Utashi wa Mungu na Upendo wa Mungu - Luisa Piccarreta
42 subscribers
311 photos
56 files
688 links
Fahamu kuhusu kutimia kwa Sala ya Baba Yetu kupitia Maandishi ya Mtumishi wa Mungu Luisa Piccarreta, Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - Kuishi Utashi wa Mungu
Download Telegram
SAA YA KWANZA

Tuufuate Utashi wa Mungu katika Matendo Yake yote, ili tukeshe pamoja nao na ili tuupate Uhai Wake wa Kimungu ndani yetu. Tuufuate katika tendo la kuumba Mbingu na Jua.

Yesu, Uhai Wangu, pigo la moyo wangu duni, pumzi ya roho yangu ndogo, makao ya akili yangu, udogo wangu wote unazamia ndani Yako, unapotelea ndani Yako. Mimi ni mtoto mchanga ambaye hajaweza kutembea bado. Ninakujongea Wewe, najibana kwenye mkono wako, na pamoja nawe nataka niingie katika Mwanga ule usiokoma wa Utashi Wako wa Kimungu.

Haya basi tazama, Baba wa Mbinguni tayari anatamka ile FIAT ya kwanza, na ndipo anafungulia mwanga mkubwa kabisa ambao unaangaza bila kikomo cha mipaka. Ewe Yesu Wangu, lo, unijalie roho yangu ipate nguvu yote, maweza, utakatifu, na mwanga wa FIAT yako abudiwa, ili mimi nisiweze kusikia kitu kingine tena ndani yangu isipokuwa Uhai wake hiyo FIAT! Nitakapokuwa nimetajirishwa tayari na Uhai wa hiyo FIAT, nitaweza kukumbatia na kubeba kila kitu, nitaweza kujaziliza kwenye kila kitu, na hata nitaweza kuiteka na Yenyewe na kuishusha ifike duniani kusudi irejee kwa shangwe kuja kutawala kati ya wanadamu!

Kwa hiyo basi, ewe Pendo Langu, uniache niendelee na hija yangu katika Utashi Wako, ili niendelee kufanya ziara ya kufuatilia Matendo Yake yote. Oh! Ni nzuri na inapendeza ilioje kuutafakari Utukufu Mkuu na wa Juu, ambao kwa kutamka FIAT moja tu unaweza mara kulipanua na kulisambaza hili anga samawati likiwa limejaa miliadi ya nyota zinazometameta kwa mwanga wao! Anapotamka FIAT nyingine anaumba jua; anapotamka nyingine tena anaumba upepo, hewa, bahari, na vitu vyote vilivyomo. Na anaviumba na kuvileta vyote hivyo katika mpangilio na uuwiano unaovutia na kuiteka roho ya yule anayetazama.

Ee Yesu Wangu, Chema Changu! Oh, mimi napenda nilitwae na kulifanya la kwangu, hilo Pendo lililobebwa na FIAT yako ya Kimungu wakati ikiumba anga lenye kufurika na nyota. Nataka niweze pia, kwa upande wangu, kupanua na kueneza anga langu la pendo ndani ya FIAT yako yenye Enzi. Kwa njia hiyo, ninapoijaza anga yote kwa pendo langu, nitapenda nitoe sauti yangu kwa kila nyota inayokuwepo ili nayo irudie pamoja na mimi kusema: “Yesu, Mimi ninakupenda!...... Ebu Ufalme Wako ufike hima hapa duniani!..... Utashi Wako wa Kimungu na upewe Utukufu kwa daima!...... Mimi ninauabudu na ninautukuza udumivu wako wa Kimungu na huo Uwepo Wako usiotetereka. Ndivyo hivyo vinavyoleta udumivu wa wanadamu katika mambo mema, na ndivyo pia vinawaandaa vema wanadamu wawe tayari kuupokea Ufalme wa Utashi Wako”.

Ewe Pendo Langu, naendelea na ziara yangu na ndipo ninafika ndani ya jua: Hapo ninakuwazia Wewe ukiwa katika dakika ile ambapo FIAT yako, toka Kifuani mwa Umungu, ilifungulia nje na kutoa mwanga mkubwa kabisa na kutengeneza tufe la jua, yaani ile sayari ambayo ndiyo ingekumbatia na kuibeba dunia pamoja na vitu vyote vinavyokaa ndani yake. Kwa mwanga huo jua lilitoa, kwa kila kimoja ya viumbe, busu lake la mwanga na la pendo. Na kwa njia ya busu lake hilo, kila kitu kiliweza kurembwa, kurutubishwa, kupewa rangi yake, kutajirishwa na kupambika.

Toka ndani ya Umungu Wako, FIAT yako ililifungulia na kulitolea nje hilo jua, yote kwa ajili ya kuonyesha tu Pendo lako kwangu mimi. Kwa minajili hiyo, mimi nataka, ndani yangu, nipate mwanga wake wote, joto lake lote na matokeo yake yote. Hilo ni kwa lengo kwamba, hata mimi niweze kukutolea Wewe, jua langu la kukuza, la kutukuza, na kwa njia yake niweze pia kubariki na kuusifia huo Mwanga wa Milele, kusifia Pendo Lako lisilozimika, Uzuri Wako pekee, Utamu Wako usiokoma na ladha zako zisizohesabika. Ndiyo kweli, Ee Yesu, mimi ninapenda nikukumbatie kwa nguvu ya huohuo mwanga wa jua, napenda nikupe mabusu yangu motomoto pamoja na ujotojoto wake, na kwa sauti yangu napenda kuimbilia huo mwangaza wake wote na pia kuimbilia matokeo yake yote. Nafanya hivyo kusudi nikuombe Ufalme wa FIAT yako kuanzia kule juu kabisa, kwa sayari ya hilo jua hadi kule chini kabisa, ambako mwonzi wake huwa unafikia.
Ewe Pendo Langu, je Wewe huonji jinsi Utashi Wako unavyopenda kuyapasua hayo mapazia ya mwanga ili uweze kuteremka na kuja kutawala kati ya wanadamu? Na mimi, nikiwa juu ya mabawa ya uangazo wa hilo jua, ninakujia ili kukuomba utupelekee haraka huo Ufalme wa FIAT yako. Kutoka pale katikati ya hilo jua, mimi ninakuomba uteremshe mng’ao wake ndani ya moyo wa binadamu ili kuwaangaza kwa Neema Yako, na ili kuwajalia Pendo Lako lenye kuunguza ndani yao chochote kile kilicho kibovu kisichoendana na Utashi Wako. Oh, ni kweli, endapo Mwanga Wako utateremshwa hadi kuwafikia wanadamu, basi uzuri wa Kimungu utawamulika ndani yao, hasira na uchungu vitakoma, na wote watajipatia utamu wako na hivyo uso wa dunia utafanywa kuwa mpya.

Ni kwa jinsi gani ninavyofurahia, Ewe Uhai Wangu, kuweza halafu kukuambia hivi: “Umenipa jua na mimi ninakupa jua! Mimi ninayo sayari chini ya mamlaka yangu, sayari ambayo inakuomba Wewe ulete Ufalme wa FIAT Yako. Je Wewe unataka kuugomea huo mwanga mkubwa ambao unakuomba? .......” . Kwa hiyo basi, Ee Yesu, fanya haraka hima! Hilo jua ndilo mjumbe wako wa Kimungu. Haya basi, Ewe Pendo Langu, fanyiza kwamba mwangaza wake, utakapowagusa tu wanadamu wote, papo hapo uufunue Ufalme wa FIAT Yako, ufunue utakatifu wake, na ufunue lile tamanio la kuwaona wanadamu wakipenya ndani yake FIAT kwa ajili ya kuwafanya wafurahie na wawe watakatifu.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba..
SAA YA PILI

Tuufuate Utashi wa Mungu katika tendo la uumbaji wa bahari na wa upepo

Ewe Yesu, Uhai Wangu, FIAT Yako inanisukuma, na kwa hiyo basi ona, mimi nipo hapa tayari kwa ajili ya kufuatilia lile tendo la kuumba bahari. Lakini ni nini hicho ninachosikia? Ninasikia sauti ya mbubujiko wa maji unaoendelea. Ni ishara ya ujimudu Wako wa tangu milele na usiokoma. Mimi naingia ndani ya huo ujimudu wa Kimungu, ujimudu unaoendelea bila kukoma, ujimudu unaoleta uhai kwa watu wote. Ninaufanya huo uwe ni ujimudu wa kwangu ili hatimaye niweze kuugawa wote kwa watu wote kwa ajili ya kukuomba Wewe Ufalme wa Utashi Wako, kwa niaba ya watu wote.

