni jambo linalompendeza Mungu sana sana, kiasi kwamba, hata pakitakiwa miujiza itendeke, Yeye ataifanya, ili mradi kutuzuia tusitende utashi wetu. Kwa upande wetu yatakiwa tu uamuzi wa dhati, yaani kuwa tayari na hiari hata kutoa uhai wetu kwa ajili ya kuishi ndani ya Utashi wa Mungu. Na mpendwa wetu Yesu na Malkia Mtawala Mkuu, wao watachukua jukumu la kuhakikisha kuwa utashi wetu wa kibinadamu hautusaliti. Wao watakuwa ndio walinzi wetu na watatuandalia neema nyingi kabisa zenye kutuzunguka. Na zaidi zaidi, Bwana Wetu hafundishi mambo magumu, na wala haagizi hayo, na wala hayataki hayo. Bali badala yake Yeye, kwa namna ya kushangaza na kupendeza, anarahisisha kitendeke au kitokee kile anachokitaka Yeye toka kwetu. Kwa kweli, kwa kutaka kuturahisishia, Yeye huchukua nafasi yetu, na hutenda pamoja nasi jambo lile analotaka sisi tulitende.

Mie nakuomba sala zako na zile za binti yangu Amelia. Jitahidini kuwa watakatifu. Utashi wa Mungu uwanyoshee mikono yake ili mkue na kukomaa ndani yake. Mambo yote yachukueni kama ni vyombo vinavyowaletea Utashi wa Mungu ili kuwapeni uhai wake, utakatifu wake...... Na hako katoto kenu kadogo, kasaidieni kakue katika utakatifu na kama zawadi ya FIAT. Hatujui pengine Mungu atakuja kulipa matamanio yenu ya kumwona siku moja akiwa mtawa na mtakatifu.

Haya, sasa nawaacheni ninyi nyote katika Utashi wa Mungu. Mkae daima ndani yake. Huku nikitoa heshima mara elfu kwa Baba, kwa Mama na kwa Mwana, nawaageni,

Ni mimi awapendaye sana,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 32.
Kwa Mama Antonietta Savorani, Mjane wa Faenza

Fiat

Binti yangu mwema katika Utashi wa Mungu,

Asante sana kwa kujihusisha na kukitangaza Kitabu cha Malkia wa Mbingu na kile cha Mateso: zoezi hilo siyo tendo lingine bali ni lile tendo la kurudia kumwita Mama wa mbinguni, na Yeye Mfalme wa Mateso ili waje kuwa katikati ya wanadamu ili kutuwezesha sisi kujifunza namna ya kuishi zaidi mbinguni kuliko kuishi duniani. Kwetu sote ingekuwa ni bahati iliyo kubwa kabisa kama tutaweza kuishi katika Utashi wa Mungu. Ndiyo maana, Yesu na Mama yake, yaelekea hawakomi kurudia kusema: “Asante, Asante binti yangu! Ili kukulipa Sisi tutatengeneza Mbingu yetu ndani ya moyo wako. Kwa hiyo tutakuwa tukikaa daima na wewe, uhai wako na uhai wetu vitaunganika kuwa uhai mmoja tu”. Kwa sababu hiyo, kitu ninachokushauri ni kujitahidi kufanana na mema unayopata ya namna hiyo; uwe makini sana kumsikiliza Yesu Mtamu, ambaye huwa anazungumza kwenye moyo wako. Yeye anapenda kukufanya uwe mtakatifu, lakini kwa ajili ya hilo anataka utoe utashi wako na kuuweka mikononi mwake kwa lengo la kutekeleza muujiza wa utakatifu.

Ninakushauri mambo matatu: imara na ukakamavu katika jema, amani inayodumu, na imani ya mwana. Imani itakuwezesha kuishi kama mtoto mdogo mikononi mwa mama yake, na kwa mambo mengine yote yanayohitajika, Yesu na Mama wa mbinguni ndio watayashughulikia. Wao watakuwa wanakujibu kwa matendo: “Wewe fikiria namna ya kuishi kadiri ya Utashi Wetu, na sisi tutakuwa tukiyashughulikia mambo yote kwa ajili yako hata juu ya wokovu wa ndugu zako”. Je mpaka hapo huridhiki!

Utaniambia iwapo wasichana rafiki zako wataweza kuniandikia. Binti yangu, imeniwia ni vigumu kwangu kuweza kuwajibu, na kwa hiyo, nashauri kuwa ni vema kama watajaribu kujisomea Kitabu cha Mama Bikira Maria. Oh, ni mambo mengi mangapi ambayo huyu Mama Mkuu Maria atawaeleza zaidi na kupita yale ambayo wao wanataka kusikia toka kwangu! Halafu kuna kile Kitabu cha Mateso, ambamo Yesu anazungumza ana kwa ana, kati ya moyo wake na moyo wa mwanadamu. Katika toleo hili la tano ninalokutumia mtaona mambo mapya, yakiwa yameongezwa mara mbili zaidi kutokana na “Mada juu ya Utashi wa Mungu”. Someni mada hiyo na hivyo mtaweza kunieleza faida kubwa inayowaletea.

