Utashi wa Mungu na Upendo wa Mungu - Luisa Piccarreta
41 subscribers
283 photos
53 files
576 links
Fahamu kuhusu kutimia kwa Sala ya Baba Yetu kupitia Maandishi ya Mtumishi wa Mungu Luisa Piccarreta, Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - Kuishi Utashi wa Mungu
Download Telegram
SAA YA KUMI NA TATU

Tunashuhudia siku ile Mtoto Yesu Mpenzi, kwa mara yake ya kwanza, alipojitokeza nje kwa watoto wa Misri. Tunamshuhudia akiwabariki, na sisi tunamwomba Yeye, kwa njia ya Baraka Yake, atie mhuri juu ya tashi za kibinadamu.

Ewe Mtoto Wangu wa Mbinguni, Pendo Lako linakusukuma utoke nje ya kile kibanda kidogo na uende nje. Na watoto wa Misri, wakivutwa na uzuri wako unaopendeza, wanakusanyika kwa wingi kukuzunguka, na Wewe, kwa upendo mkubwa unazungumza nao. Wakiwa wametekwa Nawe, wao wanakusikiliza. Baada ya kuwafundisha unahitimisha kwa kuwabariki na halafu unatoka ukikimbia kwenda kwa Mama Yako kwani pendo lake linaleta mwangwi ndani ya moyo Wako.

Wakati naye Mama anapokuita Wewe unakimbilia mara mikononi mwake. Ewe Pendo Langu, mimi ninapenda kukufuata katika kila kitu kwani napenda iwe inasikika tena ile kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’. Kauli hiyo iwe inasikika chini ya hizo hatua zako nyepesi, isikike unapotembeza hiyo mikono yako midogo, isikike katika maneno yako matamu, pendevu, yenye nguvu ya kuteka akili, na yaliyojaa uhai.

Napenda isikike hata katika mtazamo wa macho yako yanayovuta na kupendeza. Na katika hayo yote ninakuomba Ufalme wa FIAT Yako. Wakati huo unapowabariki watoto, ubariki hata mimi Binti Mdogo wa Utashi Wako na kwa Baraka Yako, ugonge mhuri wa uhai wa Utashi Wako ndani ya hii roho yangu ndogo. Ninaendelea kukufuata, Ewe Mtoto wa Kimungu, wakati unapokwenda kufanya matembezi katika mashamba na pale unapofurahia kupita kuchuma maua. Unaponyosha mkono wako ili kuchuma maua, mimi ninakupenda Wewe na juu ya kila ua unalochuma, mimi napenda kurudia kile kiitikio changu cha ‘Ninakupenda, Ninakupenda’.
Hata hapo ninakuomba upeleke kwa Baba Yako wa Mbinguni hili ua dogo la huyu Binti Mdogo wa Utashi Wako, ili kusudi asiweze tena kujua, wala asiweze kupenda na wala kutaka kitu kingine chochote isipokuwa FIAT Yako ya milele.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA KUMI NA NNE

Tunamfuata Yesu ambaye, baada ya kukaa kama mkimbizi, sasa anarejea kwake Nazareti. Kwa kumnyeshea mvua ya kauli yetu ya ‘Ninakupenda’, tunamwomba, kwa sauti elfu na elfu, Ujio wa Ufalme Wake wa Kimungu.

Ewe Mtoto Yesu, Uhai Wangu, natambua kuwa kipindi chako cha kuwa mkimbizi kimemalizika na sasa unarejea Nazareti; na mimi nataka nikufuate hatua kwa hatua, yaani, napenda kuambatana nawe nikikusindikiza katika mvua inayokunyeshea kauli za ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, na Ninakuheshimu’. Kwa hiyo, ili niweze kusaidiwa, ninaita msaada wa mwanga wa Jua unyeshe ‘Ninakupenda’ kama mwanga. Ninaita na mmetuo wa nyota zote nao uinyeshe ‘Ninakupenda’. Na ule mvumo wa upepo, iwe ule wa sauti ya kulia, au upepo ule unaopiga kelele kali, au ule unaopiga kama miluzi, nao ninauita uinyeshe ‘Ninakupenda, Ninakupenda’. Ninawaita na ndege wote wanaoruka hewani, ili nao wakusindikize kwa musiki wao, kwa nyimbo zao, na kwa sauti zao za kutetemeshwa, zote zikisema: ‘Ninakupenda, Ninakupenda’. Ninawaita na hao kondoo wadogo, nao walie na kuita wakisema ‘Ninakupenda’. Naiita na bahari, nayo itoke na kuvuka toka kule kwenye ufukwe wake, ili ikusindikize kwa mawimbi yake ya ‘Ninakupenda’. Lakini, je wafahamu ni nini hasa, anachotaka huyu Binti Yako Mdogo anapokunyeshea mvua hii ya ‘Ninakupenda’? Nataka kitu kimoja tu: Ukubali kunipatia Ufalme wa Utashi Wako. Na wakati unapojifungilia pale kijijini Nazareti, mimi ninajifungilia pamoja Nawe, ili niwe ninaendeleza hii mvua ya ‘Ninakupenda’ yangu, ili kusudi nikushinde Wewe kwa njia ya pendo hata uweze kunipatia mimi kile ambacho Wewe Mwenyewe unataka, ambacho na Mama Malkia anataka na ambacho na mimi pia ninataka: Yaani, kwamba Utashi Wako upate kujulikana na upate kutawala kati ya wanadamu.

Ewe Yesu, Uhai Wangu, mimi sasa nipo tayari na Wewe, hapa katika nyumba hii ya Nazareti. Hatua kwa hatua napenda kukufuata ili niendelee kugonga mhuri wa ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’ juu ya kila kitu unachofanya Wewe, na ili kusudi nikuombe Wewe Ufalme wa Utashi Wako. Iwapo mikondo ya pendo inatiririka kati ya Wewe na Mama Yako, ndivyo pamoja nayo inatiririka ‘Ninakupenda’ yangu. Hiyo yote ni kwa kusudi la kuwaombeni Wewe na Mama wa Mbinguni kuwa Utashi Wako ujulikane. Kama Wewe unakula chakula, hapo na mimi nagonga ‘Ninakupenda’ yangu, ili kwa kauli hiyo nikuombe lishe ya Utashi Wako kwa ajili ya wanadamu wote. Unapokunywa maji, mimi natiririsha ‘Ninakupenda’ yangu ndani yake, ili kukuomba kwamba maji safi ya Utashi Wako, yatiririkie katika matumbo yetu, kwamba, ndani ya watu wote yakatengeneze mzunguko wa damu, ambayo, katika viungo vyote vya mwili wetu, itakuwa ikituwezesha kuonja uhai wa Utashi Wako wa Kimungu. Unapogonga mti au ubao wowote kwa mikono yako hiyo ya uumbaji, hapo unakuwa ukigonga ubao wa utashi wangu wa kibinadamu ili kusudi upate kuongokea katika mwanga wa Utashi wa Mungu.
Hiyo ‘Ninakupenda’ yangu inaendelea kukufuata Wewe. Wakati wa shughuli zako za ufundi seremala, unapotwaa misumari na nyundo katika mikono yako, ninakufuata, ili kwa njia ya ‘Ninakupenda’ yangu, niweze kukuambia hivi: Pigilia kwa misumari tashi zote za kibinadamu ili ziruhusu Utashi Wako uweze kuishi kwa uhuru. Wakati ule unaporudi na kuingia peke yako chumbani mwako kwa ajili ya kusali au kwa ajili ya kulala, mimi huwa sikubali kukuacha peke yako. Mimi huwa ninapenda kuwa pale kando yako, na endapo sipati kitu cha kukuambia, basi nitakuwa nikipwepa hapo sikioni pako nikisema: “Ninakupenda, Ninakupenda, Ninakupenda, Ninakuabudu”. Na kwa sala zako Wewe Mwenyewe, nitakuomba Ufalme wa FIAT Yako, na nitakuomba pia, kwa nguvu ya usingizi wako, uutie usingizini utashi wa kibinadamu, ili kusudi usiwe tena na uhai wowote, na badala yake, niwe ninaupata daima uhai wa Utashi Wako wa Kimungu peke yake. Ewe Yesu Wangu Mtukufu, mimi ningejionja uchungu sana iwapo kama nisingeweza kukufuata katika mambo yote, na kama nisingekuwa naendelea kukushughulisha na usindikizi wangu na kama nisingekufanya uwe unasikia daima kiitikio cha kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’, kwa ajili ya kukuomba Wewe, nikiwa pamoja na matendo Yako, Ufalme wa Utashi Wako. Ni kwa vile, ninapokuwa kando yako, mimi huwa ninaonja mapigo yale yale ya Moyo Wako, yaani ya kuwa nao huo Moyo Wako unataka kitu hicho hicho, na hata wenyewe Utashi Wako wa Kimungu, nao unataka ujulikane kwa watu, na unataka utawale na kuamrisha kati ya wanadamu.