Ebu ona, Ewe Yesu, nikiwa na FIAT Yako ninateremkia kwenda kilindini mwa bahari na popote ninapopita na kuona mtikisiko au ujimudu, ninapoona uhai fulani, ninapoona mbubujiko wowote wa maji, hapo hapo ninatoa mlio wangu usiokoma nikisema: “Ninakupenda Wewe, ninakuabudu, ninaku-shukuru, ninakutukuza, na ninakushangilia!”. Kwa sauti yangu ninapiga kelele kushinda ule mbubujiko wa maji ya bahari, kupita kelele za maji yanayotikiswa na samaki, kupita kelele zozote za mawimbi madogo na makubwa ya maji, na katika kila nafasi ninapaza sauti kuomba Ufalme wa FIAT Yako! Je, Ee Yesu, Wewe husikii jinsi matone yote ya maji, katika mbubujiko wao, sawa na kelele za sauti nyingi sana, nayo yakisema: “FIAT, FIAT, FIAT!”. Na je husikii jinsi mawimbi ya maji na makelele yao makali yanavyopiga na yanavyojaribu kupasua na kufumua tumbo la bahari, na hivyo kutaka kulazimisha Utashi Wako utoke nje, uwameze ndani yake na ukawatawale wanadamu wote, na ili hatimaye wanadamu hao waweze kuruhusu FIAT ya Kimungu itawale ndani yao wenyewe ?

Ndani ya bahari hii, ninapoona na kusikia mbubujiko wa maji yake, mimi nakuja kusifia na kupenda huo ujimudu Wako usiokoma; katika mawimbi yake yanayopanda juu sana, ninapenda kutafakari juu ya Usafi ule usio na doa lolote; katika ukuu na upana wa bahari, ninatafakari Neema Yako na Ukuu Wako unaopita kila kitu, Ukuu unaoficha kila kitu. Nikiwa na hisia hizo zote, ninakuomba Wewe Ee Yesu, umfanye binadamu awe mtu mwadilifu, awe na nguvu, na awe msafi rohoni. Umjalie aweze kuishi amefichama ndani ya Utashi Wako Mtakatifu, lakini papo hapo akiwa anahusiana nao kikamilifu, ili aweze kutembea daima katika ujimudu uleule wa Kwako ambamo alikuwa ametokea!

Ewe Yesu Uhai Wangu, sasa napenda nitafakari juu ya Upepo na ubaridi wake unaoburudisha, juu ya pepo kali na athari zake za kimbunga, na za kisulisuli, juu ya pepo ambazo huwa zinaathiri, zinabomoa, zinazotulia pengine, halafu zinapanda na kuvuma, zinazoa na kuhamisha vitu. Hapo ninawaza juu ya kupenda, juu ya kusifu, juu ya kutukuza, na juu ya kushangilia himaya na mamlaka ambayo Utashi Wako unayo juu ya Upepo. Kuna wakati upepo unalia kimya kimya na kuna wakati upepo unapiga makelele kwa nguvu. Ni Pendo la Utashi Wako wa Kimungu kwa Yule anayelia katika upepo akiwa anatamani ajulikane. Na pale anapoona kuwa hasikilizwi na mtu, huyo anapiga makelele, anazungumza kwa sauti za ajabu ajabu. Ni kwa vile Yeye anataka atawale na kwa vile anadai kuwa na himaya yake mwenyewe kati ya wanadamu. Kwa kutumia mamlaka ya Utashi Wako Mkuu wa Juu, fanyiza kwamba Ufalme Wake FIAT Yako ufike kati ya wanadamu, na ukatawale juu yao wanadamu, kwa namna kwamba pasitokee kamwe mwanadamu anayeweza kuthubutu kuipinga hiyo FIAT. Kwa nguvu ya ubaridi wake mwanana, uwavute na kushawishi hao wanadamu. Tumia nguvu ya mabavu yake na ya mhemuko wake ili kuubomoa utashi wa kibinadamu ndani yao ili kusudi uweze kuwainua na kuwateka waingie katika Utashi Wako. Uwawezeshe hao wanadamu kusikia vilio vyako vyote vinavyoendelea, uwawezeshe pia kuelewa kuwa Wewe unataka kutawala kati yao. Kama utaona kuwa husikilizwi nao, basi piga kelele, zungumza kwa sauti kali ukitumia sauti zako zile za ajabu na za mafumbo, hata masikio yao yapate uziwi kutokana na kelele hizo. Hatimaye fanyiza kwamba kila mtu afikie kutambua na kukiri kwamba huo Utashi Wako Mtakatifu ndio Bwana Mkuu wake.
Kwa hiyo basi, Ewe Pendo Langu, hata mimi sasa napenda kukimbia juu ya mabawa ya huu upepo kusudi, kwa kupitia upepo huo, niweze kukuomba ujio wa Ufalme wa FIAT Yako. Katika kila wimbi la upepo huo napenda nipeleke, busu la FIAT hiyo, kwa kila mwanadamu. Niwapelekee mapapaso yake, na pia makumbatio yake matamu.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba..
SAA YA TATU

Pindi tunapofuata Utashi wa Mungu , tunaruka juu ya dunia nzima tukipita kugonga mhuri wa kauli yetu ya ‘Nakupenda’ juu ya kila kitu kilichoumbwa
.

Ewe Yesu Wangu, Moyo Wangu, Uhai Wangu. Uumbwa wote umekunywa na kunyonya hadi ukajaa Utashi Wako mwabudiwa. Matendo ya Utashi Wako ni mengi wala hayahesabiki katika vitu vyote vilivyoumbwa. Kwa sababu hiyo mimi, ili niweze kuyafuatilia matendo hayo, naamua kuanza kufanya hija kuzunguka ulimwengu mzima. Nafanya ziara kuzunguka kwenye hewa na pale ndani yake ninagonga mhuri wangu wa ‘Ninakupenda’, ili kukuomba kuwa, wanadamu hawa, wakati wanapopumua, wawe wanavuta hewa ya huo Uhai unaotawala ndani ya Utashi Wako.

Kwa kauli yangu ya ‘Ninakupenda’, ninapenda nibariki, nitukuze, na nipige muhuri juu ya utaratibu na harmonia iliyopo katika Uumbwa wote, ili niwafikishie wanadamu wote ule mpangilio na harmonia ya Ufalme wa Utashi wa Mungu. Nataka niruke juu ya dunia yote na kupita kugonga muhuri wangu wa kauli ya ‘Ninakupenda’, iwe juu ya unyasi mdogo kabisa, juu ya vimimea vyovyote vidogodogo, juu ya maua yote, juu ya miti yote iliyo mirefu kabisa, juu ya vilele vya milima, na hivyo hivyo hadi kule kwenye vilindi vyeusi totoro. Nitapita naruka na kubariki vyote hivyo ili kusudi nikuombe ueneze popote Ufalme wa FIAT Yako. Nitaviimbilia vitu vyote na nitatoa sauti yangu kwa vyote, ili kusudi vitu vyote vifikie kusema hivi: “Utashi Wako ufike kutawala hapa duniani”.

Ebu sikiliza Ee Yesu, mimi nagonga mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu hata ndani ya huyo ndege mdogo anayeimbilia, anayetetemesha, na hata anayekoromesha sauti yake. Pamoja na huyo ndege bado ninakuomba utuletee Ufalme wa FIAT Yako. Naendelea kugonga mhuri wa Ninakupenda yangu hata ndani ya huyo kondoo mdogo anayelia akiita, ndani ya huyo njiwa anayelia kama anasikitika. Hata kwa milio ya hao mimi ninakuomba Wewe utuletee Ufalme wa FIAT Yako. Hamna kitu kingine chochote ambacho hakina hamu ya kuchangia katika kurudia kiitikio hiki: ‘FIAT, FIAT’. Ewe Yesu Wangu, ninataka nipenye hadi ndani na katikati ya dunia, ili nikaweke huu moyo wangu pale ndani. Pigo la moyo wangu, wakati litakapokuwa linagonga, liwe linakupenda kwa niaba ya watu wote, liwe linawapenda watu wote, liwe linawakumbatia wote, na kutoka pale katikati ya dunia, moyo wangu uwe unapiga kelele nakulia: Ufike Ufalme Wako na Utashi Wako utawale!

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba..
SAA YA NNE

Pindi tunapokusanyika sote katika Bustani ya Eden, hapo tunajiunga katika sherehe ya Mungu ya kumwumba Mwanadamu.

Ewe Yesu, Uhai Wangu, ninaonja kuwa Pendo Lako linanisukuma likinilazimisha niendelee kuzunguka, na Utashi Wako unaniita ukinitaka niwe pamoja na matendo Yake yote. Inaelekea kuwa Wewe huridhiki iwapo Binti Yako Mdogo hatakuwa pamoja na matendo ya Utashi Wako. Hata kama hajui bado kitu chochote, hata hivyo kwako Wewe ni raha, ili mradi awepo kama mtazamaji na awe hapo kwa ajili ya kurudia kiitikio cha “Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru”.