Nawahimizeni ninyi nyote, muwe mkimwomba Bwana, ili watu wote walitambue na kulijua jambo jema na kubwa la namna hii, na hivyo uso wa dunia utabadilika. Na kwa upande wangu, napenda kutoa uhai wangu kusudi watu wote waujue Utashi wa Mungu.

Mie najikabidhi katika sala zenu, na katika sala za marafiki zenu wema. Basi, nikiwaacheni ninyi katika nafasi ya heshima ya Utashi wa Mungu, ninawaleteeni busu lake la Mwanga na la Pendo. Ni mimi nikisema.

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 02
Kwa Padre Antonio, wa V.
12 Novemba, 1917

Y.M.Y.

Utashi Mtakatifu wa Mungu uwe ni pigo endelevu la moyo wetu.

Mheshimiwa Padre Antonio,

Ni Yesu peke yake awezaye kutufariji wakati wa mateso yetu; kwa hiyo tumgeukie yeye peke yake, tujitupe mikononi mwake mithili ya watoto laini na wachanga. Na endapo maumivu yanatufanya tutoke machozi, basi kwa machozi yetu tuloweshe mikono yake ya kibaba, na Yesu Mtamu, atakapoona mikono yake imelowana na matone matone ya machozi yetu, Yeye Mwenyewe atatukausha machozi yetu na atatuambia: “Mwanangu, je umekuja kwangu kulia machozi? Mbona Mimi ninapenda kugeuza machozi yako yawe furaha, machungu yako yawe utamu. Katika moyo wako nitamwagia bahari ya neema zangu...”. Kwa hiyo, hebu tukabidhi yote kwa Yesu hata tatizo hili la nchi yetu tunayoipenda. Yeye atafanya hayo yote yawe na manufaa kwa roho zetu.

Natumaini kuwa mpaka kipindi hiki mtakuwa mmepata taarifa juu ya wale ndugu zenu. Muwakabidhi kwa roho tohorani wanaotakaswa ambao ni wao watakaoshughulika kuwaweka katika usalama. Watoleeni ahadi ya Misa kama saba mfululizo na kwamba kama ndugu wenu watabaki salama .....

Na Mimi naomba sala zenu. Katika kipindi hiki kigumu namna hii tuzidi kusali sana sana. Sala ndiyo itatukinga na kivuli cha adui na badala yake itatufunika kwa kivuli cha kimungu ambacho kitatufanya sisi tusionekane mbele ya macho ya adui.

Nikiwakumbukeni kwa heshima zote (nk.)

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu

Corato, 12 Novemba, 1917
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 01
Kwa A D. Michele Samarelli, (Bari – Italy)
14 Oktoba, 1917

Y.M.Y. [Yesu, Maria, Yosefu]

Utashi Mtakatifu wa Mungu na uwe ni busu letu endelevu linalotuunda sote katika Yesu.

Mheshimiwa sana Mwana Tauhidi,

Yesu Mwema atufungilie ndani ya Utashi Wake hata atuwezeshe tusiwe tunakumbuka tena utashi wetu. Oh, ni jinsi gani tutakavyofurahia, kwa vile katika matendo yetu yote, tutakuwa tukionja nguvu na msukumo wa kimungu, tutaonja pumzi ya Yesu katika sauti yetu, na tutakuwa tunaonja pia uwezo na upendo wake Yesu Mwenyewe. Na ndipo kwa kweli tutaweza kumwambia Yesu: “Ninakupenda; na ni kweli, kwa vile katika Utashi Wako ninakuwa na mamlaka hata juu ya Pendo lako. Kwa sababu hiyo Pendo stahiki kwako halipo katika kauli yangu mimi ya ‘nakupenda’, bali lipo tu katika Pendo lako Wewe”.

Yesu hawezi akakubali ashindwe kwa pendo la mwanadamu wake. Atatupenda kwelikweli hata tuchanganyikiwe na upendo wake. Katika kila pigo la moyo wetu, katika kila pumzi na katika kila wazo letu, itatujia sauti isemayo, ‘nakupenda’ ya Yesu Mtamu, na sauti hizo za ‘nakupenda’ zitatujia na zitasikika nyingi tu hata sisi tutashindwa kuzihesabu zote.