Kwa sababu hiyo, ninakufuata hata unapokwenda Hekaluni. Wewe lakini, kwa tendo lako la kumwepa Mama Yako, ulikuwa umeleta maumivu makali na ya uchungu aliyoyakabili katika muda wa siku tatu za kupotea kwako. Mimi ninatiririsha ‘Ninakupenda’ yangu ndani ya lile teso la Mama yako na katika tendo la kupotea kwako, ili kusudi niombe kwamba utashi wa kibinadamu upotelee mbali. Kwa jinsi hiyo sisi, tunapokosa kuuona, tuwe tunaamua kuishi kwa Utashi wa Mungu na tuishi katika ile furaha ambayo ninyi, Mama na Mtoto, baada ya kupoteana, mliweza kuionja kwa karibu zaidi, pale mlipokutana tena. ‘Ninakupenda’ yangu inakuomba kwamba wanadamu wasikuletee tena uchungu na maumivu yale ambayo utashi wa kibinadamu huwa unakuletea mara kwa mara, lakini badala yake wawe wanakupatia furaha zilizo safi na raha mbalimbali zilizo nzuri kabisa za FIAT Yako ya Kimungu inayotawala ndani yao.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA KUMI NA TANO

Tumfuate Yesu kule jangwani. Tunapofika na kusimama pale kwenye mto Yordani, tumwombe atupatie Ubatizo wa wokovu wa Utashi wa Mungu ili kusudi watu wote waupate Uhai Wake.

Ewe Chema Changu Kikuu cha Mbinguni, mimi naharakisha kukufuata kwani vinginevyo muda hautanitosha kuweza kukufuatilia katika yote. Ninakuona tayari umejiandaa kutoka kwenda jangwani. Unamkumbatia Mama yako ukimbana kwenye Moyo wako unaoumia na kulia kwa pendo, na unamwambia: “Kwaheri, ubaki hapa, Ee Mama. Ninakuachia FIAT Yangu ya Kimungu, iwe hapa kama msaada kwako badala yangu, iwe kama uhai wako na kama mjumbe wa mawasiliano kati ya Mimi na Wewe’ . Utashi Wangu utakuwa unakuambia kila kitu atakachokuwa anatenda Mwanao, na wewe utakuwa ukinifuata katika kila kitu, kiasi kwamba, hata kama utakuwa mbali, FIAT itakuwa inakuleta karibu kabisa nami, hata tutajiona kuwa ni kitu kimoja tu”.

Ewe Yesu, nipe mkono wako na unichukue nije Nawe, ili chochote utakachokuwa unatenda kisiweze kunitoroka akilini mpaka niweze kufungilia ndani yake ile ‘Ninakupenda’ yangu, kwa ajili Yako, kusudi nikuombe Ufalme wa Utashi Wako wa Kimungu juu ya dunia. Kwa hiyo, wakati Wewe unaendelea kutembea peke yako, mimi ninakufuata hatua kwa hatua nikiwa nimebeba kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’. Katika kila pumzi yako nataka nikufanye uwe ukipumua ‘Ninakupenda’ yangu. Kila moja la neno lako nalifungilia ndani ya ‘Ninakupenda’ yangu. Katika kila mtazamo wa jicho lako nataka uwe unakutana na ‘Ninakupenda’ yangu. Na wakati unapowasili pale Yordani mimi napenda nitiririshe ‘Ninakupenda’ yangu ndani ya maji yale. Natiririsha kwa jinsi kwamba, kama vile Mtakatifu Yohane Mbatizaji alivyotiririsha maji kichwani pako kwa ajili ya kukubatiza, ndivyo sasa na Wewe uonje kuwa Binti Yako Mdogo kamwe hatakuacha peke yako bali anaambatana nawe kwa njia ya ‘Ninakupenda’ yake. Kwa kutiririsha kauli hiyo katika maji yale anataka akuombe Wewe utoe maji ya ubatizo ya Utashi Wako wa Kimungu kwa ajili ya wanadamu wote, ili huo uwe ndio mwanzo wa Ufalme Wake. Ewe Pendo Langu, katika tendo la kisherehe la Ubatizo wako, napenda nikuombe neema moja ambayo Wewe kwa uhakika hutanikatalia: Ninakuomba kwamba, kwa mikono yako mitakatifu, uibatize hii roho yangu ndogo katika maji yaletayo uzima na ya uumbaji ya Utashi Wako wa Kimungu. Ninaomba hilo ili kusudi roho yangu isionje kamwe, isione, na wala isiujue uhai mwingine isipokuwa uhai wa FIAT Yako. Ah, kweli kabisa, ninakuomba kwamba uwepo wangu usiwe ni kitu kingine, bali uwe ni tendo moja pekee la Utashi Wako.
Ewe Yesu Wangu, Pendo Langu tamu, mimi ninakufuata kwenda jangwani. ‘Ninakupenda’ yangu haitakuacha peke yako katika jangwa hili. Nitabaki kuwa kando yako usiku na mchana. Nitakapokuona, ukiwa na masikitiko sana, ukiwa na mahangaiko, unapokufa kwa pendo, na nitakapokuona ukisali na ukilia kutokana na upweke wa Utashi Wako wa Kimungu baada ya wanadamu kuutoroka, mimi nitabaki kando yako. Wewe unaonja mara moja na hai kabisa maumivu ya Utashi huu wa Kimungu, siyo tu kwa vile hautawali kati ya wanadamu, bali kwa vile Utashi huu umeachwa katika upweke mithili ya jangwani, ni kama umeachwa uhamishoni. Kwa hiyo Ubinadamu Wako Mtakatifu mno unalia na unaomba, kwa niaba ya familia yote ya binadamu, kwamba zile tashi mbili, yaani, ule wa Kimungu na ule wa kibinadamu, budi zikutane na zijipatanishe zenyewe. Utashi wa kibinadamu unauita Utashi wa Mungu, ili kuuruhusu uje utawale, na Utashi wa Mungu unasamehe juu ya kipindi kile kirefu, ambamo wanadamu walikuwa wameushika na kuuzuia uhamishoni. Mimi nayachukua machozi yako na kuyafanya yawe ni ya kwangu, sala zako ziwe ni za kwangu, vionjo vya kifo vya Moyo Wako unaoungua kwa pendo, navyo viwe ni vya kwangu. Naendelea kukifuatilia kila kitu kwa ‘Ninakupenda’ yangu. Natengeneza minyororo mitamu ya pendo, na ninaingiza nafsi Yako yote ya Kimungu ndani yake kwani ninataka nikuvute kwa lazima ukubali kunipa Ufalme wa Utashi Wako wa Kimungu hapa duniani. Ebu sikiliza Ewe, Uhai Wangu, mbona ni yenyewe mapigo ya Moyo Wako, ni matamanio yako Mwenyewe, ni machozi yako, ni maumivu yako, ndiyo hayo yanayotaka na yanayoomba Ufalme wa FIAT Yako. Kwa hiyo basi, endapo hutaki kunisikiliza mimi, basi nakuomba ujisikilize Wewe Mwenyewe, na unipe jibu kusudi tutoke katika jangwa hili huku ukiniambia hivi: “Ah, ndiyo basi! Ufalme wa Utashi Wangu utafika hapa duniani!”

Ewe Yesu Wangu, Moyo wa moyo wangu, ninakuona ukiharakisha mpango wa kutaka kutoka jangwani. Naona unapitia tena kule kwenye mto Yordani ili, kwa upendo, ukamchungulie tena mpenzi wako Yohane. Moyoni mwake unatia mafuriko ya pendo na neema, na halafu kwa haraka haraka unaendelea na safari hadi kuifikia nyumba yako ya Nazareti, ambako pendo la Mama wa Mbinguni linakuita kwa mfululizo. Na tazama, Oh, nini hiki ninachoshuhudia kikinivuta hapa mbele yangu! Mama na mtoto wanarukiana, huyu katika mikono ya mwenzake, na kwa kuyeyushiana, hawa wawili wanatengeneza pendo moja tu. Maadam Malkia wa Mbinguni amekuwa akionja hitaji kali mno la kumwona tena Mtoto wake. Moyo wake wa kimama ulikuwa umeunguzwa moto wakati huu alipokuwa hayupo, wakati yeye Mama alikuwa anatamani kujimwaga ndani ya Mwanae, ili aweze kupokea umande wa Pendo Lake, ili asibaki ameteketezwa na miali ile ya moto, iliyokuwa ikimtafuna. Na Yesu, Mkombozi Wangu wa Mbinguni, kwa upande Wake, alikuwa naye akionja hitaji kali sana ya pendo la Mama. Ni kwa sababu hiyo alirukia mikononi mwa Mama Yake kusudi akatoe pendo na kupokea pendo. Hata mimi, nikiwa nimeshika ule mwali mdogo wa moto wa ‘Ninakupenda’, narukia katika makumbatio yenu hayo yaliyo safi sana, narukia katika makaribiano yenu, narukia katika mioto ya pendo la Mama na Mtoto wake, na kwa wote wawili, Mama na Mtoto, ninawasihi ninyi nyote mnipatie Ufalme wa Utashi Wenu. Ewe Mama Mtakatifu, urudie pamoja nami na usali pamoja nami, kwamba Utashi wa Mungu ujulikane, utawale, hapa duniani kama kule Mbinguni.