Ndipo mimi naendeleo na mzunguko wangu hadi ninafikia pale ndani ya Bustani ya Edem. Hapo ninakuona ukiwa katika tendo lile ambapo, Wewe Pendo Langu, pamoja na Utatu Mtakatifu, ulipokuwa ukitengeneza pambo lako penzi, yaani ile sanamu nzuri kabisa ya binadamu. Ni kwa pendo kubwa jinsi gani unavyomtengeneza! Ni uzuri mwingi kiasi gani hujamjazia bado! Ni marembo ya rangi ngapi na mitindo mitindo ya kimungu mingapi ambayo hujamwagia juu yake mpaka kufurika! Na wakati huo unapoendelea kumtengeneza, nakuona ukirudia kumtazama tazama, na unasema: “Ah, ni nzuri ilioje hii sanamu yangu!”. Halafu Pendo Lenu linafurika na kufurika kwa nguvu. Na kwa kukosa kujizuia, Ninyi mnaikumbatia hiyo sanamu nzuri na ya kupendeza, ingawa kama haijapewa roho bado, mnaikumbatia na kuibana kwa nguvu, na kwa nguvu zaidi kifuani penu. Halafu mnailisha kwa kuipatia uhai, na mnaipatia na ufanano wa Kwenu. Kishapo Nyinyi Wenyewe mnaingia ndani yake na kuijaza kabisa, kiasi kwamba hii sanamu, iliyo ni johari lenu, inashindwa kuwabeba ndani yake. Kwa hiyo, na yenyewe inajaa na kufurikia nje yake yenyewe, na inajikuta ikitengeneza bahari zake kwa ajili ya kumpenda Muumba wake. Hilo pendo lililotengenezwa, nalo linavimba sana na kutengeneza mawimbi makubwa makubwa yanayoruka na kuja kujipiga juu ya Pendo umbaji. Yanazuka mashindano ya upendo, ya uabudu, na ya utukufu baina ya Muumba na mwanadamu.

Pendo la kwangu linatetemeka mbele ya hilo tendo la ibada namna ile la kumwumbwa kwa binadamu. Ninasikia sauti yako ya uumbaji isiyokoma kurudia rudia ikisema: “Ni nzuri ilioje hii sanamu iliyotengenezwa na Sisi! Mwangwi wa pendo lake, ni jinsi gani unavyotuvuta na kutushawishi, na kutujeruhi! Ni jinsi gani sauti yake ilivyo tamu, na jinsi gani inavyosikika vizuri! Na ukumbatio wake anaotupatia, ni jinsi gani ulivyo ni laini na papo hapo ni wa nguvu! Ni jinsi gani tupatavyo raha kutambua kwamba tulimpatia uhai! Hii sanamu itaendelea kuwa ni raha yetu, furaha yetu, na itaendelea kuwa ni mchezo wetu wa kutufurahisha.
Yesu Wangu, katika kutetemeka kwangu kutokana na Pendo, ndivyo ninavyoingia kwa kweli ndani ya tendo lile ambamo Utukufu wako Mkuu mno, ukiwa unafurika Pendo, ulianza kuvuta pumzi kwa nguvu, pumzi iliyomvutia binadamu ndani Yenu ili kumjazia pumzi ya uhai. Pamoja na uhai, unampatia ufanano Nanyi, na kama urithi wake, mnampatia FIAT Yako ya Kimungu. Hata mimi napenda nipokee hiyo pumzi Yenu inayohuisha. Ninataka niwapende, na niwaabudu katika ukamilifu na utakatifu ule ule aliotumia yule Baba wa kwanza Adamu. Ninataka nipate yale mabahari Yenu ya Pendo na ya Mwanga. Na ingawa kama mimi ni mdogo bado, hata mimi nataka nitengeneze mawimbi yangu makubwa kabisa ya pendo. Hayo mawimbi yatavimba na kupanda hadi kufikia kifuani penu, yatapiga na kugonga kwenye mawimbi ya Kwenu yasiyokoma wala kukatika. Ndipo nami nitaanza kushindana na Muumba Wangu. Nitakuwa nampa Pendo langu ili niweze kuyapata mabahari mengine zaidi ya upendo. Katika mawimbi hayo, nitakuwa nikikuomba Wewe kwamba Ufalme Wako Ufike na FIAT Yako ijulikane. Ninaingia ndani ya ule umoja wa Utashi Wako, ukiwa ni umoja ule ule uliokuwa ndani ya lile johari lako penzi, naingia hapo ili utashi wangu mimi na Utashi Wako Wewe viwe ni Utashi mmoja, na pendo liwe ni moja. Katika huo umoja unaobeba mambo yote, napenda sauti yangu isikike hadi Mbinguni, na ikawafikie wanadamu wote, ikapenye hadi kwenye giza totoro ya vilindini, na ikapige kelele kwa nguvu ikisema: “Ufike Ufalme wa Utashi wa Mungu! FIAT, FIAT VOLUNTAS TUA, hapa duniani kama kule Mbinguni!”. Na katika umoja huo wa Utashi wa Mungu, nitakuwa ninautwaa utakatifu na kuufanya uwe wa kwangu, na ndivyo nitatwaa na utukufu, uabudu, shukrani za mawazo, za mitazamo, za maneno, za matendo, na za hatua mbalimbali za yule Adamu aliyekuwa bila waa lolote. Kwa namna hiyo nitakuwa nakurudishia Wewe, kwa kurudia rudia, yale matendo yake, ili utakapokuwa unaona ndani yangu huo Utashi Wako wa Kimungu unavyotenda kazi, Wewe utaridhia kuwa Ufalme Wako uweze kufika.

Katika Bustani hii ya Edeni, kulikuwepo daima na sherehe baina ya mwanadamu na Muumba. Binadamu alikuwa ndiye doli la Kimungu, alikuwa furaha Yao, alikuwa ndiye raha iliyomfurahisha zaidi Baba wa Mbinguni. Katika huo umoja wa muungano wa Utashi wa Mungu aliokuwa nao, binadamu alifaidi kuchukua nafasi ya kwanza kati ya Uumbwa wote. Kwa hiyo, mambo yote yalikuwa katika harmonia, na katika mpangilio. Anga, nyota, Jua, na bahari, vyote vilionja kuwa vimepata heshima ya pekee kuweza kumtumikia na kumtii Adamu kila alipokuwa anawaashiria kufanya lolote. Alikuwa yeye ndiyo tabasamu ya vitu vyote, alikuwa ni furaha yao, na mtamaniwa wa kila kitu. Na yeye Adamu alikuwa akipeleka kila kitu kwa Muumba Wake, na Mungu alikuwa akielekeza daima macho Yake juu ya Adamu, ili kuhakikisha kuwa pasikosekane kitu chochote kwa ajili ya kumletea raha zake kikamilifu.

Mungu, akimwangalia na kumwona kuwa yu katika upweke, akapenda kuongeza raha yake Adamu iwe maradufu. Alimtia usingizi wa namna ya ekstasi nzito kabisa, na akamfanya alale mikononi Mwake. Ndipo akamtoa ubavu wake mmoja ambao kwayo alimtengeneza mwanamke aliyekabidhiwa kwake awe mwenzi wa kufanana naye. Kwa tendo hilo alimjalia ujazo wa uwingi wa furaha. Na, lo, huyu Eva, akiwa ndiye mama wa kwanza kabisa, alipoingia na yeye katika muungano wa umoja wa Utashi wa Mungu, naye alijiunga kufanya mashindano na Adamu.

Walikuwa wakishindana kati yao, kuona ni nani kati yao, wakiwa ndani ya mabahari yao ya pendo, angeweza kutengeneza mawimbi mengine makuu zaidi ya pendo, ambayo yangeruka juu zaidi na kwenda kugongana na yale mabahari ya Kimungu katika ukuu wao usio na ukomo. Kwa njia hiyo Adamu na Eva wangefikia kujipatia mabahari mengine ya pendo, na kujipatia neema nyingine za Kimungu. Na mawimbi ya pendo lao yalizidi kupanda na kushuka hata kufanya mabahari yao yazidi kuongezeka, kupanuka na kuenea.
Ewe Yesu Wangu, katika muungano huo wa Utashi moja wa Mungu, ninatumbukiza hata hii roho yangu duni ndani ya hayo hayo mawimbi makuu ambayo kwayo Adamu na Eva, kwa pendo kuu, walikuwa wakiupenda na kuutukuza Utukufu Wako Mkuu Mwabudiwa. Mimi, kamwe sitatoka na kutoroka, toka hapo ndani ya Utashi Wako. Bali nitabaki hapo na kufanya kila kitu kiwe ni cha kwangu: Anga, Jua na dunia. Kwa njia hiyo, hapo chini ya miguu ya kiti chako cha juu, nitakuja kuleta na kuweka pendo lote, sifa zote, utukufu na uabudu ambao, katika Uumbwa wote, ulikuwa ukijitokeza kutoka kwenye Kifua Chenu Kiabudiwa.

Katika mawimbi hayo ya pendo, nitakuwa nikipiga kelele endelevu kusema: “Ufike Ufalme Wako! Utashi Wako ujulikane!”. Ewe Pendo Langu, ni jinsi gani ninavyoonja raha katika hii Bustani ya Edeni! Hapa ninaonja ile nguvu ya muungano wa Utashi Wako mmoja wa Kimungu ndani ya hawa wanadamu wa kwanza. Muungano huu unafanya tendo lao liwe ni tendo moja na lile la Muumba. Umoja huo huleta mema yote na kuyafanya yawe ni mali ya pamoja na ya jumla baina ya Mungu na hawa binadamu wawili.

Furaha Zako na raha Zako, Ewe Yesu Wangu, ni pia furaha na raha za kwao. Na mimi niliye Binti Mdogo wa Utashi Wako, napenda nianze upya maisha yangu, katika muungano huu wa umoja wa Utashi Wako, nikiwa pamoja na wazazi wangu Adamu na Eva. Katika mabahari haya ya pendo ninapenda kutengeneza makao yangu, nataka kutengeneza mawimbi yangu ya furaha na ya raha.

Nitakapoyarusha na kuyagongesha katika mabahari Yako ya milele, nitapenda kukufikishia furaha na raha hata niweze kukuona ukitabasamu daima, na daima ukiwa na raha zako.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba..
SAA YA TANO

Pindi tunaposhuhudia kosa la Adamu na Eva pale katika Bustani ya Edeni, tushiriki maumivu ya Kimungu na tujitahidi kulipa fidia kwa njia ya kauli yetu ya Nakupenda.

Mimi sitatoka kamwe nje ya muungano huu wa umoja wa FIAT Yako. Ninapenda, hatua kwa hatua, niwe ninawafuatilia wazazi wangu wa kwanza. Nitawafuatilia hata pale ambapo, kwa bahati yao mbaya sana walithubutu kutoka nje ya muungano huo wa umoja wa Utashi Wako, kwa kudiriki kufanya utashi wao. Walianguka kutoka kileleni juu kabisa na kutua chini kilindini kabisa kwenye matatizo yote. Ilikuwa mbaya kiasi kwamba hata Mbingu na dunia zilitikisika kwani zilishuhudia wanadamu wale wazuri wa kupendeza kabisa wakihama toka pale ndani ya Utashi wa Muumba Wao. Wote wakawa wanatetemeka na hata Ninyi Wenyewe, Ewe Utukufu Mkuu Mwabudiwa. Ninyi mlipatwa na uchungu hivi hata mkaamua kujivika koti la Haki dhidi yao pale mliposhuhudia ile sanamu nzuri ya kupendeza ikijing’oa. Na aidha, mlishuhudia kuvurugwa kwa furaha zenu, na kupasuliwa kwa yale madoli, yaliyokuwa yakiwaletea burudani, ambayo lile johari Lenu penzi lilikuwa likiwaletea toka ndani ya Utashi Wenu Wenyewe.

Ndiyo maana, Ewe Yesu Uhai Wangu, mimi sitaki kutoka nje ya huo muungano wa umoja wa Utashi Wako wa Kimungu. Ni kwa vile ninataka nijazilishe na kurudisha kile ambacho wanadamu wa kwanza walikipoteza. Nataka niondoe toka kwao lile kovu kubwa la udhalili lililobandikwa juu ya panda la uso wao kwa vile walitekeleza utashi wao wa kibinadamu. Na ni kwa vile nataka niendelee kushikilia pamoja Nawe zile furaha, zile raha, na hata yale madoli uliyokuwa unayo katika nyakati zile za mwanzoni mwa Uumbwa. Napenda nikupe na busu langu, nikupe na fidia yangu endelevu, kwa ajili ya yale maumivu makali kabisa mliyoyapata hata yalipelekea muamue kuvaa vazi la Haki. Mimi napenda niwavue hilo vazi la Haki na badala yake napenda niwavalishe vazi la amani, vazi la mwanga, la muungano wa umoja wa Utashi Wenu. Na mwishowe nataka niwe na kilio kimoja tu: “Ufike Ufalme wa FIAT Yako, Afadhali zirejee zama zile za mwanzoni mwa Uumbwa; afadhali zikaanza tena zile sherehe, zile furaha, na zile burudani zilizokuwepo baina Yako na wanadamu!”. Mimi sitakuacha, wala sitadiriki kuteremka toka hapa magotini pako, iwapo hutanipatia neno la kunithibitishia kuwa utarejesha tena Ufalme wa Utashi Wako kati ya wanadamu.

Ewe Yesu Wangu, Uhai Wangu, Utatu Mwabudiwa, mimi Binti Yenu Mdogo, sitaweza kuwaacheni peke yenu katika uchungu ndani ya umoja wa Utashi Wenu. Kamwe sitaweza kutoka nje. Ninaahidi na ninaapa kamwe kutotekeleza utashi wa kwangu. Kwa kweli, ili nisiwe ninaufikiria na kuukumbuka, naamua sasa kuufunga kwenye miguu ya Kiti Chako cha kifalme ili uwe unalipa fidia endelevu na rasmi kwa ule utoro na uasi waliokuwa wamefanya Adamu na Eva dhidi ya Utashi Wenu Mwabudiwa. Na Mimi, katika muungano wa umoja wa Utashi Wako, ambao ndio peke yake nataka niwe ninautambua, nikiwa ninajiainisha kuwa kitu kimoja na Wewe uliye Uhai Wangu Mtamu, napenda niyapange mbele yangu, kuanzia wazo lile la kwanza kabisa la Adamu hadi lile wazo la mwisho la wanadamu watakaokuja kuwa hapa duniani, kwa lengo la kuweza kutia mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu juu ya kila wazo, nibandike na fidia yangu, nibandike na utukufu kwako. Na kwa kila wazo la wanadamu, ninataka nikuombe Wewe utujalie Ufalme wa Utashi Wako, utujalie kwamba kila akili iweze kuelewa maana ya ‘Utashi wa Mungu’, na watu wote wawe wanauruhusu Utashi wa Mungu uwe unatawala na unaamrisha.

Katika muungano wa umoja wa Utashi Wako nataka nikajipange ndani ya kila mwono wa jicho la mwanadamu, nataka nikajiweke katika nafsi yangu ndani ya kila neno kusudi nikapige mhuri wa ‘Ninakupenda’ kwa ajili yako na nikapige mhuri wa fidia yangu ili kukuomba Wewe Ufalme Wako. Katika kila kazi, katika kila hatua, na katika kila pigo la moyo napenda kukuambia: “Ninakupenda na Ninakulipa fidia kwa dhambi zote wanazotenda”. Na mwishowe napenda nikuombe utupatie Ufalme wa FIAT ya Kimungu.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA SITA

Pindi tunapoendelea kutoa fidia yetu, tutapitia orodha ya watu maarufu waliopo katika Agano la Kale

Katika muungano huu wa umoja wa Utashi Wako wa Kimungu, ninapenda nijazilishe ule utukufu wote na lile pendo lote, ambalo wanadamu walitakiwa wawe wamekutolea, kama wangekuwa wameishi katika muungano na huo Utashi Wako. Nataka nijazilishe kwa ajili ya wanadamu wale wote walioishi tangu mwanzo wa dunia hadi siku ile ya Tufani kuu. Nafanya hivyo kwa ajili ya kukuomba Ufalme Wako kwa niaba ya wanadamu hao wote. Napenda niruke juu nikiwa ndani ya Utashi Wako wa Kimungu ili niweze kufuatilia vitu vyote na wanadamu wote.

Kwa minajili hiyo, nakuja kugonga mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu juu ya sadaka ya Ibrahimu na juu ya utii wa Isaka. Ninalitekeleza hilo, ili kwa ajili ya sadaka hiyo na utii huo, nikuombe Wewe Ufalme wa Utashi Wako wa Kimungu. Kadhalika, ndani ya muungano huo wa umoja wa FIAT Yako ninayaona yale mateso ya Yakobo kama vile pia mateso ya Yosefu pamoja na utukufu wake. Ndipo na mimi, kwa ajili Yako, ninagonga mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu juu ya mateso hayo yote. Wakati huo ninakuwa nikikuomba Ufalme Wako. Bado naendelea kuruka nikifuatilia matendo ya Utashi Wako. Ninagundua Maweza ya miujiza ya Musa, nagundua nguvu za Samsoni, utakatifu wa Daudi, na saburi ya Ayubu. Fadhila hizo zote ni vivuli vilivyoletwa na Utashi Wako hata vikatua juu ya watu hao. Nami, pindi ninapopita kugonga mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu ninakuomba, kwa ajili ya wanadamu wote, kwamba Utashi Wako wa Kimungu utawale.

Hebu angalia, Ewe Pendo Langu, mimi muda wote huu nipo nikifuatilia bado matendo ya Utashi Wako ndani ya wanadamu wote, ili kwa njia ya matendo yao hayo yenyewe, nifikie kukuomba Wewe kwamba, FIAT Yako afadhali ijulikane, ipendwe na itamaniwe na wanadamu wote. Ewe Yesu, Uhai Wangu, ninatambua kuwa Utashi Wako Mpendevu wa Kimungu unazidi kuwakaribia wanadamu. Kwa mwanga wa tochi zake, Utashi Wako tayari unawamulika Manabii, ukiwafunulia hao juu ya ujio Wako hapa duniani. Unawahakikishia juu ya muda halisi, juu ya mahali halisi, na juu ya ishara na mazingira yatakayokuwa yameambatana nao. Na mimi kwa upande wangu, wakati ninapopita nikiruka juu ya kila Nabii na juu ya kila ufunuo unaoutoa, ninapita nikimgonga kila mmoja wao, na kila ufunuo, kwa mhuri wa kauli yangu ya ‘Ninakupenda’, ‘Ninakuheshimu’, na ‘Ninakushukuru’. Na katika kila nafasi ninakuomba Ufalme wa Utashi Wako.

Kila ahadi uliyokuwa ukitoa, kila ufunuo ulioutoa na kuuonyesha mintarafu ujio Wako hapa duniani, vilikuwa ni kauli uliyokuwa ukiwapatia, ya kutuliza na kutumainisha. Ndani ya ahadi na funuo hizo, ulikuwa ukiunganisha daima Ufalme wa Ukombozi Wako na Ufalme wa Utashi Wako. Sasa ni kwa nini, Ewe Pendo Langu, hutaki kuuharikisha huo Ufalme? Mbona Wewe huwezi kutenda kazi Zako kwa nusunusu, na wala Wewe huwa hutoi mema yako kwa nusunusu. Haya basi, fanya hima: Endapo ulikuwa umetupatia nusu ya mema.

Yako, sasa kamilisha kila kitu, kwa kuruhusu Ufalme Wako ufike. Huyu Binti Yako Mdogo wa Utashi Wako, hataweza kukuacha. Ataendelea hadi akuchoshe. Kwa hiyo, nitakuja kusitisha mazungumzo yangu pale tu nitakapouona Utashi Wako ukitawala na ukiamrisha kati ya wanadamu.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA SABA

Sasa tunajitumbukiza katika mabahari ya mwanga na ya utakatifu ya Mama wa Mbinguni. Pamoja naye tuwe tunaomba Ufalme wa Utashi wa Mungu ufike duniani.

Ewe Pendo Langu, ninaonja kuwa Pendo Lako limejaa mno na linafurikia ndani yangu. Ninakuona ukivua joho lako la Haki, na Ninyi Nafsi zote Tatu za Mungu mnajipanga na kujiweka tayari kwa ajili ya sherehe mpya; na inaelekea sherehe hii ni kubwa zaidi ya ile iliyokuwa imefanyika katika tendo lile la kumwumba binadamu. Ninyi Wenyewe, mnatoa nje yenu wenyewe, mabahari ya Maweza, ya Hekima, ya Pendo, na ya Uzuri upendezao usioelezeka. Halafu mnayakusanya mabahari hayo mahali pamoja. Kishapo, kutoka kwenye kina cha mabahari hayo, kwa nguvu na uwezo wa neno Lenu la uumbaji, mnamwita Malkia Mdogo ambaye mnamtia na uhai. Mnamtengeza awe safi kabisa, bila doa lolote, na mnamfanya awe amejaliwa na neema za uzuri upendezao. Ni mzuri hivi hata anamteka Yule Mwenyewe aliyemuumba.

Kipindi hicho cha kuibeba mimba ya huyu Malkia Immakulata, panazinduliwa sherehe nyingi baina ya Mbingu na ya dunia. Uumbwa wote unashangilia na unapiga magoti yao. Wote wanampongeza na wanamshangilia kama Malkia wao. Hata mimi ninapiga magoti yangu mbele yake huyu ambaye Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanamgombania, ili mmoja wao au mwingine anayemtaka ajiburudishe naye zaidi, na kama anamtaka, aweze kumfaidi kwa vikubwa zaidi. Katika hatua hiyo, ninyi Wote, Nafsi Tatu za Mungu, hamtendi kitu chochote tena, isipokuwa kujaa na kufurika Pendo ambalo mnaendelea kummwagia daima huyo Malkia Mzaliwa mpya. Na wala hamuachi kamwe kumwaga viwango vingine zaidi vya neema juu yake ili kukuza mabahari yake yawe makubwa zaidi na mapana bila ukomo wowote. Ndani ya binadamu huyu wa Mbinguni, mnamgundua Yule Mwanamke, ambaye ndiye atapasika kuwapatieni Ninyi kila kitu, atakayepasika kulipa fidia ya mambo yote, na atakayepasika kuwarejeshea ule utukufu wote wa Uumbwa. Kwa minajili hiyo basi, huku mkiendelea kumshikilia, mkimbana penye magoti Yenu ya Kibaba, mnamfunulia kumwonyesha na kumweleza juu ya kisa cha binadamu aliyekuwa ameanguka katika dhambi, mnamweleza juu ya uchungu wenu, na mnamweleza juu ya Utashi Wenu Mwabudiwa, ambao ulikuwa umegomewa na kusukumizwa mbali na binadamu. Mwishowe Ninyi mnayakabidhi mambo yote kwake huyo Malkia.

Katika hatua hii, Ewe Yesu Wangu, mimi ninatehemu, ninaonja uchungu sana sana kushuhudia jinsi Utashi Wako pendevu ukigomewa na kusukumizwa mbali. Papo hapo ninastaajabu ushujaa wa huyu Malkia Mdogo Mzaliwa mpya, ambaye anautoa uhai wake kama zawadi. Anaapa kuwa hapendi kusikia wala kuujua tena, na ndipo anautumbukiza ndani ya FIAT Yako, ambayo sasa ndiyo anayoitwaa iwe ni uhai wake. Anatoa mamlaka kwa FIAT hiyo, na ndani yake anaunda Ufalme wa kwanza wa Utashi Wako ndani ya roho yake. Na kutoka pale ndani ya roho yake ninasikia kiitikio chake hiki endelevu: “Ufike Ufalme wa Ukombozi, afike Neno hapa duniani, ifike na amani kati ya Muumba na mwanadamu! Mimi sitateremka toka hapa penye magoti yenu ya Kibaba, endapo Ninyi hamtanijalia hicho ninachowaombeni”. Na angalia sasa, Malkia Mdogo analia machozi, hata anailowesha mikono Yenu ya Kibaba kwa machozi yake. Mara nyingine anawatazama na kutabasamu na halafu anawaombeni. Kisha, anapojitumbukiza katika yale mabahari mliyompatia, anawaleteeni furaha mbalimbali na raha ya Utashi Wenu, hata anaweza kuwashindeni na kuwalegezeni, ili tu aje ampate Mkombozi ajaye. Oh, ni mbinu ngapi na ujanja gani wa pendo, alizotumia Mama yangu wa Mbinguni juu yenu! Ni jinsi gani alivyokuwa akiwateka kwa mitindo yake ya kupendeza ajabu, kiasi kwamba Wewe, Pendo Langu, mwishowe ukashindwa na kukubalia maombi yake na kilio chake kisichokoma.


Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA NANE

Pamoja na Mama wa Mbinguni tunaendelea kumsihi Mungu Baba wa Mbinguni, ajalie kwamba Utashi wa Mungu ujulikane kwa watu wote na pia kwamba Ufalme Wake ufike.

Ewe Yesu, Uhai Wangu mtamu mno, ebu uchukue na uipeleke roho yangu hii ndogo pale juu ya magoti ya kibaba ya Mungu Baba yetu wa Mbinguni, ikawe pale pamoja na Mama yangu Malkia. Roho yangu iwe pale kusudi iwe inasali, inalilia na kutamani kwamba Ufalme wa FIAT Yako ya Kimungu ufike. Na kwa tabasamu zangu za pendo, kwa mabusu yangu ya upenzi, na kwa mabembelezo yangu kwenu Nyote Nafsi Tatu za Mungu, niweze kuziteka kwa nguvu ile ile ya utekaji iliyomo katika Utashi Wako. Niuteke Utatu Mtakatifu hadi ukubalie ombi langu la kuleta Ufalme Wako hapa duniani. Na kwa kweli, ninapojitumbukiza ndani ya mabahari ya Mama yangu, huyu binti mdogo wa Utashi Wako wa Kimungu, anapenda kutengeneza mabahari yake madogo madogo ndani ya mabahari ya Mama yake. Yeye Mama atatoa nafasi kwa binti kuweza kuingia ndani ya mabahari yake ili aweze kutengeneza mabahari yangu ndani ya mabahari yale yale yake Mama, ili niweze kuendelea kusihi Ufalme wa Ukombozi kama yeye alivyokuwa amesihi.

Basi sasa, ewe Mama Mtakatifu, toa mkono wako kwa Binti yako Mdogo, na wewe mwenyewe unisaidie niweze kuogelea katika bahari ya pendo lako, ili pale nikaweze kugonga muhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu isiyokoma katika bahari yako ya pendo na pale niweze kutengeneza bahari yangu ndogo. Ndipo, kwa bahari ya pendo la Mama, pamoja na bahari ya pendo la Binti tunakusihi utupatie Ufalme wa FIAT Yako. Kishapo ninaendelea na kuingia katika bahari ya uabudu ya Mama yangu, ili pale ndani nikatengeneze bahari yangu ndogo ya uabudu kwa Muumba Wangu na nikaendelee kuomba Ufalme Wake. Naendelea kuruka juu ya mabahari ya sala zake, ya maombi yake, na matamanio yake, ili nitengeneze mabahari yangu ya sala, ya maombi na ya matamanio kwa ajili ya kuweza kusihi Ufalme wa FIAT kwa njia ya sala zile zile za Mama wa Mbinguni. Ewe Mama yangu Malkia, mabahari yako hayana ukomo. Kwa sababu hiyo, ipo daima nafasi kwa ajili ya kuweza kuingiza vitendo vidogo vidogo vya Binti yako Mdogo. Basi, unisaidie Wewe mwenyewe kuingiza haya mambo yangu yafuatayo, ndani ya bahari ya maumivu yako na ndani ya bahari ya uchungu wako mkali: ingiza maumivu yangu madogo madogo, ingiza miaka yangu mingi na migumu ya kitandani, maumivu ya kuachika na sadaka mbalimbali, na lile teso lililoniumiza zaidi kupita yote, la kuachika mara kwa mara na Yesu, teso linalonigharimu maumivu ya mauti endelevu.

Ewe Mama yangu, unganisha maumivu yangu hayo yote kwa pamoja, ukayaingize katikati ya bahari ya mateso yako mengi na makubwa. Ndipo na mimi niweze kutengeneza bahari yangu ndogo ya teso. Kwa bahari yako ya teso, pamoja na bahari ya kwangu, niweze kuomba bila kukatisha, kwamba Ufalme wa Utashi wa Mungu ufike haraka, kwamba uteremke na kuja kati ya wanadamu, na kwa sherehe ya ushindi, Utashi huo utawale na ushike himaya yake kati yao.

Ewe Mama yangu, je wewe hupendi kumfurahisha Binti yako Mdogo, kwa kuweza kusema pamoja nami, kuweza kubeba pendo moja tu, kuwa na Utashi mmoja tu, kuwa na tendo moja tu na kuwa na sauti moja tu isemayo: ‘MAPENZI YAKO YATIMIE’ hapa duniani kama kule Mbinguni’*** ?

Na kama vile wewe, kwa njia ya mabahari hayo, wewe, kwa kutolea tumbo lako pawe mahali pa kumpokelea, uliweza kumfanya Neno atoke Mbinguni na ukamfanya ateremke kuja hapa duniani, ndivyo na sasa, kwa njia ya mabahari haya, ufanye FIAT ya Juu itoke kwenye kiti chake cha Mbinguni na ifike hapa duniani. Mimi najitolea mwenyewe kuipokea, kusudi iingie na kubaki imebebwa mithili ya mimba ndani ya roho yangu, na pale itengeneze Ufalme wake ndani yangu mimi, na kutoka kwangu iweze kwenda kutawala katika wanadamu wote.

***Katika Kilatini: FIAT VOLUNTAS TUA, SICUT IN COELO ET IN TERRA!

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA TISA

Tunaendelea kufuatilia Utashi wa Mungu katika tendo la kutungwa mimba ya Neno na katika tendo la kuambatana na Yesu, Mfungwa Mdogo, katika tumbo la Mama Yake.

Ewe, Mama yangu Mkuu mwenye mamlaka, mimi ni mdogodogo mno. Sipendelei kubaki peke yangu bila wewe, kusudi katika matendo yako yote, uweze kuunganisha na matendo ya kwangu ili kufanya liwe tendo moja tu litakalotuwezesha wewe na mimi, kwa pamoja, kuomba Ufalme wa Utashi wa Mungu. Kwa minajili hiyo, katika FIAT ya Kimungu hiyo hiyo, mimi ninafuatilia sasa lile tukio la kutungwa mimba kwa Neno ndani ya tumbo lako la kimama. Ninalifuatilia kusudi, pale ndani ya tumbo lako, nikaingize na kuyapanga matendo yangu yote niliyokwisha kuyafanya ndani ya FIAT, halafu nikaweke juu yao mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu endelevu, ili yawe kama kikosi cha kukesha pamoja na Neno. Nitaweka hapo pia maumivu yangu madogomadogo ili wakati unapomtunga mimba ndani yako, mimi niwe ninamwingizia matendo ya kwangu pamoja na yale ya kwako, ili kwa pamoja yawe yanamfanya atungike mimba. Ndipo hapo mimi ninamwomba Ufalme wa Utashi wa Mungu, kwa nguvu ya lile pendo kuu aliloonyesha pale alipoteremka kutoka Mbinguni, na kuja kujifungilia ndani ya mahabusu haya membamba ya tumbo lako,

Oh, wewe kama Mama yangu, mimi ninapenda nijifungilie ndani ya tumbo lako nikiwa pamoja na Yesu Wangu mdogo, ili niwe ninakesha pamoja naye, katika upweke anaouonja ukimtesa. Hapo nitakuwa nikishuhudia kwa macho yangu maumivu yake yote, ili niweze kuyafuatilia kwa mhuri wa kauli yangu ya ‘NINAKUPENDA, NINAKUHESHIMU, NINAKUSHUKURU’. Hapo ninaona kwamba, maadam Mtoto Wangu Yesu anaanza kupata yale maumivu makali sana, na vifo endelevu, kutokana na zile mara zote ambapo wanadamu walikuwa wameusukumia mbali na kuugomea Utashi wa Mungu, na wala hawakuruhusu uanze kuendesha uhai wake katika roho zao. Kwa hivyo, Utashi ulikuwa unaonja kifo, na Wewe, ee Yesu, pale pale umekuwa ukipenda kubeba vifo vyote hivyo juu ya mabega yako. Umefanya hivyo kwa ajili ya kulipa malipizi kwa Utashi Mkuu wa Mungu. Kwa hiyo ninakuona, ingawa kama u kadogo bado, lakini unateseka na maumivu makali kabisa. Ninaonja moyo wangu ukipasuka ninapokuona unaingia katika hatua ya kufa. Kwa upande wangu, Ewe Mtoto wangu Mchanga na laini, ninapenda, hapa ndani ya roho yangu, niwe ninatoa uhai kwa FIAT ya Kimungu katika mara zile zote ambapo wanadamu wamekuwa wanaigomea na kuisukumizia mbali. Mara nyingi nimekuwa nikitaka kuulia mbali utashi wangu, kwa mara zile zote ambapo wanadamu wamekuwa wakiupatia fursa ya uhai. Badala yake, ndani ya Ubinadamu Wako mdogo, ninataka nitiririshe uhai wa Utashi Wako wa Kimungu ambao ninaubeba hapa ndani yangu. Ninafanya hivyo ili kusudi, hayo maumivu makali mno unayoyapata pamoja na maumivu ya kifo unayoyakabili, yaweze kupunguza makali yake.
Ewe Mpenzi sana Mtoto Mchanga, ni maumivu mangapi unayoyapata hapo ndani ya tumbo la Mama yetu Malkia! Ninakuona ukikosa umudu wowote, unashindwa hata kutikisa kidole chochote kile wala kamguu kako. Huna hata kanafasi kwa ajili ya kuweza kufungua hayo macho yako mazuri, hamna hata kamwanya kadogo kanakoweza kukupitishia walau mwonzi moja wa mwanga. Hapa, katika mahabusu haya membamba ya tumbo la kimama kila kitu ni kiza totoro. Hali hiyo yote inanieleza maumivu ambayo Wewe unayoyapata. Inanieleza jinsi wanadamu walivyosababisha Utashi Wako Mwabudiwa kukosa kabisa ujimudu wa aina yoyote. Inanieleza pia ni jinsi gani wanadamu wote wanavyokuwa ni vipofu hata kushindwa kuuangalia na kuujua Utashi wa Mungu. Na inanieleza kwamba, bila Utashi wa Mungu, roho zao wanadamu hubaki katika usiku wa kiza totoro. Na mimi, Ewe mpenzi wangu Yesu Mdogodogo, ninapenda nipeleke uhai wa Utashi Wako pale ndani ya yale mahabusu finyu, yaliyokuwa ndiyo makao yako ya kwanza hapa duniani. Kwa tendo hilo ninataka nitengeneze pambazuko katika lile giza totoro inayokuzunguka. Nataka nibandike hapo busu langu, nataka nibandike na mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu juu ya kila kiungo cha mwili wako ambacho kinakosa ujimudu wowote. Ndipo nitakuwa nikikuomba kwamba, kwa maumivu hayo unayopata, Utashi Wako wa Kimungu uanze kutekeleza ujimudu wake ndani ya wanadamu. Nitaomba kwamba kwa nguvu ya mwanga wake, ufukuzie mbali ule usiku wa giza la utashi wa kibinadamu, na badala yake, hapo ndani yao wanadamu, Utashi Wako utengeneze pambazuko endelevu lisilokoma la FIAT Yako.

Ewe Mtoto Wangu Mpendevu, kama mimi, katika ombi langu hili, sitaweza kukushinda Wewe sasa hivi wakati u bado kadogodogo, hata uweze kunijalia Ufalme wa Utashi Wako wa Kimungu, ebu basi unieleze, ni lini nitakuja kukushinda? Je, unajua lakini, Ewe Mtoto mpenzi, kwamba huyu msichana mdogo wa roho yangu, kwa maweza na nguvu ya FIAT Yako, anapenda akushinde Wewe kwa pendo. Kwa sababu hiyo basi, mimi, katika hiyo FIAT, ili kuja kunisaidia, ninaita matendo yote ya Utashi Wako wa Kimungu, yaje sasa na yasimame na yajipange kukuzunguka Wewe, kama kikosi cha jeshi lenye nguvu kabisa. Ninaita pia anga lote pamoja na jeshi lake lote la nyota, lifike kukuzunguka. Ninaliita na Jua pamoja na nguvu ya mwanga wake, na nguvu ya joto lake, ninaita na upepo pamoja na mvumo wake mkali wa himaya yake, ninaiita na bahari, pamoja na mawimbi ya dhoruba kali, na ninaita pia na Uumbwa wote. Mwishowe nitahamasisha na kunogesha mambo yote, nikiimbilia kwa sauti yangu, huku nikizunguka kufuatilia na kubandika juu ya matendo Yako yote, ule mhuri wa kauli yangu ya ‘Ninakupenda’ pamoja na ile kauli ya wanadamu wote. Hiyo ni kwa ajili ya kukuomba Ufalme wa FIAT Yako ya Kimungu.
Ewe Mtoto Wangu Mchanga na Laini, je unakiona, hicho kikosi cha kukupokea na kukusindikiza, nilichopenda kukuandalia, ili upate kukikuta wakati unapotoka tumboni mwa Mama? Kazi Zako zote zikiwa zimejipanga kama kikosi cha jeshi kinachokuzunguka Wewe, huyu msichana mdogo anapenda kukuambia Wewe na wanadamu wote: “Ninakupenda, Ninakupenda, Ninakupenda! Ninakuheshimu, Ninakushukuru, Ninakuabudu!” Na pamoja na watu wote ninapenda nibandike mhuri wa kauli yangu ya ‘Ninakupenda’ na nibandike pia busu langu la kwanza juu ya hiyo midomo yako inayotetemeka, wakati ukitoka tumboni mwa Mama na ukiwa unakimbilia kwenda kukumbatiwa na mikono ya Mama wa Mbinguni. Na yeye alikukumbatia sana na kukubana kifuani pake, alikubusu, na alipokupa maziwa yake unyonye alikupasha joto na kukutuliza usilie. Kwa jinsi nilivyo bado ni msichana mdogo mno, hata mimi napenda nikaingie pale katika mikono ya Mama nikumbatiwe, na juu ya busu lile lile analokupa, nami ninabandika busu la kwangu. Katika maziwa yake Mama, ninapenda kutiririsha ‘Ninakupenda’ yangu, kusudi, kama Mama anakulisha kwa maziwa yake, mimi nitakulisha kwa pendo langu. Kila kitendo anachokufanyia yeye Mama, nami napenda kukutendea hicho hicho. Ebu angalia, Ewe Mtoto Wangu Mpendwa, mimi hapa sipo peke yangu, nina kila kitu hapa: Lipo jua kwa ajili ya kukupasha joto, zipo hapa Kazi Zako zote kwa ajili ya kukutuliza usilie. Kwa minajili hiyo nipo nikifuatilia vilio vyako, malalamiko yako laini, na kwa vile unajiona hupendwi na wanadamu, mimi napenda niwe kama yaya Wako ili niwe ninakubembeleza kwa kukuimbilia: ‘Ninakupenda, Ninakupenda’ hata uweze kupata usingizi. Yote hayo ni kwa lengo kwamba mara nitakapokuona unashituka toka usingizini, mimi niwe ninakuomba Ufalme wa FIAT Yako.

Ewe Mama yangu, tafadhali unisaidie. Wewe, ukiwa pamoja na mimi, umwambie Mtoto huyu wa Kimungu: “Tafadhali umfurahishe huyu Binti yetu Mdogo ambaye hana kingine anachotaka na anachotamani na kulilia isipokuwa anaomba Utashi Wako ujulikane na utawale hapa duniani”.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba..
SAA YA KUMI

Tumfuate Mtoto Mchanga Yesu akiwa mikononi mwa Mama Yake wa Mbinguni, akiwa katika maumivu ya Kutahiriwa, na tufungilie tashi zote za kibinadamu ndani ya jeraha lake lenye maumivu
.
(Katika makala ya mkono hapa hufuata kile kilichoandikwa katika Juzuu Na. 17 - Hiki kinachofuata hapa chini ni kile ambacho kiliachwa kuandikwa katika Juzuu ile)

Ewe Mtoto Wangu Laini, kauli yangu ya ‘Ninakupenda’, ‘Ninakuheshimu’, na Ninakushukuru’ itakuwa inakufuata popote kwa ajili ya kukuomba FIAT Yako. Katika kila pigo la Moyo wako na katika kila pumzi yako, katika ulimi wako, katika mboni ya macho yako, kama vile matone ya damu yako yanavyojiongeza ndani ya Ubinadamu Wako mdogo, ndivyo na mimi nanuia kubandika mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu na busu langu juu ya kila moja ya mawazo yako matakatifu, juu ya mikono na juu ya viganja vya Mama wa Mbinguni na vya Mtakatifu Yosefu. Naweka huo muhuri kusudi hao wanapokubana kifuani pao, Wewe uwe unaionja ‘Ninakupenda’ yangu. Ninabandika muhuri hata katika pumzi za hao wanyama waliolala kimya hapo miguuni pako wakikupasha joto na kukuabudu kwa tendo lao la kufungua midomo yao na kucheua. Katika pumzi yao hiyo mimi napenda Wewe uwe unasikia ‘Ninakupenda’ yangu ambayo inakuomba FIAT Yako ya Kimungu.

Ewe Mtoto Wangu upendezaye na kuvutia sana, hiyo kauli yangu ya ‘Ninakupenda’ itakufuata hadi kule kwenye tendo la kukatwa kikatili wakati wa kutahiriwa. Katika ile Damu yako ya kwanza uliyomwaga, mimi nataka, kwa ‘Ninakupenda’ yangu, nipozeshe maumivu makali uliyopata. Juu ya kila tone la Damu hiyo, napenda kutia mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu, juu ya machozi yale uliyomwaga Wewe kutokana na maumivu, aliyomwaga Malkia Mwenye mamlaka kuu, na aliyomwaga Mtakatifu Yosefu walipokuwa wanakuona unavyoteseka. Damu ile, teso lile, na machozi yale, vyote vinaomba ushindi mkuu wa Ufalme Wako. Ewe Mpenzi Wangu Yesu Mdogodogo, napenda nikukumbatie kifuani penye moyo wangu ili nipozeshe maumivu na uchungu unaopata. Ndani ya hilo jeraha la kutahiriwa napenda kufungilia tashi zote za kibinadamu za wanadamu kusudi zisiwe na uhai wala ujimudu tena. Na kutoka katika jeraha hilo utokee sasa Utashi Wako wa Kimungu kuja kutawala kati yao wanadamu.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba..
SAA YA KUMI NA MOJA

Tunamfuata Mtoto Yesu anayekimbilia Misri. Tunaualika Uumbwa wote kuja kumbembeleza. Na pamoja nao wote tunaomba tuupate Ufalme wa Utashi wa Mungu.

Ewe Mtoto Wangu Mpendevu, pindi lile jeraha la kutahiriwa likiwa bado linatoa Damu, teso lingine zaidi laongezeka kukukabili Wewe: Ni mwuaji mkatili mmoja anayekutafuta ili kukuua. Wewe unapasika kwa lazima kutorokea Misri kwa ajili ya usalama wako. Hiyo ni tena ishara nyingine ya njama za utashi wa kibinadamu ambao unataka kuudhulumu Utashi Wako wa Kimungu ili kuuzuia usitawale.

Mtoto Wangu Maridadi, katika teso hili, ninapenda nitiririshe ‘Ninakupenda’ yangu, mabusu yangu ya upenzi, na pia utashi wangu ili usiwe na uhai tena, kwa ajili ya kuleta upatanisho na kujenga undugu baina ya utashi wa kibinadamu na Utashi wa Mungu na hatimaye kutengeneza Utashi moja tu. Na kwa nguvu ya hilo teso lako kali ninapenda nikuombe FIAT Yako. Basi kwa hiyo, pindi Mama anapokuwa amekubeba mikononi mwake, mimi ninafuata hatua za huyo Mama yangu. Na anapotembea, toka chini ya nyayo zake, ninapenda Wewe uwe unasikia ile kauli yangu ya ‘Ninakupenda’. Kwa sababu hiyo, hatua kwa hatua, juu ya kila atomu ya ardhi, juu ya kila unyasi au jani analokanyaga, mimi ninabandika hiyo kauli, na huku nikihamasisha mimi mwenyewe kwa sauti yangu, ninapenda Wewe uwe unasikia, toka pale kwenye nyayo za Mama yangu, kile kiitikio kinachosema: ‘Ninakupenda, Ninakuabudu, Ninakuheshimu, Ninakushukuru’. Na kama vile wewe unavyokimbia kwa lengo la kuniletea mimi uhai, mimi napenda nitoe uhai wangu uwe kwa ajili ya kutetea Uhai Wako, na napenda nikuombe sherehe ya ushindi wa Utashi Wako. Wakati huu unapokimbia, Ewe Pendo Langu, naonja moyo wangu ukipasuka, ninapokuona ukilia kwa uchungu, ukihema na ukitehemu. Moyo wangu unapasuka ninapoona jinsi unavyotafutwa, siyo kwa lengo la kukupatia mahali pa kulala, bali kwa lengo la kukuua. Mimi napenda nitulize machozi yako kwa pendo langu. Napenda pia kutwaa uwezo wa kuwa mahali mbalimbali katika Uumbwa kwa wakati ule ule. Kwa mfano, ili kukufurahisha, ninapenda usikie ‘Nakupenda’ yangu ikitokea toka kule ndani ya bahari. Mimi mwenyewe nikiwa ninahamasisha, kwa sauti yangu, matone yote ya maji, michezo yote ya samaki, napenda uwe unasikia ‘Ninakupenda’ ya viumbe vyote visivyo na sauti vinavyoishi pale baharini, na napenda usikie pia ule musiki wangu mzuri wa pendo, unaopita misiki yote, musiki wenye kile kiitikio changu: Ninataka FIAT Yako. Kwa wakati moja na uleule nataka niwe ndani ya Utashi Wako, juu ya ile milima mirefu kabisa, na katika mabonde yale ya kina kirefu. Nataka nikahamasishe mimea, maua, miti na mengine yote. Hao wote nataka wasikike wakisema: ‘Ninakupenda, Ninakupenda’. Juu ya mabawa ya Upepo ninapenda nikatengeneze sauti kali kupita zote ili Wewe uwe unasikia kauli ya ‘Ninakupenda’. Na katika mawimbi ya upepo nataka nipakie mabusu yangu motomoto na mapapaso yangu ya upenzi kwa ajili yako.
Ewe Mpenzi Wangu Mdogodogo, wakati wote unapotoroka, iwe usiku, iwe mchana, Wewe upo hadharani na unaonekana daima. Kwa hiyo ni vema tu kama mimi nipange kuviita vitu vyote vilivyoumbwa ili waje kumfurahisha Muumba wao. Basi ninaita sasa mwanga wote wa Jua. Unapoangazisha Uso Wako mzuri unatoa kauli kusema: ‘Ninakupenda’. Ninawaita na ndege wote waliopo angani, ili kwa nyimbo zao na sauti zao za kutetemesha, waweze kukutungia bembezi za pendo. Yaani tuseme, ninapenda nikupeleke hadi Misri ukiwa unasindikizwa na shangwe la ushindi la pendo langu, na kama kiitikio chake, ninakuomba Ufalme wa Utashi Wako. Sipo peke yangu, Ee Yesu, bali nipo pamoja na kazi zako zote. Je hivi husikii jinsi ilivyo nzuri na inavyopendeza: bahari, upepo, jua, nyota zinazometameta, vyote vikisema ‘Ninakupenda’? Anga, milima, mimea, vyote kwa pamoja na baina yao hupiga kelele kwa kadiri vinavyoweza vinasema: “Ninakupenda, Ninakupenda, tunautaka Utashi Wako unaotawala na unaoamrisha!”. Na mwangwi huo unasikika ukirudiwa katika kifua cha Mama Malkia na hata yeye anakuambia hivi: “Mwanangu, pendo langu hupatanisha na kuoanisha kila kitu, huunganisha tena vitu vyote, hushinda yote, na mwangwi huo unapopenya hadi ndani ya Moyo Wako, nao unakuomba FIAT Yako.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...
SAA YA KUMI NA MBILI

Tupo na Yesu pale Misri; tunamtolea moyo wetu uwe makao yake, na pamoja na Malkia wa Mbingu, tunaomba Ufalme wa Utashi wa Mungu.

Mpenzi Wangu Mtoto Yesu, wakati mimi bado ninakufuata nakuta umekwisha kuwasili tayari pale Misri. Natambua kuwa popote unakoelekea unafuatwa na mateso, na machozi, na kusahaulika, kuachika na watu wote, kiasi kwamba unapasika kuingia kujihifadhi katika kibanda kidogo na duni sana; hakijawahi kukarabatiwa wala kusafishwa, hakina madirisha. Kinapigwa na pepo na huwa kinavuja maji wakati mvua zinaponyesha. Hakuna hata mtu mmoja duniani hapa anayekupa malazi. Oh, ni jinsi gani unavyolalamika, Ewe Mtoto Wangu Mchanga kabisa, unapoona kuwa Ubinadamu Wako mdogo unakabili mkasa ule ule wa Utashi Wako Mwabudiwa, yaani, kwamba hakuna mtu ambaye, kwa ukarimu na uhuru wake, anatoa nyumba ya roho yake ili kuukaribisha Utashi wa Mungu na kuuruhusu utawale pale na kuamrisha. Ingawa kama umekwisha kufika kati yao, hata hivyo, unaonekana kuwa kama mtangatangaji tu. Kwa miaka zaidi ya elfu sita, amekuwa akiomba nyumba bila kufanikiwa kupata. Na Wewe, Pendo Langu, unalia kwa ajili ya mateso ya FIAT Yako ya Kimungu.

Ewe Mdogodogo Wangu wa Mbinguni, unaona kuwa Mama yetu, wakati anapolia pamoja Nawe, yeye anaficha machozi yake ili kunyamazisha kilio chako. Anatolea roho yake safi kabisa kabisa iwe ndiyo makao ya kudumu ya Utashi Wako wa Kimungu. Hata mimi ninafuatilia kilio chako. Ninapenda nipanguse na kukausha huo Uso Wako Mtukufu wa kupendeza. Nataka nibandike mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu juu ya kila chozi, juu ya midomo ile inayotetemeka na inayolalamika. Kadhalika napenda kubandika na busu langu la upenzi. Nataka kukuomba FIAT Yako na ninakutolea moyo wangu uwe kama makao ya kudumu daima ya FIAT Yako ya milele.

Mtoto Wangu Mpendwa, uliye makao makuu ya uhai wangu, wakati wote unapoishi katika kibanda hicho duni, ninapenda kufuatilia matendo Yako yote, nafuatilia pia matendo ya yule Malkia Mtawala Mkuu wa Mbinguni. Wakati yeye anakubembeleza kwa kukutikisatikisa, na mimi nitapenda kukubembeleza kwa kukutikisatikisa na kukuimbia ili upate usingizi. Wimbo wangu ni huu: ‘Ninakupenda, Ninakupenda’. Wakati anapokuandalia kashati kakukuvalisha, mimi, katika ule uzi anaopitisha katika vidole vyake vya kimama, wakati wa kushona, nataka nitiririshe humo ile kauli yangu ya ‘Ninakupenda, Ninakuheshimu, Ninakushukuru, na Ninakuabudu’ kusudi wakati Mama yetu wa Kimungu atakapokuwa anakuvalisha, Wewe uwe unaonja kuwa vazi lako limeshonwa pamoja na ‘Ninakupenda’ yangu ambayo inakuomba FIAT Yako.
Ewe Moyo wa moyo wangu mdogo, wakati utakapoanza kujimudu na zile hatua za kwanza za kuyumbayumba, mimi napenda nitilie mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu, juu ya ile ardhi utakayokuwa unaikanyaga, ili kusudi uwe unasimama juu ya miguu yako mwenyewe. Na kwa mikono yangu, nitatengeneza uzio ili kukulinda na kukutegemeza usije ukayumbayumba na kuanguka. Ikitokea unayumba, mimi nitaweza kukukumbatia na kukubania kwenye moyo wangu. Ninagundua, Ewe Mtoto Wangu wa Mbinguni, kwamba mara baada ya kuacha kunyonya, na wakati huo ukiwa na uwezo wa kutembea mwenyewe, hata kama ungali bado ni kadogodogo, wewe unatoka na kujitenga na Mama kidogo, unapiga magoti yako madogo juu ya ardhi tupu, na huku ukipanua vimikono vyako vidogo, unasali, na unalia kwa ajili ya wokovu wa watu wote, na kwa kusihi sana na kuomboleza, unaomba Ufalme wa Utashi Wako wa Kimungu. Na kamoyo kako kadogo, kanapiga kwa nguvu kweli, kana kwamba kanataka kupasuka kwa sababu ya pendo na maumivu makali. Ewe Yesu Wangu Mdogo, ebu uniache tu mimi niweke kauli yangu ya ‘Ninakupenda’ hapo chini ya magoti yako madogo, kusudi hiyo ‘Ninakupenda’ yangu ilainishe na kulowesha kidogo hiyo ardhi isiwe kavu na ngumu mno kwa ajili ya viungo laini vya mwili wako. Tafadhali uniruhusu nitie mhuri wa ‘Ninakupenda’ yangu katikati ya mikono yako iliyopanuliwa na uniruhusu niishikilie hiyo mikono yako midogo miwili kwa mikono yangu ili usiteseke mno. Na wakati huo ninaposhikilia mikono yako, Wewe, Ee Mpenzi Wangu, unitwae mie kwa mikono yako hiyo midogo na unitolee kwa Baba wa Mbinguni, unitolee mimi Binti Mdogo wa Utashi Wako, huku ukinijalia nipate neema hii kwamba Utashi wa Mungu utawale ndani yangu mimi na ndani ya wanadamu wote.

Baba yetu...,
Salamu Maria...,
Atukuzwe Baba...