Hapa sasa ni jibu lake. Yaelekea Yesu anakuambia: “Je unataka nikupende sana sana, nikupende mno mno? Je wataka nitie ndani yako mabahari yale makubwa ya Pendo langu hata uwe kichaa kwa pendo lako? Basi uishi daima ndani ya Utashi Wangu. Ujisahau wewe mwenyewe, uniruhusu Mimi niishi ndani yako, ndipo Pendo langu kwako litapanda na kufikia kikomo kile cha mwisho usipoweza ukaongeza kitu. Kwa namna hiyo, kadiri utakavyokuwa ukitimiza mapenzi yangu, ndivyo na Mimi nitazidi kukupenda zaidi na zaidi, kwani Utashi Wangu unastahili Pendo langu lote. Ndivyo nitakavyokuachia wewe pia Pendo langu”. Oh, Yesu ni mwema ilioje! Kama sisi tungemjua Yeye, hakika tungekufa kwa kutekwa na Pendo. Na Mwenyewe Yesu Mtekaji wetu, ili asituache tukafa, anatuficha kwa upendo ndani ya Pendo...... Tendo tu la kuona mashaka kuwa Yesu hatupendi sana ni neno la kumsikitisha sana na kumtesa Yesu. Pendo huwa linaita Pendo lingine. Na jinsi tunavyozidi kusadiki kuwa Yeye anatupenda, ndivyo tunavyozidi kuvutwa kumpenda zaidi. Na Yesu anapogundua kuwa anapendwa ndivyo na Yeye anazidi kutupenda sisi.

Sasa ningependa nikushukuru kwa ile picha nzuri sana ya Kitambaa Kitakatifu. Nilikuwa naitunza lakini Padre mwingine kaja kaninyang’anya. Na Yesu, aliye Mwema kabisa, akairejesha kwangu kwa kupitia Padre mwingine.

Asante! Najikabidhi katika sala zako takatifu...

Corato, 14 Oktoba, 1917
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 42
Kwa Sista Remigia
25 Decemba, 1935

Fiat – In Voluntate Dei!

Binti yangu mpenzi katika Utashi wa Mungu,

Asante sana kwa barua yako ya matashi mema; nami ninapenda leo kukushukuru kwa moyo wote. Ni leo jioni hii ya Noeli ninapokuandikia. Yaani, Mtoto wa Mbinguni amezaliwa. Lakini, zaidi na zaidi ni kuwa Yeye huwa anazaliwa katika kila nafasi na wasaa. Huyu Kichanga Mpenzi huwa anarudia kuzaliwa ndani ya kila tendo jema tunalofanya; huwa anazaliwa tena katika kila nafasi tunapojikabidhi mikononi mwake, na katika nafasi zile zote tunapolia na kumwita toka katika kilindi cha moyo wetu ‘Ee Bwana, nataka kutekeleza Utashi wako’.

Kwa hiyo basi, sikutakii Heri za kuzaliwa Yesu, kwani kazaliwa tayari. Bali mimi ninakutakia hasa uweze kumfanya akue, nakutakia uweze kumpenda na kishapo umpashe joto, kwa vile namwona akitetemeka kwa baridi, namwona midomo yake imenyauka na kupauka kwani hewa ina ubaridi wa barafu. Kwa hiyo Yeye anataka sasa mabusu yako ya upendo motomoto, anataka hewa ya pendo lako ambayo itampasha joto. Miguu yake na mikono yake naiona imeganda na baridi na inahitaji matendo yako, anahitaji vitendo vyako mbalimbali unavyotenda kwa ajili ya kumpenda Yeye. Mathalani unapovaa nguo zako ili kujisetiri. Na kwa chakula chake anahitaji Utashi Wake uwe unatawala ndani yako. Kwa hiyo basi, ningekuomba unisaidie kumfanya Mtoto huyo wa kimungu akue, unisaidie kumfurahisha na umpatie utashi wako ili awe anauchezeachezea katika mikono yake hiyo midogo ili wakati anapotoa machozi mengi akuone wewe unayemwezesha kubembeza na kumfanya atabasamu.

Halafu kuna jukumu lingine analokukabidhi huyo Kichanga Mpenzi. Anataka wewe uwafahamishe na kuwajulisha hao wasichana wanaoishi nawe, kuwa ni budi wao wote wawe na Yesu moyoni mwao na uwafundishe jinsi ya kumjua Yeye Yesu. Ukitekeleza hayo, ndipo unaweza kuwa na amani kwani utakuwa unatengeneza tabernakulo nyingi sana kwa ajili ya Kichanga Yesu. Unajua mimi sipendi na wala Yesu hapendi wewe upoteze amani.

Katika kila kitu wewe uwe unatafuta Utashi wa Mungu na hivyo nafsi yako yote itageuka kuwa ni sala endelevu katika kila kitu. Si maneno ndiyo yanayofanya sala, bali ni muungano wetu na Utashi wa Mungu. Ndipo hapo kila kitu hugeuka kuwa kitukufu, kila kitu hugeuka kuwa kitakatifu, na kila kitu huwa ni sala ndani yetu. Halafu unajua amani ni jicho la vitendo vyetu na ndiyo itakuonyesha namna ya kumpenda Yesu na itakufanya umpende kweli.

Padre Benedetto naye anakutakia heri na anakubariki. Uniombee na mimi kwani ninahitaji sana sala zako. Ninakuacha sasa udumu umefungiliwa ndani ya FIAT. Angalia usithubutu kamwe kutoka. Na ninamwomba Mpendwa Mtoto Yesu akubariki.

Ni mimi shangazi yako akupendaye sana.

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu

Corato, 25 Decemba, 1935