Wakati huu ambapo Mama na Mtoto wanajipumzisha kidogo katika pendo lao na wakati wanapochukua uhai, papo hapo wanajiandaa kwa ajili ya kukabili hali ya kuachika ya kipindi kirefu zaidi. Tayari Yesu Wangu, ambaye daima mtu hawezi akamfikia katika kiwango cha Pendo Lake, anachukua njia ile inayoelekea kwenye maisha yake ya hadharani. Anamkumbatia kwa nguvu kabisa Mama Yake, kwenye moyo wake, kwa ajili ya kumtia nguvu huyu Mama, kwa mara nyingine anaaga na anatoka peke yake kabisa, kwa ajili ya kwenda kueneza Neno lake la Kimungu kwa mataifa, kwenda kuunda wafuasi wake, na kwenda kutangaza Injili Takatifu.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA KUMI NA SITA

Tumfuate Yesu kwenye Harusi ya Kana na pale tunamwomba augeuze utashi wa kibinadamu na aubadilishe na Utashi wa Mungu. Tuendelee kumfuata katika maisha yake ya hadharani.

Ewe Yesu, Pendo Langu na Uhai Wangu, ninatambua kwamba, kabla ya kuanza maisha yako ya hadharani, Pendo liwakalo la Moyo Wako linakuvuta kwenda kwanza kuhudhuria harusi ya Kana. Mimi, pamoja na Mama Yako, ninafuata hatua zako, nikiwa nimebeba ‘Ninakupenda’ yangu. Ninausikia Moyo Wako ukigonga kwa mapigo ya Pendo na maumivu.

Hapo unakumbuka harusi ile nyingine, iliyohudhuriwa na kubarikiwa Nawe pale katika Bustani ya Edeni. Ni ile ya Adamu na Eva walipokuwa hawana doa la dhambi. Ilikuwa ni ndoa katika nyanja mbili: kwanza ilikuwa ni ndoa kati ya Utashi Wako wa Kimungu na utashi wa kibinadamu, pili ilikuwa ni ndoa kati ya mtu mwanaume na mtu mwanamke. Katika ndoa hii, kama posa, Wewe uliutoa Uumbwa wote na hata Utashi Wako wa Kimungu ulio hai. Wewe uliutia Utashi Wako huo ndani ya moyo wao na ndani ya vitu vyote vilivyoumbwa.

Kwa minajili hiyo, uwepo Wako leo katika harusi hii, kitu kisichokuwa cha kawaida kwako, kunaniambia kwamba Wewe unapenda Utashi Wako wa Kimungu utawale, na unataka upange upya mambo yote ndani ya wanadamu.

Na mimi upande wangu, Ewe Yesu Wangu, nataka nije hapa kando Yako ili, katika mtazamo wako mtamu wa macho, katika sauti yako yenye musiki mtamu, na katika hiyo mitindo yako ya kuringa, niweze kujaza kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, na Ninakushukuru’. Kwa nguvu ya Pendo lile lililokusukuma Wewe uyapokee maombi ya Malkia wa juu mwenye mamlaka hata ukatenda muujiza wa kugeuza maji kuwa divai, mimi ninakuomba utende sasa, pia kwa pendo la Mama Yako wa Mbinguni, muujiza mkubwa wa kugeuza utashi wa kibinadamu uwe ni Utashi wa Kimungu, na uufanye huo Utashi wa Mungu utawale hapa duniani sawa kama kule Mbinguni.

Ewe Mama Mtakatifu, wewe uliyekuwa unahangaika sana kwamba Yesu ageuze maji kuwa divai, ili kuwasaidia wale wanaharusi, naomba usimwache Yesu atoke na kwenda kwenye utume wake wa hadharani, bila kwanza kukubali kwamba Utashi Wake ufike na utawale juu ya dunia.

Ewe Chema Changu Kitamu, hii kauli yangu ya ‘Ninakupenda’, pamoja na kale kawimbo bembezi endelevu, kwa ajili ya kukueleza kuwa ninataka Utashi Wako wa Kimungu utawale hapa duniani kama kule Mbinguni, hivyo havitakoma kamwe. Na ili kukulazimisha, nataka nikufuate katika kila kitu kusudi niweze kutia ‘Ninakupenda’ yangu katika matendo yako yote.

Nitaiweka hiyo ikuzunguke, ndani yako na nje yako, kama kikosi cha jeshi kali ili liwe linakupwepea sikioni mwako likisema: Ebu nipatie FIAT Yako hiyo inayogonga Moyoni Mwako, ebu nipe Utashi Wako huo unaozungumza ndani ya neno lako, Utashi huo unaotenda kazi mikononi mwako, huo unaotembea katika hatua zako, na ambao ndani ya nafsi yako nzima unakuambia: Ninataka Utashi Wako unaotawala hapa duniani kama kule Mbinguni. Lo, ebu umsikilize huyo Binti Yako Mdogo, ebu ujisikilize Wewe Mwenyewe, Wewe unayependa kwamba tuishi katika FIAT Yako!.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA KUMI NA SABA

Tumfuate Yesu katika maisha yake ya hadharani, katika miujiza yake, na tumwombe atende ule muujiza mkuu wa kuzifufua roho za watu katika Utashi wa Mungu.

Ewe Yesu Wangu, Uhai Wangu Mpenzi, ninakuona unapotoka na kuagana na Mama Yako. Lakini, tashi zenu hazitengani, bali, ni kwa vile tu unapasika kuaga ili ukaanze maisha yako ya hadharani. Miguu yako inaelekea Yerusalemu kwa ajili ya kwenda kufundisha Neno Lako takatifu pale Hekaluni. Na pale utawaambia wazi hadharani kwamba Wewe ndiye Yule aliye Masiha wa kweli wanayemtamani. Lakini, ni maumivu mangapi yanaingia Moyoni Mwako! Ni mateso mangapi! Wanaposikia mahubiri yako, badala ya wao kujitupa miguuni pako na kukupokea kama mwokozi wao wa Mbinguni, wao wanakuangalia kwa macho ya kutisha na ya chuki, wanakusikiliza huku wakinung’unika, kiasi kwamba hakuna hata mtu mmoja kati yao anadiriki kusogea na kukukaribisha akikuambia: “Njoo karibu nyumbani kwangu”. Wewe unaachwa mpweke! Kutokana na utovu wa shukrani kati ya watu wale, unapasika kuombaomba mkate, unapasika kuwa unatoka nje peke yako; tena ni lazima uwe unatoka usiku tu, kwani unalala sakafuni na wala huna cha kujifunika, bali unalala ukitazama nyota za angani wakati wote wa usiku. Nyota zile, kwa memetuko wao mzuri na wa taratibu, zinakusindikiza, na Wewe unapitisha usiku wote katika machozi na katika sala kwa ajili ya hao hao watu ambao hawataki kukujua.

Ewe Yesu Pendo Langu, ebu njoo hapa katika mikono yangu ili uweze kujipumzisha kidogo. Ninataka niwe ninalia na kusali pamoja Nawe, nataka nipange usindikizi wangu wa ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’ katika maumivu unayoyapata, katika machozi yako unayomwaga, katika maneno yako yasiyopokelewa. Nataka niweke ‘Ninakupenda’ yangu mbele ya hatua zako, nyuma na mbele ya hatua zako, ili kusudi miguu yako isiwe inaonja ugumu wa udongo usiokuwa na shukrani, bali badala yake iwe inaonja ulaini wa ‘Ninakupenda’ yangu na ninapenda nikuambie: Ewe Yesu, je waona jinsi unavyoteseka? Basi fanyiza ili Utashi Wako wa Kimungu utawale na ndipo maumivu yako yatakoma.

Yesu Wangu, Uhai wa moyo wangu duni, Pendo lako halisimami. Unaendelea kurejea Hekaluni na unaendelea kuwagawia watu Neno lako takatifu. Ingawa kama watu wakubwa na wasomi hawataki kukutambua na kukuheshimu, kundi kubwa la masikini, la wasiosoma, na wanaoteseka na maradhi mbalimbali, wanakukimbilia na kukusonga, wakiwa wanavutwa na mitindo yako ya upendo na wema, wakivutwa na sauti Yako yenye kuteka, kwani wanapokusikiliza ukizungumza huwa wanaonja kuguswa sana, na kuchomwa moyoni mwao. Ni hawa mafukara ndio wanafungua angalau mshipa wa furaha na raha ndani ya Moyo Wako. Kwa hoja hiyo, unaonja walau kwamba unaweza sasa kuwafariji, kuwafundisha, kuwaponya masikini ambao, wanahesabika kuwa kama takataka za jamii. Wewe unakuwa sasa ni rafiki, mwalimu, na mganga tabibu mwema wa masikini. Kwa hao wote Wewe unayo maneno ya faraja. Na kwa ajili ya kuwaponya, Wewe hunyanyapai kuvigusa viungo vyao vya mwili vilivyo na maradhi mbalimbali.

Unakwenda mji kwa mji, na mimi nataka nifuate hatua zako, ili nikaweke ile alama yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakushukuru, ninakuheshimu’ katika njia mbalimbali, na katika miji. Na mara kwa mara nitakuwa nakusogelea na kukubana mkononi nikikupwepea katika sikio Lako: Ebu unipe Ufalme wa Utashi Wako, na ili kukusukuma unipatie hilo ninalokuomba, kwa pendo lile lile la matendo ya kwako.
Lakini, pindi unapozungukia mitaa na miji, panatokea kisa cha kushangaza sana katika makundi yanayokuzunguka Wewe: vipofu, mabubu, viziwi, vilema, waliopooza, wakoma na wenye maradhi na matatizo mbalimbali ya kibinadamu, wanaleta uchungu sana katika Moyo Wako wa Kimungu. Oh, ni jinsi gani unavyotetemeka! Uchungu gani unauelemea Moyo Wako unapoona jinsi hali ilivyogeuka, kuwa matatizo na mahangaiko, na kuwa hali ya kutisha. Ni hali ile ile ya maumbile ya kibinadamu, ambayo hapo awali ilikuwa ni hali nzuri sana, ya kupendeza, na kamilifu wakati ilipotoka katika mikono Yako ya uumbaji. Hayo yote ni matokeo ya utashi wa kibinadamu ulioporomoka na kuharibika. Huo utashi umefurikisha nje yake mambo yake machafu na ukafanya ubinadamu wote upoteze furaha yake.

Lo, Ewe Pendo Langu, ninakuomba kwamba ile FIAT Yako irejee na itawale kati yetu. Kama Wewe ukitaka, unaweza. Na yenyewe FIAT itafukuzia mbali yale matatizo na machungu yote yaliyoletwa na utashi wa kibinadamu. Kwa sababu hiyo mimi ninatiririsha ‘Ninakupenda’ yangu katika tendo lako lile ambapo unafungua macho ya vipofu ili wajipatie tena uwezo wa kuona, ili waweze kuutambua na kuujua Utashi Wako wa Kimungu. Ni vipofu wengi ilioje wa Utashi Wako wa Kimungu! Dunia hii imejaa hawa vipofu duni. Kwa hiyo ninakuomba kwamba wote wapate uwezo wa kuona ili waweze kuutambua na kuutazama Utashi Wako Mtakatifu kabisa.

Lakini natambu, Ewe Pendo Langu, kuwa hatua kwa hatua, unapita kutenda mema mengi kwa watu wale masikini. Anapojitokeza mbele yako yule kiziwi, Wewe, kwa amri ya sauti yako, unamfungulia masikio yake. ‘Ninakupenda’ yangu inatiririkia katika sauti yako inayoamrisha, na pale ninakuomba kwamba ufungue masikio ya wale viziwi wengi wa Utashi Wako wa Kimungu. Katika hatua nyingine, Wewe unafungua ulimi wa yule aliye bubu. Ni bubu wengi wangapi, ambao hawana ulimi tena wa kuweza kuzungumzia ‘FIAT’ Yako ya Kimungu! Na mie hapa, kifudifudi miguuni pako, ninajiegesha penye magoti yako, na ingawa kama ni bado msichana mdogo sana, kamwe sitajitoa hapa mpaka pale utakaponitendea ule muujiza wa kufungua ulimi wa wale bubu wengi, ili hao wote waweze kuzungumzia juu ya Utashi Wako Mwabudiwa. Yesu Wangu, Moyo Wako unaonja dakika za majonzi na maumivu mengi kwa ajili ya mahangaiko ya wanadamu, matatizo yote yakiwa yametokana na utashi wa kibinadamu. Yaelekea sasa unapita kueneza miujiza yako ili kuwakomboa toka matatizo hayo. Tunaomba utujalie neema ya kuuita tena Utashi Wako wa Kimungu ufike kutawala kati ya wanadamu wote. Basi kwa hiyo, uponye na kunyosha viungo vya viwete, uwatakase wakoma, uwaponye waliopooza.

Na mimi, Ewe Mkombozi wa Mbinguni, nitakuwa nikiambatana nawe, nikiwa na hii kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu na Ninakushukuru’. Na je wajua kwa nini ninakupenda, na kwa nini ninakufuata? Ni kwa vile ninapenda unyoshe miguu ya yule anayechechemea katika Utashi Wako, napenda utakase vizazi vya binadamu kutoka ukoma wa utashi wa kibinadamu, ukoma ulioleta ulemavu wa roho na hata ulemavu wa mwili. Napenda uponye wale wengi waliopooza kutokana na utashi wa kibinadamu.

Ewe Pendo Langu, utashi wa kibinadamu ndio uliopanda mbegu ya maovu yote. Kwa sababu hiyo nakuomba utende ule muujiza wa miujiza: kwamba Utashi Wako utawale, hapa duniani kama vile kule Mbinguni ili kwa njia hiyo maovu yote yapate kukoma.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA KUMI NA NANE

Tumfuate Yesu katika matukio mengine ya maisha yake ya hadharani.

Ewe Chema Changu Mpendwa, Wewe unaendelea na maisha yako ya hadharani huku ukiendelea kueneza popote Neno lako la Kimungu, na ukiendelea kuwafariji wale wanaoteseka. Unamsikia mama mmoja anayelia kwa ajili ya mtoto wake aliyefariki, na sasa yupo njiani akienda makaburini kumzika. Mbele ya mama huyo anayelia, Moyo Wako unashindwa kuvumilia kuyaona yale machozi yanayomtoka. Wewe unalijongea jeneza, unayaita yale maiti yaamkie kwenye uzima na unamkabidhi mtoto yule kwa mama yake. Ewe Pendo Langu, ‘Ninakupenda’ yangu haiwezi kukuacha katika tendo lako hili la kutoa uhai kwa mtu aliyekufa. Ninakuomba uziite zile roho nyingi sana, zilizokwisha kufa mbele ya Utashi Wako wa Kimungu, na ufute machozi ya Utashi wako wa Kimungu, ambayo ni machozi yako pia. Utashi Wako, zaidi ya mama yeyote, umekuwa ukilia kwa kipindi cha karne nyingi sana, unapoangalia watoto wake wengi sana wakiwa wamekufa sababu ya kutoishi ndani yake.

Ewe Yesu Wangu, Uhai Wangu Mtamu mno, Pendo Lako linakusukuma uwe unakimbiakimbia huko na kule, kwenda kila mahali. Unapoitwa kumfufua msichana mdogo wewe hukukataa. Kwa mkono wako unamshika mkono wake, na katika tendo la kumwinua juu, unamwita kurejea katika uzima. Unasema: “Msichana huyu hajakufa, bali analala”. Ewe Pendo Langu, ni wengi walioje, ambao wanalala katika usingizi wa utashi wao wa kibinadamu, na mimi ningependa kutiririsha ‘Ninakupenda’ yangu katika tendo lako lile la kunyosha mkono ili kumfufua msichana. Ndipo ninapenda kukuomba, unyoshe mkono wako wa kulia, kuwaita warejee kwenye uhai ndani ya Utashi Wako. Wala hapatakiwi kitu kingine, isipokuwa kuguswa na Mkono Wako wa uumbaji, yaani kuguswa na tendo la Maweza Yako juu ya roho hizo, ambazo zinalala katika usingizi wa utashi wa kibinadamu. Utende hilo sasa kusudi uunde kikosi cha kwanza cha Ufalme wa FIAT Yako ya Kimungu.

Ewe Yesu Wangu Mpole, kuna bado tukio lingine la kushangaza linalokungoja bado: Wanakuja kwako Marta na Magdalena , wakikufuata ili kukutaarifu kuwa kaka yao amekwisha kufariki. Wanalia, na Wewe unashikwa na uchungu hivi, hata unaanza kulia pamoja nao, na unawaomba wakuchukue kwenda kukuonyesha kaburi lake Lazaro. Ulipowasili kaburini, unawaamrisha walifungue kaburi. Ulitazama na kuona kuwa, baada ya siku nne tu mwili wake ulikuwa umeoza, hata hakuweza kutambulikana tena, na wala hakuweza kusogelewa kwani mwili ulikuwa unatoa harufu mbaya. Wewe unatehemu, unatetemeka na kulia machozi, na kwa sauti ya kuamrisha yenye kutetemeka kutokana na uchungu wako mkali, unasema: “Lazaro, amka uje nje!”. Na ndivyo unamfufua.

Ewe Pendo Langu, kwa nini unalia na kwa nini unapata uchungu mkali katika tendo la kumfufua Lazaro? Ndipo Yesu, alinishika na kunibania kwake na mimi nikamshika na kumbana sana ili niweze kusikia mapigo Yake ya Moyo unaoteseka. Mwangwi wa sauti yake ukawa unasikika ndani ya moyo wangu akiniambia: “Binti Yangu Mdogo, huyu Lazaro aliyekufa, kwangu mimi, amekuwa anawakilisha ubinadamu wote uliokuwa umezeekea katika uovu. Kwa utashi wa kibinadamu, ubinadamu umegeuka kuwa ni maiti iliyooza na inayotoa harufu mbaya. Hiyo hali halisi ya maovu yake, imefanya familia nzima ya binadamu iwe inanuka na isiwe inavumilika mbele yangu. Hali hiyo inaniletea machozi, inanifanya nitehemu kwa maumivu. Na wewe tafadhali uwe unalia pamoja nami na uwe unasali”.
Ah, ndiyo, Ewe Uhai wa Moyo Wangu, mimi ninalia pamoja nawe. Maneno yako hayo ya ‘Lazaro, amka uje nje!’, mimi ninataka niyajaze na ‘Ninakupenda’, na ‘Ninakuabudu’, ili kauli hiyo ikushawishi uwe unayarudia rudia juu ya kila moyo. Huku ukiwa unayamwaga machozi yako kama umande uletao baraka, uwe unarudia kusema: “Toka nje ya kaburi hilo la utashi wa kibinadamu, na ebu uingie tena katika uhai wa Utashi wa Mungu”. Kwa minajili hiyo, watakapokuwa wakisikia uamrisho wa sauti Yako, wote waamke na kuuunda Ufalme wa ‘FIAT’ Yako.

Ewe Yesu Wangu Mpendwa, mimi sitakuacha peke yako kamwe. Ingawa kama sijui ni kitu gani cha kukuambia, lakini, angalau ninajua kukuambia ‘Ninakupenda, Ninakupenda’. Ninataka, matendo yako yote, hatua zako, maneno yako, na hata machozi yako yote, niyasuke pamoja na ‘Ninakupenda’ yangu ndogo, na mwishowe nataka nikuombe utupatie FIAT Yako yenye kutawala, na yenye kuamrisha. Kwa sababu hiyo mimi ninakufuata pamoja na wanafunzi wako. Wakati unapolala usingizi pale ndani ya mashuha, ikiwa ni ishara ya pumziko unalotaka kumpatia mtu yule atakayeishi katika Utashi Wako wa Kimungu, dhoruba kali inawatia hofu Mitume, hali inayowafanya wapige kelele wakilia: “Mwalimu, Utuokoe, vinginevyo tutateketea!”. Yesu Wangu, hicho siyo kitu kingine isipokuwa ni dhoruba itokanayo na utashi wa kibinadamu ambao, unapovumisha mawimbi yake ya kutisha na makali katika bahari ya maisha, huwa inatutishia kutuzamisha. Ewe Yesu Wangu Mleta amani, pamoja na Mitume, na kupitia ‘Ninakupenda’ yangu, ninapiga nami kelele kwa nguvu nikisema: “Mwalimu, utuokoe, vinginevyo tutateketea!”. Tafadhali, amrisha hii dhoruba ya utashi wa kibinadamu na uifanye itulie. Kwa nguvu ya amri ile ile uliyoitoa juu ya ile dhoruba iliyowakabili Mitume, sasa upatanishe utashi wa kibinadamu na Utashi wa Kimungu, ili utuwezeshe tupumzike katika mikono ya uhakika ya ‘FIAT’ Yako ya Juu kabisa.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA KUMI NA TISA

Tumfuate Yesu katika tendo lake la kuingia Yerusalemu na tumwombe atupatie ushindi wa Utashi wa Mungu dhidi ya utashi wa kibinadamu. Kishapo tumfuate katika tendo lake la kuweka Sakramenti mbalimbali.

Ewe Chema Changu Mpendwa, ninakuona unageuka na kuelekea Yerusalemu tena. Mimi nanakusindikiza kwa kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’. Lakini, ni uchungu upi ambao Moyo Wako unakosa kuukabili dakika hii? Unapoingia hapa Hekaluni unaona ni jinsi gani watu wanavyoikufuru? Je imekuwa sasa ni soko badala ya kuwa ni nyumba ya Baba Yako? Hapo Wewe unatwaa mijeledi ya kamba kamba, na kwa taratibu na kwa amri ya kimungu unaanza kupita kulia na kushoto, ukipindua juu na chini mambo yao yote, huku ukiwafukuzia nje wote wale wanaolikufuru Hekalu. Kutokana na nguvu ya kitendo Chako cha kuamrisha, hamna hata mmoja anayethubutu kukupinga, bali wote wanakukimbia. Ewe Yesu Wangu, Mtawala wa Kimungu, ‘Ninakupenda’ yangu inaingia na kuzifunika zile kamba za mijeledi ili uzichukue tena kamba hizo kwa ajili ya kuuchapa na kuufukuzia mbali utashi wetu wa kibinadamu, ambao umelikufuru sana Hekalu lako hai, yaani roho zetu. Lo, hebu uuchape mijeledi kabisa, kiasi kwamba usithubutu tena kutawala bali utoe kabisa nafasi na kiti chake cha mamlaka kwa Utashi wa Mungu.

Ewe Mchumba Wangu wa Mbinguni, ‘Ninakupenda’ yangu inakufuata katika tukio lile la kuingia Kwako kwa shangwe katika mji wa Yerusalemu. Mimi ninagonga mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu juu ya yale matawi waliyoshika makundi ya watu, naugonga juu ya nguo zile wanazotandika njiani mbele ya miguu yako, ninaugonga katika zile kelele na mashangilio ya ‘hosana, hosana’ wanayokuimbia hao makundi ya watu. Ninagonga muhuri huo kwa ajili ya kukuomba ulete ushindi wa Utashi Wako. Ewe Mfalme Wangu Mtukufu, hilo Umbo Lako la Mtekaji, la Mshindaji, linaelekea kuniletea habari njema ya furaha. Lo, hebu unifurahishe! Kwa Binti Mdogo wa Utashi Wako, hebu sema hivi: “Utafika Ufalme wa MAPENZI YAKO YATIMIE hapa duniani kama vile kule Mbinguni” . Mimi sitakuacha kamwe bali nitaendelea kukuchosha kwa ‘Ninakupenda’ zangu hadi pale nitakapokuwa nimekushinda na wewe utakapofikia kuniambia: “Binti Yangu, Wewe umeshinda. Ninakuahidia kwamba Ufalme Wake utashuka hapa duniani. Wewe sasa na unifuate Mimi. Pendo Langu lina linaonja hamu ya kusindikizwa nawe. Maadui zangu wametafsiri vibaya hayo makelele ya makundi ya watu wanapoimba ‘hosana, hosana’ na kwa sababu hiyo wanatafuta namna ya kuondoa uhai wangu. Mimi lakini, kabla sijakufa, ninapenda niweke Sakramenti mbalimbali kama kumbukumbu ya mwisho ya Pendo Langu la kina, kwa ajili ya wana Wangu, na kwa ajili ya uhai wa kudumu kati yao. Na wewe utaendelea kuniomba daima hiyo ‘FIAT’ yangu ya Kimungu, katika kila Sakramenti, ili kusudi watu wawe wanajipatia Ufalme Wake”.

Ewe Pendo Langu, naendelea kukusogea na kujibana kwako. Na pindi unapoweka Sakramenti mbalimbali, mimi ninaingiza ‘Ninakupenda’ yangu katika kila ubatizo, ili kwa nguvu ya kauli hiyo, nikuombe ‘MAPENZI YAKO YATIMIZWE’ kwa ajili ya kila mmoja aliyebatizwa. Hiyo ‘Ninakupenda’ yangu ninairudia tena katika Sakramenti ya Kipaimara, ili kukuomba ushindi wa Utashi wako wa Kimungu ndani ya kila mwana-Kipaimara. ‘Ninakupenda’ yangu inakuwa ni muhuri wa Sakramenti ya Mpako Mtakatifu ili kusudi nikuombe, kitendo cha mwisho cha uhai wa kila aliye kufani, na kiwe katika Utashi Wako wa Kimungu. Ewe Yesu Wangu, hiyo ‘Ninakupenda’ yangu, ninaitia katika Sakramenti ya Daraja Takatifu ili nikuombe tupate Mapadre wa Utashi Wako na wa Ufalme wake ndani yao. ‘Ninakupenda’ yangu inaenea hadi ndani ya Sakramenti ya Ndoa Takatifu ili kukuomba Wewe utujalie familia zilizoundwa na kujengwa katika ‘FIAT’ yako ya Kimungu. Hiyo ‘Ninakupenda’ yangu, inapanda hadi ndani ya Sakramenti ya Kitubio ili kukuomba Wewe kwamba kila Kitubio wanachofanya na kiwe ni kifo cha dhambi na uwe ni uhai wa Utashi Wako wa Kimungu ndani yao.
Ewe Yesu, Uhai Wangu, hiyo ‘Ninakupenda’ yangu haitakuacha kamwe kwani itakuwa na Wewe kwa umilele. Kwa sababu hiyo, ninaiweka kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’ ndani ya kila Hostia ya Sakramenti, katika kila chozi la siri unalolidondosha ndani ya kila Hostia iliyogeuzwa, katika kila tusi na uovu unaotendewa, katika kila fidia unayotoa. Ninaiweka hapo ili, pamoja Nawe, niweze kukuomba kuwa: Ufike Ufalme wa Utashi Wako, hapa duniani kama kule Mbinguni. Ewe, Mpiga-mishale Wangu wa Mbinguni, kutoka katika kila Tabernakulo, uzijeruhi tashi za kibinadamu, eneza minyororo Yako ya Pendo, utumie mbinu zako zote za upenzi ili uweze kuzishinda tashi zote za kibinadamu. Badala yake tunaomba utujalie Utashi Wako, ili kusudi huu utashi wetu ufikie kuwa kitu kimoja na Utashi Wako, na iwe hivyo hapa duniani kama vile kule Mbinguni.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA ISHIRINI

Tumfuate Yesu katika Bustani ya Getsemani na katika maumivu ya Mateso Yake
.

Ewe Yesu Wangu Mteseka, baada ya Wewe kujiweka na kubaki katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, unasambaza uhai Wako katika kila Hostia ili kusudi uweze kushuka na kuingia katika kila moyo, na ili kusudi uwe daima tayari kuwafikia wanadamu mbalimbali wanaokuhitaji. Hilo umelitenda ili kutuambia kwamba: “Mimi sitawaacha bali ninabaki pamoja nanyi nyote, ili kusudi niweze kujenga Ufalme wa Utashi Wangu wa Kimungu kati ya watoto Wangu”. Pendo lako sasa limeridhika. Halafu unaingia katika bahari ya Mateso yako. Hatua za miguu yako zinaelekea kwenye Bustani ya Getsemani. Ninakuona ukianguka kifudifudi ardhini ukisali. Lakini pindi ukisali, unaingia katika mahangaiko na fadhaa, unahema, unaingiwa na maumivu makali sana, na unatoka jasho la damu. Mambo yote yote yanakuja mbele yako. Maumivu yote na dhambi zote, zote zikiwa ni matokeo ya silaha chafu za mauaji zilizopo katika utashi wa kibinadamu ambao unapiga vita dhidi ya Mungu. Ah, ni kweli, utashi wa kibinadamu, kwa kutumia silaha zake, huleta maumivu makali kwa Utashi wa Mungu. Kwa karne nyingi sana utashi huo wa kibinadamu umekuwa ukiuzuia Utashi wa Mungu, na bado unaendelea hata leo kuuzuia. Ewe Yesu Wangu unayekabiliwa na maumivu makali kabisa, huu moyo wangu duni unashindwa kuvumilia unapokuona Wewe umeanguka ardhini na unaogelea na kulowana katika Damu Yako Mwenyewwe. Ni hasa kwa ajili ya hoja hiyo, mimi ninakuomba utupatie Ufalme wa Utashi Wako wa Kimungu hapa duniani, ili kusudi, kwa nguvu ya silaha zake za Kimungu, uweze kuzishinda silaha za utashi wa kibinadamu, uweze kuutesa na kuuingiza katika maumivu makali, hata kuweza, kwa haki kabisa, kulipa kisasi kwa maumivu marefu ya karne nyingi sana, yaliyosababishwa nao huo utashi wa binadamu. Na bila kuupatia tena mwanya wa uhai, Utashi wa Mungu ushike uwanja wake wa uhai katika kila moyo. Na mimi, Ewe Yesu Wangu, ninapokuchukua na kukushika sasa kwa mikono yangu, ninapenda nikutulize kwa kutiririsha kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu’. Ninaitiririsha katika kila tone la Damu uliyomwaga, katika kila umivu, na katika kila hangaiko na kuhema kwako. Katika kila dhambi unayoiona, ninapenda nitengeneze mawingu ya ‘Ninakupenda’, ili kusudi jicho lako lisiweze kuangalia kitu kingine chochote isipokuwa hiyo ‘Ninakupenda’ yangu. Napenda pia kuwa kila picha chafu na ovyo ya madhambi mengi ifukuziwe mbali kutoka kwako. Naiweka hiyo ‘Ninakupenda’ yangu ili kukuomba kwamba Utashi Wako wa Kimungu utawale hapa duniani.

Ewe Yesu, hebu unisikilize: Kama Utashi Wako ungetawala, Wewe usingejikuta katika maumivu mengi na wala usingepata mateso makali yanayokumaliza namna hii. Kwa sababu hiyo, kabla ya kuondoka toka hapa Bustanini, tafadhali unipe kauli yako, umfurahishe huyu Binti Yako Mdogo na uniambie kwamba ushindi wa Utashi Wako wa Kimungu unafika.
Yesu Wangu Mteseka, maadui zako tayari wamekwisha kuingia hapa Bustanini. Wanakushika na kukufunga kwa kamba na minyororo, wanakukanyaga kwa miguu yao, wanakuburuza, wanakupeleka toka baraza moja la mahakama hadi baraza lingine. Ewe Pendo Langu, mimi ninakufuata hatua kwa hatua, ili juu ya maumivu yako yote nikaweke alama ya ‘Ninakupenda’ yangu na ndivyo niweze kukuomba kwamba, kwa kamba zako na minyororo yako, uufunge utashi wetu wa uasi, ili usithubutu tena kuupinga Utashi Wako wa Kimungu, bali badala yake uuache huru kabisa na kuuruhusu uwe unatawala. Ewe Yesu Wangu, maadui zako wala hawatulii, wanakujaza maumivu makali, wanakutemea mate hata kuziba uso wote. Wanakushitaki kama mhalifu wa jinai, na wanakuhukumu kufa na wanakufunga katika mahabusu. Ewe Mfungwa Wangu Yesu, mimi sitakuacha. ‘Ninakupenda’ yangu inafunika yale mate yote waliyokutemea ili kusudi Wewe usiwe unapata harufu ya mate hayo, bali upate harufu ya ‘Ninakupenda’ yangu. Nataka nikufunike mwili mzima na hiyo ‘Ninakupenda’ yangu ili kusudi katika maumivu yako yote, na katika matusi wanayokutukana, ‘Ninakupenda’ yangu iwe inakutetea na kukulinda, iwe inakunogesha, na iwe ni silaha itakayowafukuza na kuwakimbiza maadui zako na kuwaongoa wote kwa ajili Yako. Na hapo ndani ya gereza hilo jeusi kabisa wanamokufungia, ‘Ninakupenda’ yangu iwe ndiyo mwanga wako na msindikizaji wako anayekuomba utufungulie kutoka gereza la utashi wetu na utufanye sisi kuwa wana huru wa FIAT Yako ya Kimungu.

Ewe Yesu Wangu unayepigwa mijeledi, kwa muda fulani wanakutoa nje ya gereza ili muda huo wao waweze kubadilisha na kukuandalia mateso makali zaidi na ili wafanikishe kutekeleza nia yao ya kikatili ya kukuua. Wanakuburuza na kukupeleka kwenye mabaraza mengine ya mahakama, yaani kwa Pilato na kwa Herode. Huyu Herode ndiye anakudhihaki na kukuchezea hata akakuvalisha kitambaa cha watu vichaa. Tendo hili lilikuletea uchungu mkali usiowahi kusikika. Ewe Pendo Langu, Unapata mateso yalioje! Kwa njia ya ‘Ninakupenda’ yangu, ninataka nikushonee vazi lililoandikwa ‘Ninakupenda’ yangu ya mwanga, ili iwatie kiza hao adui zako, hata wasiweze kukutesa zaidi. Badala yake wawe wanakutambua Wewe na wawe wanakuomba ili utuondolee huu ukichaa wetu ambamo utashi wa kibinadamu umetutumbukiza. Na kwa kutufanya kuwa vichaa, unatufanya tupoteze akili yetu ya kutambua kitu kilicho chema na cha kweli, yaani kutekeleza Utashi Wako wa Kimungu.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA ISHIRINI NA MOJA

Tunaendelea kumfuata Yesu katika maumivu ya Mateso yake.

Ewe Yesu Wangu unayeumizwa sana, sasa wanakupeleka kwa Pilato tena na kule yanakusubiri mateso mengine mapya. Wanatoa hukumu ya kukupiga mijeledi. Wanakuvua nguo zako, wanakufunga kwenye nguzo ili waweze kukupiga mijeledi kwa ukatili wote. Mimi ninashika na kukumbatia nyayo zako za Kimungu ili niweze kutia alama ya ‘Ninakupenda’ yangu juu ya kila pigo unalolipata, juu ya kila kipande cha nyama zinazoraruliwa toka mwilini mwako, na juu ya kila jeraha wanalokusababishia mwilini mwako. Ninataka kupiga kelele na kulia ‘Ninakupenda’, na ninakuomba utuvue sisi lile vazi la utashi wa kibinadamu na utuvalishe lile vazi la Utashi Wako, ili kusudi tusiwe tunaonja wala kuona kitu kingine isipokuwa FIAT Yako ya Juu. Yesu Wangu uliyepigwa mijeledi, adui zako bado hawajaridhika. Kutokana na majeraha mengi hutambulikani tena. Moyo wangu unashindwa kuvumilia. Ningependa nikuokoe kwa njia ya kauli zangu za ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’ na ninapenda kukuomba utupatie FIAT Yako itakayotawala hapa duniani, ikiwa ndiyo nguvu pekee itakayositisha maumivu yako. Vinginevyo hayataweza kabisa kukoma, na mimi nitaendelea kuwa na uchungu ninapokuona Wewe unavyoteseka. Kishapo, wanakutia taji la miiba. Wanakuvalisha kipande cha kiraka cha nguo ya kifalme, wanaweka kipande cha mwanzi mkononi mwako, na ndivyo wanakutendea kama kinyago cha dhihaka. Ewe Yesu Wangu, Uhai Wangu, ninapenda hii ‘Ninakupenda’ yangu ipambe na kuremba kila mwiba unaotoboa Kichwa Chako, na ninakuomba utuondolee mbali hili taji la dhihaka, ambalo tumevalishwa na utashi wetu wa kibinadamu, utuvue na kiraka cha kitambaa cha kifalme cha utashi huo wetu, unyang’anye hiyo fimbo ya mwanzi toka mikononi mwetu, fimbo iliyo ni ishara ya matendo mengi yaliyo tupu na bila thamani yoyote, fimbo inayotupatia amri na maagizo ya kuchekesha na ya dhihaka tu. Badala yake, Ewe Yesu, utuvalishe taji la Utashi Wako wa Kimungu, utuvalishe kitambaa safi cha kifalme kitakachotutambulisha sisi kuwa watoto wake wa kweli. Utupatie mkononi mwetu fimbo ya kweli ya utawala na ya mamlaka ya FIAT Yako tunayotaka itawale na kuamrisha roho zetu.

Ewe Yesu, Mfalme Wangu, ‘Ninakupenda’ yangu inaendelea kulifuata Pendo Lako. Katika kukutana na kuunganika kuwa kitu kimoja, huunda pendo moja tu, kiasi kwamba mimi nafikia kuwa na pendo kubwa sana chini ya mamlaka yangu, hata linakufanya Wewe uwe unalisikia pendo langu wakati ule unapokuwa unasikia ile kauli ya kukuhukumu ufe, yaani pale walipopiga ile kelele ya ‘msulibishe, msulibishe’. Kwa upande wangu, mimi ninayageuza makelele hayo ya ‘msulibishe!’ na badala yake nitapiga makelele ya ‘Ninakupenda’ yangu ndani ya kila sauti, na juu ya kila mdomo. Nitasema: “Usulibiwe utashi wa kibinadamu ili Utashi Wako upate kutawala!”. Na kwa maumivu uliyokuwa unayapata wakati ule unapohukumiwa kifo, tunakuomba utuokoe kutoka kile kifo tunachosababisha juu ya FIAT Yako katika roho zetu, na fanyiza kwamba utashi wetu ufe na badala yake Utashi Wako wa Kimungu ufufuke, uamrishe, na ujenge Ufalme Wake katika matendo yetu yote.

Ewe Pendo Langu, moyo wangu unaelemewa na uchungu ninapokuona ukiupokea na kuubeba Msalaba. Wewe unaukumbatia na unauweka juu ya Mabega yako. Oh, ni jinsi gani ningependelea kuufunika Msalaba mzima kwa kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu’. Halafu ni jinsi gani ningependa nikuombe kuwa, kwa nguvu ya Msalaba Wako, machungu yale yote, ambayo Pendo Lako linayapeleka kwa wanadamu, yaweze kuleta nguvu ya FIAT Yako, itakayowaandaa wanadamu kuweza kuipokea himaya yake. Oh, ni jinsi gani ningependa nipige kelele katika kila umivu unalolipata, na katika kila tone la Damu Yako. Napenda niseme: FIAT Yako ifike!. Katika kila anguko, katika kila moja ya nywele zako zilizolowa kwa Damu Yako, katika kila kitendo cha kusukumwa ovyo ulichokipata ninasema: Ninakupenda, Ufike na Ufalme wa Utashi Wako!.
Yesu Wangu unayehema, unayekanyagwa kwa miguu, unayeburuzwa ardhini, sasa unawasili juu ya kilima cha Kalvario. Wanakuvua nguo zako, wanakulaza juu ya mti wa Msalaba, na kwa ukatili usiosemekana wanakupigilia Msalabani. Ninapenda kutiririsha ‘Ninakupenda’ yangu juu ya viungo vyote vya mwili wako vilivyoumizwa na kujeruhiwa, juu ya mifupa yako iliyotetereshwa na kulegezwa, juu ya matobo yote uliyopata wakati misumari ilipopigiliwa. Katika maumivu yako yote, ninapenda nitie kwanza kabisa mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu, na papo hapo napenda nikuombe utuvue sisi mambo yale yote yanayozuia Utashi Wako wa Kimungu usifufuke ndani ya mioyo yote na kuweza kueneza Ufalme Wake katika dunia yote.

Ewe Yesu Msulibiwa, pale Msalabani juu, unahema na na unateseka vibaya sana. ‘Ninakupenda’ yangu igonge mhuri wa kusitisha mihemuko yako, mhuri wa kusitisha maumivu makali na ya mateso ya Moyo Wako, na usitishe miali ya moto inayouunguza huo Moyo. ‘Ninakupenda’ yangu na iwe ni kiyoyozi chako, na izime kiu chako cha moto. Kwa mhuri huo wa ‘Ninakupenda’ ninagonga alama juu ya kila neno ulilowahi kutamka pale Msalabani. Katika hiyo ‘Ninakupenda’ yangu, ninapokea pumzi yako ya mwisho ili nikuombe, kwa ajili ya maumivu yale makali uliyoyapata pale Msalabani, utujalie sisi neema ya kuungua kwa kiu cha kuishi katika Utashi Wako wa Kimungu. Utashi Wako uliokuwa umeshuhudia mahututi yako katika utashi wetu, sasa ushuhudie kifo cha utashi wetu na FIAT Yako ifufuke katika mioyo yote, ipate ushindi na iweze kujieneza katika kizazi chote cha binadamu na itawale hapa duniani kama vile kule Mbinguni.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA ISHIRINI NA MBILI

Ndani ya ‘Ninakupenda’ yetu tunafungilia Ubinadamu Mtukufu wa Yesu, uliokufa. Pamoja Naye tunateremka kwenda Limbo. Na pale, tukiwa pamoja na Malkia wa Mateso, na pamoja na roho takatifu zile zote, kwa pamoja tunamwomba kuwa Utashi Wake wa Kimungu upate ushindi kati ya wanadamu.

Ewe Pendo Lako, ninakuona umekwisha kuzimia. Oh, ni jinsi gani ningependelea niweze kuzimia pamoja Nawe, lakini sikubahatika kujaliwa hilo! FIAT, FIAT!..... Ninapenda nikupokee mikononi mwangu ili kusudi niweze kufungilia huo Ubinadamu Wako Mtukufu ndani ya ‘Ninakupenda’ yangu. Kwa njia hiyo, katika kila kitu utakachokuwa unaona, uwe unaiona ‘Ninakupenda’ yangu, katika kila unachokisikia uwe unaisikia ‘Ninakupenda’ yangu, uwe unaigusa ‘Ninakupenda’ yangu. Hii ‘Ninakupenda’ yangu haitakuacha kamwe: Utashi Wako wenyewe ndiyo uhai wa ‘Ninakupenda’ yangu. Lakini je unajua ni nini anachotamani huyu msichana mdogo? Anataka kwamba, Ule Utashi wa Mungu ambao Wewe uliupenda na uliutekeleza katika maisha yako yote ya hapa duniani, huo sasa uufanye ujulikane kwa wanadamu wote, ili kusudi wote wapende na watekeleze Utashi Wako hapa duniani kama vile kule Mbinguni. Huyu msichana mdogo anataka akushinde na kukuteka katika pendo ili kusudi Wewe utoe Utashi Wako wa Kimungu kwa wanadamu wote. Lo, Ewe Chema Changu, ebu ukafurahishe haka kasichana kadogo duni, ambako hakatafuti kitu kingine, isipokuwa kile unachokitaka Wewe, yaani, kwamba Utashi Wako ujulikane na utawale hapa duniani pote.

Ewe Yesu uliyekufa, wakati ninapokuwa nimeufungilia Ubinadamu Wako katika kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’, nimekutengenezea namna ya mazishi katika ‘Ninakupenda’ yangu. Ninakuomba na Wewe uuzike utashi wa kibinadamu ili usirudie kuishi tena. Mimi pamoja na Mama Yako Mteseka, aliye pia ni Mama Yangu, ninapenda kuambatana nawe kwenda Limbo. Ninakusindikiza katika ‘Ninakupenda’ yangu. Pale nashuhudia tukio na hali ya kustaajabisha sana: Hapa mahali patakatifu, namwona Baba yangu Adamu, namwona Abrahamu, Mababu na Manabii wote, na hata Mpendwa Mtakatifu Yosefu na watu wote wema wa Agano la Kale. Oh, ni jinsi gani wanavyofurahia kukuona! Halafu, huku wakianguka kifudifudi penye miguuni Yako mitakatifu, wanakuabudu, wanakupenda, na wanakushukuru. Lakini inaelekea kuwa sherehe yao haijakamilika bado. Basi wote kama kwaya ya pamoja, na kwa sauti moja, kuanzia na yule Baba wa kwanza Adamu, wanakuambia: “Tunakushukuru kwa yale yote uliyotenda na kuteseka kwa ajili yetu sisi sote. Maadam umekwishatekeleza na kutimiza ile sehemu ya kwanza, yaani sehemu ya kutukomboa, sasa tunakuomba umalizie na kukamilisha ile sehemu ya pili, yaani, ufanye Utashi Wako wa Kimungu utawale hapa duniani kama kule Mbinguni”.

Ewe Pendo Langu, je husikii hizo sauti nyingi za wapenzi wako? Hata mwenyewe Malkia wa mateso anakusihi, na mimi nikiwa pamoja naye tunasema: Ufike, ufike hapa duniani Ufalme wa Utashi Wako. Fanyiza kuwa watu wote waujue Utashi Wako Mwabudiwa. Leo, siku hii ya kifo chako, ndiyo siku ya ushindi Wako mbalimbali, ndiyo siku ya sherehe yako ya ushindi. Je inawezekana kweli kwamba hupendi kunijalia sherehe ya ushindi wa Utashi Wako wa Kimungu dhidi ya utashi wa kibinadamu? Basi sasa, hebu nisikie sauti Yako tamu mno kabla hujatoka hapa Limbo. Unijalie kwamba Utashi Wako utawale na ushike himaya yake hapa duniani kama kule Mbinguni.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA ISHIRINI NA TATU

Katika ‘Ninakupenda’ yetu, hebu tuambatane na lile tendo la Ufufuko Mtukufu wa Ubinadamu Mtukufu wa Yesu. Tufuatilie pale ambapo Mfufuka atakuwa anamtokea Mama Yake na atakapowatokea Wanafunzi. Pale tutamwomba kwamba Utashi Wake wa Kimungu ujulikane kwa mapadre wa Kanisa Lake.

Ewe Yesu Wangu Mshindi, ninakuona unapotoka kule Limbo, ukiwa umetangulizana na lile jeshi lote la roho zile za watu wenye haki. Unaelekea na kurejea kaburini ili kusudi upate kushinda mauti na ili ukaufufue Ubinadamu Wako Mtukufu. Ni dakika tukufu ilioje! Kwa sababu hiyo ninataka niweke ‘Ninakupenda’ yangu juu ya kaburi wakati wa tendo lako la kufufuka, niiweke juu ya ule mwanga, na juu ya ule utukufu unaokuzunguka. Nataka nikuombe ufufuko wa Utashi Wako wa Kimungu ndani ya utashi wa binadamu. Sisi sote tufufuke ndani yako. Je Wewe hutaki kunipatia kile kilichobebwa ndani Yako? Basi mimi ninakuomba, kwa nguvu ya Ufufuko Wako, uvuvie juu ya kila mwanadamu, na kwa pumzi yako yenye maweza yote, uteremshe utashi wa kibinadamu, ili kusudi Utashi Wako ufufuke katika utukufu na katika hali ya ushindi. Ewe Yesu Wangu Mfufuka, pindi ulipofufuka hukutoka na kwenda Mbinguni. Tendo hilo linanithibitishia kwamba, siku zile 40 za ufufuko, ulizokaa bado kati ya wanadamu, ni uthibitisho wa Ufalme wa Utashi Wako kati ya wanadamu. Basi mimi sikuachi kamwe. Katika ‘Ninakupenda’ yangu, ninakufuata hatua kwa hatua katika kitendo chako cha kujitokeza kama Mfufuka kwa Mama Yako. Na kwa ile furaha mliyoipata na kuifurahia ninyi wawili, mimi pamoja na Malkia mwenye mamlaka, tunakuomba FIAT Yako. ‘Ninakupenda’ yangu inakusindikiza katika lile tendo lako la kujitokeza kwa Magdalena na kwa Mitume. Ninakufuata ili kukuomba kwamba Utashi Wako wa Kimungu ujulikane kwa mapadre ambao ndio Mitume wapya. Nao hao waufanye ujulikane kwa dunia nzima.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA ISHIRINI NA NNE

Hebu tuziite Mbingu na dunia ziambatane na Yesu katika tendo Lake la Kupaa Mbinguni. Tendo hilo tunaliunganisha kwa pete ya ‘Ninakupenda’ yetu huku tukiomba kwamba Utashi wa Mungu utawale katika dunia nzima.

Mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu unaendelea kukufuata katika matendo yote yale uliyoyafanya kama Mfufuka kati ya Wafuasi Wako.

Tunaziita Mbingu na dunia zikusindikize katika tendo Lako la Kupaa Mbinguni, na katika tendo Lako la kufungua milango ya Mbingu ambayo, kwa muda wa karne nyingi sana, ilikuwa imefungwa kwa ubinadamu ulio duni.

Na juu ya ile milango ya milele, mimi ninapenda kuweka pale mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu, na ninakuomba ile Baraka uliyokuwa umetoa kwa Wafuasi Wako wote waliokuwepo katika ile sherehe ya Kupaa kwako Mbinguni, na pia ninakuomba ubariki tashi zote za kibinadamu, ili kusudi ziweze kutambua manufaa makuu ya kuishi katika Utashi Wako.

Na kwa lile Pendo ambalo kwalo ulitufungulia milango ya Mbinguni, utujalie kwamba Utashi Wako wa Kimungu ushuke kutoka milango hiyo hiyo.

Ushuke na kuja kutawala hapa duniani kama vile unavyotawala kule Mbinguni.

Ewe Pendo Langu, Wewe sasa umekwisha kuwa Mbinguni. Endapo mimi sitaona kwamba ‘Ninakupenda’ yangu ndogo imeweza kukusadikisha Wewe kuuleta duniani Utashi Wako Mwabudiwa, basi mimi sitafanya kitu kingine, isipokuwa nitakutengenezea minyororo ya ‘Ninakupenda’ kati ya Mbingu na dunia.

Kwa minajili hiyo, Wewe uniachie milango ikiwa wazi daima, ili kusudi niwe na uhuru wa kuja na kuingia hadi miguuni pako na hadi mikononi mwako, kwa lengo la kukushonelea kwa pete za mnyororo wa ‘Ninakupenda’ yangu.

Nina uhakika kwamba mwishowe ni mimi nitakushinda Wewe na hatimaye Wewe utanipatia kile ambacho na Wewe unakitaka, yaani, kwamba Utashi Wako wa Kimungu utawale katika dunia nzima.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
Mtumishi wa Mungu
Luisa Piccarreta
inti Mdogo wa Utashi wa Mungu

“Ee Yesu, miguuni pako nakuletea uabudu na utiifu wa familia yote ya wanadamu. Ninaweka ndani ya Moyo Wako ile kauli ya ‘Nakupenda’ kutoka kwa watu wote. Juu ya Midomo Yako nakupigia busu langu, ili kukubandikia mhuri wa busu la watu wa vizazi vyote. Kwa mikono yangu nakukumbatia, ili kukubana kwa kumbatio la mikono ya watu wote, kwa ajili ya kukufikishia utukufu wa matendo yote ya wanadamu”

(Kutoka: KITABU CHA MBINGU, Juzuu Na. 12 - Mei 22, 1919)
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 28
Kwa Mheshimiwa Padre Msaidizi

Fiat

Mheshimiwa sana Padre Msaidizi,

Kutoka kwa Mwalimu mwema Angela La Stella nilipata karatasi lako lililokuwa na ombi lako la kutaka nikusaidie kidogo kwa sala zangu, na kwa Komunyo yangu Takatifu nk. kwa ajili ya kazi zako za kipadre.

Basi, tangia tarehe 20 Oktoba hadi leo hii, katika kila kitu nilichoweza kutekeleza katika umasikini wangu, nimekuwa ninaweka nia ya kutenda kwa ajili yako, yaani Misa Takatifu zote, Komunyo Takatifu zote na mengineyo.

Na ili nia yangu hiyo iweze kuwa na thamani zaidi, na ili iweze kukuletea wewe matunda ya utakatifu wa kweli, matunda ya neema za kushangaza na usizotegemea, nilimwomba Yesu awe anatenda kila kitu pamoja nami ili pamoja na zawadi za kwangu, niweze kukutolea zawadi za Yesu Mbarikiwa.

Nilifanya hivyo kusudi Upadre wako ujaliwe neema hizo zaidi na zaidi.

Kutokana na hilo, ninapenda kutumia nafasi hii kukutumia Heri nyingi sana kwa Sikukuu ya Somo wako na ninamwomba mpenzi Yesu abebe na kukuletea Yeye Mwenyewe zawadi hizo.

Zawadi anazokuletea kama Heri zangu ni hizi: ‘FIAT’ ndani ya moyo wako, ‘FIAT’ katika maneno yako, na ‘FIAT’ katika akili yako, ili hatimaye hiyo FIAT iiongoe nafsi yako yote na kuiumba upya nafsi hiyo hata iwe ni kitendo kimoja tu cha Utashi wa Mungu.

Na kutokea hapo wewe uwe ni mtu unayebeba Utashi wa Mungu na kuupeleka kwa watu wote.

Ni Utashi huo ndio unaoweza kuingiza amani, umoja, na utakatifu ndani ya watu wote.

Tunaonja sana hitaji kali kabisa la kupata utakatifu wa kweli, hasa hasa ndani ya Padre.

Na ni ‘FIAT’ ya Mungu peke yake ndiyo yenye kuweza yote, kwa vile ndiyo inayomiliki maweza yote.

Maweza hayo yapo katika nguvu yake na uwezo wake wa uumbaji.

Ndiyo inayoweza hatimaye kuleta na kuingiza ndani yetu ngazi na daraja la kweli la utakatifu.
Nakuomba na ninajikabidhi katika sala zako takatifu.

Na sasa, kwa heshima, nikibusu shavu lako la kulia, na nikipiga magoti mbele yako ninakuomba sana baraka yako ya kibaba. Ndimi,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu