Utashi wa Mungu na Upendo wa Mungu - Luisa Piccarreta
42 subscribers
289 photos
54 files
586 links
Fahamu kuhusu kutimia kwa Sala ya Baba Yetu kupitia Maandishi ya Mtumishi wa Mungu Luisa Piccarreta, Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - Kuishi Utashi wa Mungu
Download Telegram
Mtumishi wa Mungu
Luisa Piccarreta
inti Mdogo wa Utashi wa Mungu

“Ee Yesu, miguuni pako nakuletea uabudu na utiifu wa familia yote ya wanadamu. Ninaweka ndani ya Moyo Wako ile kauli ya ‘Nakupenda’ kutoka kwa watu wote. Juu ya Midomo Yako nakupigia busu langu, ili kukubandikia mhuri wa busu la watu wa vizazi vyote. Kwa mikono yangu nakukumbatia, ili kukubana kwa kumbatio la mikono ya watu wote, kwa ajili ya kukufikishia utukufu wa matendo yote ya wanadamu”

(Kutoka: KITABU CHA MBINGU, Juzuu Na. 12 - Mei 22, 1919)
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 28
Kwa Mheshimiwa Padre Msaidizi

Fiat

Mheshimiwa sana Padre Msaidizi,

Kutoka kwa Mwalimu mwema Angela La Stella nilipata karatasi lako lililokuwa na ombi lako la kutaka nikusaidie kidogo kwa sala zangu, na kwa Komunyo yangu Takatifu nk. kwa ajili ya kazi zako za kipadre.

Basi, tangia tarehe 20 Oktoba hadi leo hii, katika kila kitu nilichoweza kutekeleza katika umasikini wangu, nimekuwa ninaweka nia ya kutenda kwa ajili yako, yaani Misa Takatifu zote, Komunyo Takatifu zote na mengineyo.

Na ili nia yangu hiyo iweze kuwa na thamani zaidi, na ili iweze kukuletea wewe matunda ya utakatifu wa kweli, matunda ya neema za kushangaza na usizotegemea, nilimwomba Yesu awe anatenda kila kitu pamoja nami ili pamoja na zawadi za kwangu, niweze kukutolea zawadi za Yesu Mbarikiwa.

Nilifanya hivyo kusudi Upadre wako ujaliwe neema hizo zaidi na zaidi.

Kutokana na hilo, ninapenda kutumia nafasi hii kukutumia Heri nyingi sana kwa Sikukuu ya Somo wako na ninamwomba mpenzi Yesu abebe na kukuletea Yeye Mwenyewe zawadi hizo.

Zawadi anazokuletea kama Heri zangu ni hizi: ‘FIAT’ ndani ya moyo wako, ‘FIAT’ katika maneno yako, na ‘FIAT’ katika akili yako, ili hatimaye hiyo FIAT iiongoe nafsi yako yote na kuiumba upya nafsi hiyo hata iwe ni kitendo kimoja tu cha Utashi wa Mungu.

Na kutokea hapo wewe uwe ni mtu unayebeba Utashi wa Mungu na kuupeleka kwa watu wote.

Ni Utashi huo ndio unaoweza kuingiza amani, umoja, na utakatifu ndani ya watu wote.

Tunaonja sana hitaji kali kabisa la kupata utakatifu wa kweli, hasa hasa ndani ya Padre.

Na ni ‘FIAT’ ya Mungu peke yake ndiyo yenye kuweza yote, kwa vile ndiyo inayomiliki maweza yote.

Maweza hayo yapo katika nguvu yake na uwezo wake wa uumbaji.

Ndiyo inayoweza hatimaye kuleta na kuingiza ndani yetu ngazi na daraja la kweli la utakatifu.
Nakuomba na ninajikabidhi katika sala zako takatifu.

Na sasa, kwa heshima, nikibusu shavu lako la kulia, na nikipiga magoti mbele yako ninakuomba sana baraka yako ya kibaba. Ndimi,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 67.
Kwa Federico Abresch, wa Bologna

Fiat! – In Voluntate Dei!

Mpendwa Mwanangu katika Utashi wa Mungu,

Kwa Mama yeyote, aliye na watoto wake wanaokaa mbali, faraja pekee anayoonja ni pale anapofahamu kwamba watoto hao wanapenda kuishi katika Utashi wa Mungu.

Ninawaza ni jinsi gani Yesu Mpendwa anavyotamani jambo hilo, na ninafikiri pia kuwa msumari unaomchoma na unaomtoboa Yesu zaidi, ni pale watoto wake wanapokosa kuishi katika Utashi Wake.

Na lakini, yule Malkia wa Mbinguni angefanya nini kama angetuona sisi tukiishi pamoja Nao ndani ya utashi ule ule mmoja?

Ni hakika kabisa wangetuletea sisi uhai ili uwe mali yetu na ili tuufaidi. Hivyo ndivyo kuishi hasa katika Utashi wa Mungu.

Mungu Mwenyewe huchukua mambo yetu yote na kuyaweka moyoni mwake, na badala yake anatupatia utakatifu wake ili tupate kuufaidi, anatupatia Pendo lake, anatupatia Nafsi yake, ili mradi afurahie kutuona sisi tukiishi ndani ya ule Utashi Wake ambao ndio unaotuletea mema yake yote.

Mpendwa katika Utashi wa Mungu, kuishi katika Utashi wa Mungu haimananishi kubadili vitendo vyetu bali ni kubadili utashi tu: badala ya kuacha utashi wetu ushike hatamu katika vitendo vyetu, yatakiwa tuache Utashi wa Mungu ushike hatamu katika kila kitu tutendacho.

Na je wewe unataka kufahamu ni nini kinachotokea katika kila kitendo chetu?

Pendo la Mungu ni kubwa hivi na pia Wema wake ni mwingi hivi kiasi kwamba kila tunapoanza sisi kutekeleza tendo lolote huku tukihusisha Utashi wa Mungu, hapo hapo Uhai wa kimungu huanza kutengenezwa ndani ya hilo tendo letu.

Na uzima huo wa Mungu hurudia kutengenezwa katika matendo yetu, mara zote tunapotekeleza tendo letu lolote lile.

Je unadhani ni neno dogo nikikuambia kuwa, ili mradi nikiruhusu Utashi Wake ushike hatamu, Mungu huwa ananipa uwezo na nguvu ya kutengeneza Uhai mwingi wa kimungu katika matendo yale yote ninayofanya?

Muujiza huo mkubwa hutokea kila mara, iwe katika vitendo vya kimaumbile na vya kawaida au katika vitendo vidogo vidogo, ili mradi tu pawepo na Utashi Wake.

Na mintarafu udhaifu wetu, mahangaiko yetu na mengineyo, usijali sana. Bora tu pasiwepo utashi wetu sisi kwa vile ndio huo unaotuharibia mambo yetu.

Matatizo na shida zetu hizo zote vinaweza kutumika na Mungu kama kikanyagio au kikalio ambapo Utashi wa Mungu hutengenezea kiti chake cha mamlaka na cha utawala juu yetu sisi wenyewe.

Au ni kama vile kokoto na vifusi vya vipandevipande vya mabomoko ya jengo vinavyoweza kutumika na mtu anayeanza kujenga nyumba yake.

Au pia ni kama udongo ulio mkiononi mwa Mungu aliye ni Mkulima wa mbinguni, ambaye bila utashi wetu sisi, anatumia shida na matatizo yetu na kuyafanya yachanue maua mazuri ya kupendeza kwa ajili ya usitawi wa Ufalme Wake. Katika mikono ya kimungu ya FIAT, kila kitu kinatumika kwa ajili ya utukufu wake Mungu na kwa ajili ya manufaa yetu sisi.

Hata hivyo, ninakushauri usiwe unawaza mno juu ya matatizo, shida na mapungufu yako. Kwa jinsi unavyozidi kuyafikiria hayo, ndivyo yatazidi kukuelemea na kukukandamiza moyoni.

Kumbe lakini, kwa jinsi unavyoacha kuyawazia, ndivyo yatazidi kufifia na hivyo yataacha kukutesa.

Zaidi ya hilo, elewa kwamba Yesu Mtamu huwa hatazami na kupima kile tunachoonja bali anapima zaidi kile tunachopenda.

Yaani, mara nyingi anatuonea huruma na anatuongezea Neema yake na nguvu yake hata kuyafanya matatizo na shida zetu zigeuke kuwa neema na nguvu yetu.

Na hatimaye, Yesu Mpenzi, kwa vile anapenda sisi tuishi katika Utashi Wake, huwa hapendi kujihusisha na wale waliokufa, bali anajihusisha na wale walio hai.

Kwa sababu hiyo, matatizo na shida zetu ni ishara tu kwamba tupo bado hai na wala hatujakufa bado.

Na Yeye, kwa vile anataka ajitokeze kama Mshindi, anayashinda matatizo hayo na anayageuza kuwa mapambo mazuri kabisa ya Ufalme Wake.
Kwa hiyo basi, jipe shime, uwe na ujasiri na uwe na imani.

Hizo ndizo silaha zinazomshinda hata Mungu.

Endapo hatutatekeleza hatua za awali, hatutaweza kufanya hatua ya pili, na ya tatu, na nyingine nyinginezo zinazofuata.......

Kama hatutajitumbukiza baharini, basi hatutaweza kuoga wala kuogelea ndani yake.

Basi, lililo muhimu ni sisi kuanza kwa dhati; mengineyo yatafuata yenyewe. Najikaabidhi sasa katika sala zako.

Umwambie na huyo mtoto mdogo Pio kwamba katika kila kitu atendancho awe anasema hivi: “Yesu, utwae utashi wangu na unipe Utashi Wako”.

Umsaidie na kumlea awe mtakatifu ili awe kweli kweli mtoto wa Utashi wa Mungu.

Ninaikabidhi familia yote katika Utashi wa Mungu.

Kwa njia hiyo utajipatia wewe mwenyewe ile neema ya kuujua zaidi huo Utashi wa Mungu.

Nawatakieni ninyi nyote salamu za FIAT.

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 23
Kwa Mama Cecilia
25 Februari, 1933

Y.M.Y.A. – Fiat
I.V.D. D.G.

Mheshimiwa Mama yangu Mpendwa,
Unisamehe kwa kutokukuandikia barua, lakini uwe na uhakika kuwa mimi huwa sikusahau mbele ya Bwana Wetu ili akupe daima nguvu na neema unazohitaji katika majukumu muhimu na magumu kabisa aliyokukabidhi.

Mimi ninatarajia kuwa kazi yako ya kwanza kabisa ni kuwalisha mdomoni manovisi wako kwa mkate wa Utashi wa Mungu.

Lakini, ndani ya mkate huo unaowalisha, ni budi uwe unatia dosi kali za viungo vya upendo. Uwe ni upendo wa kimbingu kabisa.

Utie pia dosi za viungo vya utamu wa Yesu toka mdomoni pako ili hata manovisi wawe wanapata na wanaonja ladha ya utamu huo.

Kwa nguvu ya dosi hizo, maneno machache wanayopata manovisi toka kwako yawe yanawatosheleza kwa ajili ya kuwafanya wawe watakatifu.

Ikiwa hivyo, hawatakuwa wanakwenda kutafuta semina ndefu ndefu ambazo, ingawa kama huwa zinavutia masikioni, lakini huwa mara nyingine zinaacha roho za wasikilizaji katika hali ya njaa na kiu.

Mama mpendwa sana, kwa niaba yangu uwaeleze manovisi kwamba wasiwe wanatafuta na kuokota vijiti vidogovidogo na nyasi nyasi kavu, bali wawe wakitafuta ule mkate wa mbingu ambao Yeye Yesu Mtamu hupenda kuwapatia kwa njia ya wewe, yaani ule mkate wa FIAT Kuu.

Na wala Yesu hatawauliza jambo lingine isipokuwa jambo hili, yaani: Je, katika kila tendo Mapenzi ya Mungu yalitimizwa?

Mama mpendwa, kama wewe unavyofahamu vema kuliko mimi, neno muhimu kupita yote ni kutokugomea chochote mbele ya Utashi wa Mungu.

Kugomea gomea jambo fulani, kukataa kutawaliwa na Utashi wa Mungu ina maana ya kubomoana na kuvunjavunja utakatifu; ni sawa na kufanya utakatifu uwe vipande vipande kiasi kwamba sisi wenyewe tusiweze tena kuelewa namna ya kupata utakatifu.

Tutageuka kuwa ni mwili ambamo viungo vyake vya mikono na miguu yake na hata moyo wake vimeng’olewa.

Oh, utakatifu gani duni wa jinsi gani huo ambamo hakuna uhai kamili wa Utashi wa Mungu?

Kwa hiyo, Mama yangu, ebu tuwe tunaupenda sana sana Utashi wa Mungu, tuwe tunautekeleza daima.

Hata kama itagharimu uhai wetu, mbona tutarudishiwa uhai ulio bora na mzuri zaidi?

Ebu tujitahidi kushughulika ili kuufanya Utashi huo wa Mungu ujulikane na kupendwa na watu wengine.

Hebu sasa turejee kwenye jambo letu linalotuhusu.

Mimi sisadiki kwamba kumetokea na wala kwamba kutatokea namna yeyote ile ya kivuli cha kugombana au kuchukiana.....
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 90
Kwa Sista Remigia

Fiat

Binti yangu mpenzi Sista Remigia,

Ninakuomba usiwe unapoteza muda. Oh, ni jinsi gani ningependelea kusikia ukisema: “Mimi siwazii iwapo nipo mzuri au kama napendeza au iwapo sipendezi. Wala siwazii iwapo naona ubaridi au naonja joto. Wazo langu ni moja tu, yaani ni kwa namna gani ninavyoweza kutiririsha matendo yangu yote na hata nafsi yangu mwenyewe ndani ya Utashi wa Mungu”. Ikiwa hivyo basi ni Yesu Mwenyewe atafikiria namna ya kukufanya wewe kuwa mtakatifu na ni Yeye atakayekufanya uwe na utulivu endelevu katika mambo yako, atakufanya uwe mwema kadiri anavyotaka wewe uwe. Kwa mara zote unapojifikiria juu yako wewe mwenyewe, hata ikiwa ni katika mambo mema, Yesu hatathubutu kukufunga kamba au hatamu, na kukuongoza kwa lazima, ili akufanye uwe Yesu wa pili atakayekuwa ni mrudufu wa uhai wake. Umwachie kazi hiyo aifanye Yesu Mwenyewe, na upesi sana wewe utajionea mwenyewe, jinsi unavyobadilika kuwa mtu mwingine kabisa, tofauti kuliko ulivyo sasa hivi. Yesu anajua namna ya kufanikisha zaidi jambo hilo kuliko tunavyoweza kufanya sisi wenyewe. Kwa hiyo, umwachie tu atekeleze Yeye.

Ninapenda kukutumia matashi yangu na ushauri wangu. Lakini je unajua ni matashi gani hayo? Ni matashi na ushauri wangu kwamba sasa usiwe kamwe unajifikiria wewe mwenyewe ndani yako, bali sasa ujifikirie daima ndani ya Yesu. Oh, ni jinsi gani Yesu atakavyokupenda! Atakubeba mikononi mwake, na atakupatia kiti cha kukaa ndani ya Moyo wake mdogo. Uwe makini na endelea kuishi ukiwa umejikabidhi nafsi yako kikamilifu kabisa ndani ya Yesu.

Ninakuaga, ni mimi,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 125
Kwa Monsignor
10 Januari, 1944

Mheshimiwa sana Monsinyore,

Mimi sielewi bado namna ya kukushukuru kwa heshima yako ya kunijali hata ukaweza kunikumbuka mimi mtumishi mdogo sana wa Yesu.

Sielewi namna ya kukulipa kwa hilo. Kitu kimoja tu ninaweza kufanya, nacho ni kusali nikimwomba Yesu Mpenzi akusaidie uweze kuishi katika Utashi wa Mungu, kwani ni huu Utashi wa Mungu peke yake ndio unaoweza kutufanya tuwe na furaha na pia ndio unaweza kutufanya tuwe watakatifu kwa nguvu ya utakatifu wake wenyewe.

Zaidi ya hilo, ni kwamba tamanio moja tu la Yesu ni hili kuwa sisi tuishi katika Utashi Wake kwa vile, kama tunaishi ndani ya Utashi Wake, Yeye ataweza kutupatia kitu kile anachopenda kukitoa kwetu.

Yesu anapenda kututengeneza na kutufinyanga upya katika Pendo lake, lakini kwa bahati mbaya utashi wetu wa kibinadamu ni mdogo mno hata hauna nafasi na mahali pa kumweka. Yesu anataka atupatie neema lukuki, lakini utashi wetu hauna uwezo wala nguvu za kuzipokea neema hizo.

Kwa hoja hiyo, Yesu, anatamani kuuona Utashi Wake Mtakatifu ndani yetu, siyo tu kwa lengo la Yeye kuweza kutupatia sisi kile atakacho, bali ni kwa lengo la kutufanya sisi kuwa kivuli halisia au nakala halisia ya Yeye mwenyewe.

Ni kwa sababu hiyo, anapotuona tukiwa tayari katika Utashi Wake, Yeye husherehekea na kusema: “ Hatimaye nimeweza kupata mahali pa kuweka nafsi yangu. Utashi Wangu hapa utaweza kuhifadhi vizuri neema zangu, Pendo langu, na hata Utakatifu Wangu”.

Basi, Padre mwema, ebu kwa moyo wetu wote tupende kuishi katika Utashi wa Mungu.

Utashi huu utakuwa unatuhifadhi sisi daima, utakuwa unatukinga na hatari zote, na utakuwa unatuweka huru dhidi ya mabaya yote.

Oh, laiti watu wote wangalijua nini maana halisi ya kuishi katika Utashi wa Mungu!

Wote wangekuwa wanapania kuupata na kuishi ndani yake na hapo mabaya yote yangekoma mara moja na pale pale!

Hayo ndiyo matashi yangu mema ya Mwaka mpya kwako. Ya kwamba uweze kuishi daima katika Utashi wa Mungu na kwamba Yesu akufanye wewe uwe mmisionari wa Utashi wa Mungu.

Uniwie radhi kwa maneno yangu hayo, ambayo labda huenda nikawa nimekosea katika kukueleza. Kwa mara nyingine napenda sana nirudie shukrani zangu.

Na sasa napenda nikuage nikikukabidhi ndani ya bahari ya Utashi wa kimungu, katika mikono ya Yesu, na ndani ya bushuti la Mama Malkia wa mbinguni.

Ninabusu shavu lako la kulia, na nikipiga magoti, nakuomba baraka yako ya kibaba. Ndimi.

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu.

Corato, 10 Januari, 1944
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 57
Kwa Mama Cecilia, wa Oria

In Voluntate Dei! [Katika Utashi wa Mungu!]

Mama yangu mwema na Mheshimiwa sana Mama,

Hapa napenda kujibu barua yako ya upendo sana. Ni mshangao na furaha ilioje kwangu kukusikia ukinieleza kuwa katika jamii sasa kunatawala amani na utiifu! Kama kuna amani, maana yake kuna Mungu! Watoto wake ni kama sasa wameokwa katika amani. Kwa hiyo hao wote ni vyombo vya amani, yaani ni watu wa kueneza amani kwa wengine. Maneno yao na namna ya mwenendo wao havitaleta kadhia, maudhi na uchukivu, bali huwa ni maneno na matendo yaliyopakwa mafuta ya uponyaji yenye kuleta amani, yenye kunogesha mioyo ya wale walioelemewa na uchungu zaidi. Katika jamii kama hiyo wale wanaokuwa wachokozi na wakorofi watajionja mara wamepoteza mapembe yao na wanapumbazwa mbele ya mtu yule aliye mtulivu na mwenye roho ya amani. Na unajua Mama yangu, kuwa amani, ni ishara tosha kuwa mahali hapo ni Utashi wa Mungu ndio unatawala, au kama uhai, au walau kama fadhila na nguvu. Wakati Utashi wa Mungu unakwenda kutawala ndani ya mtu fulani, kwanza kabisa hutuma ujumbe wake wa amani. Maana yake, mara nyingi huanza kwa tendo la kufumbia macho mambo ya vineno vineno, magomvigomvi, uvivuuvivu na vimakosamakosa ili kusudi tusipoteze amani wala muda. Na hivyo FIAT ya Kimungu hupata wasaa wa kutengeneza njia ndani ya roho yetu na huanza kujenga pale kiti chake cha ikulu na uhai wake, na hatimaye hueneza hapo himaya yake. Oh, ni jinsi gani ningependelea kama wewe mama yangu uliye mbali unifurahishe kwa jambo hili, yaani, wewe uwe ni tendo moja tu la Utashi wa Mungu na uwe ni chombo cha kupeleka huo Utashi wa Mungu kwa watoto wako wote........ Hapo sadaka yangu ya kumwacha mama abaki mbali nami, na sadaka ya kumkosa hapa, itapunguza machungu yake, kwani nitakuwa nikifikiria kuwa mama yangu yupo katika utume maalum wa kuwasaidia watu waujue Utashi wa Mungu. Na mimi, toka hapa nilipo, nitakuwa nasali, nitakuwa namsindikiza, na nitakuwa ninasimama dirishani kuchungulia ili niyaone matunda ya utume huo wa mbinguni. Kwa sababu hiyo, wakati barua zako zinapoigusa tu FIAT kwa ajili yangu mimi, mimi hapo hapo najisikia kushituka kwa furaha katika moyo wangu, na hapo ninasema: “Nitamwacha Mama abaki bado mbali nami, kwani ananifaa walau kwa ajili ya Utashi wa Mungu”.

Ebu sasa tuzungumzie mambo yetu. Nilikuwa nimekutumia zile anuani 23. Nasadiki ulizipata na utakuwa umewaandikia na kuwatumia tayari. Nilikuwa nimekutumia pia maandishi mengine kwa ajili ya matangazo ya usambazaji. Kama utakuwa unahitaji bado matangazo mengine, nieleze nami nitakutumia.

Ebu sikiliza mama yangu, ninataka nikufundishe ukorofi mtakatifu: Kwa kila ‘Ilani ya Malkia wa Mbingu’ na kwa kila Kitabu utakachokituma kwa mtu, uwe unamwambia huyu Bibi wa mbinguni kuwa unamtuma na kumwagiza akuletee zawadi ile kuu ya Utashi wa Mungu. Kwa njia hiyo, kila ‘Ilani’, kila Kitabu, vitakuwa ni rehani ya ziada utakayokuwa unaikabidhi katika mikono yake ya kimama, siyo kwa ajili ya wewe mwenyewe tu, bali hata kwa yeye yule uliyempelekea Kitabu na hiyo Ilani. Na yeye Malkia Mwenye Mamlaka, atakapokuwa anatazama na kuona rehani nyingi vile mikononi mwake, atajionja amefungwa na anadaiwa kwa lazima. Basi atakupatia kile ambacho Yeye mwenyewe hupenda kukupatia, yaani atakupatia Utashi wa Mungu kama uhai.

(.....) Jamii yangu yote ya hapa inakusalimu, Padre Benedetto anakubariki kwa moyo wote na mimi, nikikuacha umechukuliwa na Utashi wa Mungu, ninakubusu kwa shavu la kulia na ninasema,

Ni wako katika upendo kabisa,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 79
Kwa Padre Ludwig Beda, O.S.B.,
Kloster Andesch, Germany
30 Aprili, 1939

In Voluntate Dei

Mheshimiwa sana Padre,

Yesu anakuambia ‘Asante sana’ kwa ukarimu wako katika kuniandikia barua. Ni faraja ilioje uliyoleta katika roho yangu duni na kwa Padre wangu mwungamishi Don Benedetto! Sisi sote tumekuwa katika kipindi kigumu sana. Yesu Mwenyewe alilia kwa uchungu na ndani yangu moyo unapasuka ninapomwangalia akilia. Ilikuwa ni alama kubwa ya upendo kutufunulia kile ambacho Mama Malkia wa mbinguni alikuwa akianza kutuletea ili kutuonyesha jinsi anavyotupenda na jinsi alivyotamani kabisa moyoni mwake kutufundisha sisi namna ya kuishi katika Utashi wa Mungu, pia kutufundisha namna ya kukua na kukomaa ndani yake, na jinsi alivyokuwa anataka kutulisha kwa chakula cha FIAT ya kimungu.

Hapa Italia, wakati kilipotoka kitabu kile ‘Malkia wa Mbingu Katika Ufalme wa Utashi wa Mungu’, ndipo huyu Mama mwema alipochukua hatua ya kwanza ya kutuwezesha kufahamu jinsi anavyotupenda, kiasi cha kutuingiza na kutuchukua sisi tumboni mwake, ili toka pale atupatie kile kitu cha manufaa ambacho yeye ndiye anayekibeba. Kwa bahati mbaya lakini, njama za maadui wa kitabu chake hicho walizuia hatua hiyo isiendelee kutekelezwa. Yeye mwenyewe akarudishwa na kupelekwa tena katika pande zile za juu mbinguni. Toka pale juu, kwa subira isiyoshindikana, yupo anangojea kwanza yafike mabadiliko ya nyakati, mabadiliko ya watu na mabadiliko ya mazingira, ili hatimaye mambo yake yaweze kuchukua mkondo wake na ili aweze kutoa na kutupatia kitu kile ambacho hata sasa kinadharauliwa na watu.

Mheshimiwa Padre, ni mapenzi na uamuzi wa Mungu kwamba Ufalme wake ufike hapa duniani; kwa hiyo ni uhakika kabisa kwamba utafika, iwe kwa njia ya upendo au kwa njia ya adhabu. Vinginevyo, uumbwa utakuwa ni kazi itakayokuwa imekosa kupata taji lake. Mbele ya viumbe vingine vyenye nguvu ya kujiongeza na kujizidisha, Mungu angeonekana kana kwamba hana uwezo wowote kama Utashi Wake wa kimungu ungeshindwa tu kuzindua Uhai wake Mwenyewe ndani ya roho zetu sisi. Hapana. Hilo haliwezekani kamwe. Tuna uhakika kwamba Ufalme wa Utashi Wake utafika kwa vyovyote...
Bikira Maria Katika Ufalme Wa Utashi Mungu ⬇️⬇️⬇️ - A5 format

Imetolewa katika Sikukuu ya Huruma ya Mungu, Jumapili tarehe 11 Aprili 2021

SALAMU MARIA!
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 56
Kwa Bw. Vincenzo Messina, Mfungwa katika Gereza la Favignana, Trapani

Fiat

Mpendwa sana Ndugu yangu katika Yesu Kristu,

Nimefurahishwa sana na ombi lako la kupata Kitabu cha Malkia wa Mbingu. Nimekuwa nawaza kwamba Mama wa mbinguni anakuja hata katika gereza kufanya ziara yake ya kuwatembelea kama Mama, kama Mwalimu, na kama Mfariji na pia kwa ajili ya kuwasindikizeni na kukesha pamoja nanyi na hata kwa ajili ya kuwafundisheni namna ya kuishi Utashi wa Mungu na namna ya kuujenga Ufalme wa Utashi wa Mungu hata hapo gerezani.

Kwa hiyo ndugu yangu, jipe moyo, uwe na imani na matumaini, kwani unaye Mama wa mbinguni ambaye anakupenda mno, ambaye hatakuacha kamwe peke, na kama utamsikiliza, atageuza hiyo gereza kuwa kikanisa cha hija takatifu. Na kama udhaifu wa kibinadamu umekupeleka gerezani, yule Malkia Mwenye mamlaka anakuja kwa nguvu ya Utashi wa Mungu ili akutoe na kukuongoza kwenda mbinguni na kufanya siku zako ziwe na maumivu yaliyopunguka. Yaani, maumivu yako, kuachika kwako, kukosa mahitaji, upweke wako, yeye Mama atavibadilisha viwe ni hati za uhuru na ushindi wa milele. Atakusaidia uonje amani ambayo huwa huwezi kuipata na kuifaidi hata unapokuwa duniani. Utashi wa Mungu utakubadili wewe na utaanza kuonja uhai mpya ambao atakuletea yule Mama wa mbinguni.

Ni vema pia ujue kuwa hata mimi hapa ni dada yako mfungwa wa gerezani. Tangu zaidi ya miaka hamsini FIAT Kuu imenifunga mimi hapa ndani ya kitanda. Hata hivyo ninaridhika na ninafurahi. Lakini je ni nani anayenifanya nifurahi? Ni Utashi wa Mungu ambao najitahidi kuutekeleza daima. Hata wewe unaweza ukawa na furaha endapo utatekeleza Utashi wa Mungu. Oh, ni jinsi gani utakavyobadilika huo uchungu wako! Utaanza kuonja nguvu ya kweli ya kimungu, ambayo itarahisisha sana hali yako hiyo ya mateso.
Kamwe usiache kusali Rosari kwa Mama wa mbinguni, na kama utaweza, basi uwe wewe ndio mmisionari hapo gerezani kwa kujitahidi kuwafahamisha wenzako kwamba Malkia wa mbinguni anataka kuwatembelea ninyi wafungwa wote ili awapatieni ninyi nyote zawadi ya Utashi wa Mungu. Endapo mngehitaji nakala nyingine ya Kitabu, na iwapo ninyi hamtaweza kulipa fedha yake, mimi nipo tayari kuwatumia nakala hizo bila kudai malipo yeyote.

Nakukabidhi ndani ya bushuti la Mama yetu wa mbinguni ili uwe unasikiliza mafundisho yake ya Mbingu.

Na kwa salamu elfu na elfu nasema ni mimi dada yako mpendwa kabisa,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 03
Kwa Mama Mkubwa, Sr Maddalena del Moro, wa Santa Chiara, Ravello
20 Novemba, 1917

Y.M.Y.

Utashi wa Mungu uwafunge sana sana hata msiwe na muda wa kuwaza juu yenu ninyi wenyewe.

Dada yangu katika Yesu Kristo,

Kwa mistari hii michache napenda kujibu barua yako. Mimi naamini kuwa kinachosababisha yote hayo unayonielezea ni kukosekana kwa muungano na Yesu katika mambo yako yote. Adui anakukuta ukiwa peke bila Yesu, na ndipo anatenda kazi yake chafu, anakusumbua, anakuondolea amani ya moyoni ambayo ni ya lazima kwa ajili ya kumpumzisha Yesu Mteseka. Huyu adui angekukuta upo daima na Yesu, hakika angetoroka na kukimbia ili asiteseke na ule uwepo mwabudiwa wa Yesu. Hiyo ndiyo tiba dhidi ya maovu yote: Kaa na Yesu ndani yako daima, iwe katika mambo ya kiroho, kama vile pia katika mambo ya kimwili. Na Yesu atachukua jukumu la kukuletea amani na kukusaidia kutekeleza wajibu zako. Yaani Yesu ndiye atatenda ndani yako. Kila jambo linalokutesa ulitolee kwa Yesu ili aliinue na alilipie fidia. Tolea kwa Yesu hata ubaridi unaoupata. Kwa namna hiyo utakuwa na wasaa zaidi wa kuambatana na Yesu Mteswa. Kama utakuwa na Yesu, utajisahau wewe mwenyewe na utakuwa unamkumbuka daima Yesu tu. Naye Yesu atashughulikia matatizo yako yote........ Ah, ndiyo kweli, umpende zaidi na zaidi. Ni muungano na Yesu peke yake, ndio utafanya ijitokeze chemchemi mpya ya pendo linalokua na kuongezeka; kwani wakati unapokuwa na Yesu, utakuwa unampenda, na vinginevyo utakuwa unajipenda wewe mwenyewe na maovu yako tu. Ikiwa hivyo, ni picha mbaya gani utakayoleta mbele ya Yesu? Si kweli hivyo?

Nenda umwambie Mkubwa wako mwema kuwa utakuwa unatii katika mambo yote kwani yule anayetii hakosi, na Yesu Mbarikiwa atajaziliza kile kinachokosekana katika mahitaji yako. Na halafu ujue, pale Yesu anapoona anapendwa, huwa anasahau makosa yetu, na sisi tusingependa kupoteza akili yetu kwa kumkumbusha tena. Yesu anataka pawepo mapatano na maelewano kati yenu ili Yeye aendelee kuwa kati yenu.
Ninakuomba sana sala zako.

Binti mdogo wa Utashi wa Mungu

Corato, 20 Novemba 20, 1917
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 64
Kwa Bi. Mazari, wa Bari – 3 Decemba, 1937

In Voluntate Dei !

Binti yangu mwema katika Utashi wa Mungu,

Napenda kukushukuru kwa upenzi wako mkubwa kwangu na kwa kunihangaikia mie nisiyestahili. Mbingu, Mpendwa Yesu, Mama na Malkia, wao hao wakulipe kwa yote hayo. Yaani, na mimi kwa upande wangu, nitasali ili wao wakupe na kukuvalisha lile vazi la kifalme la Utashi wa Mungu na wakufunike na kukupasha joto kwa bushuti la upendo. Hata hivyo, wewe ni budi ufike na ujilete ili upate kulipokea na kulivaa vazi hilo la kifalme. Vazi hilo litakutofautisha na wengine na litakufanya utambulikane kama binti anayependelewa na Utashi wa Mungu; na Yesu pamoja na Mama, kwa mikono yao ya kimungu, watakufunika wenyewe kwa lile bushuti angavu la upendo. Wala usidhani kuwa ni vigumu sana kupata bahati kubwa hiyo. Kwa kweli ni rahisi kabisa, ili mradi tu wewe utapenda na kuazimia kwa dhati kabisa kuishi katika Utashi wa Mungu na kugeuza kila kitu utendacho kiwe ni Utashi wa Mungu. Huyu Yesu mpenzi na Mama Malkia Mtakatifu sana, wao watakuwa tayari kukusaidia. Watakuja na kuwa daima ndani na nje yako ili wakuongoze, ili wawe nuru yako na nguvu yako. Na endapo wataona udhaifu fulani ndani yako, na siyo udhaifu wa utashi, ni wao watakuongezea nguvu za ziada pale ambapo wewe unashindwa kufanikisha. Je unataka kufahamu zaidi juu ya hilo? Kwa ajili ya mtu yeyote yule anayetaka kuishi katika Utashi wa Mungu, Mama Malkia amekwisha kukubaliana na Mwanaye wa kimungu kuwa atamsaidia mtu huyo na kumwendeleza na kumkuza kwa pendo lile alilotumia kumsaidia kumlea, kumwendeleza na kumkuza Mwanae Yesu.. Kwa minajili hiyo kinachotakiwa ni uamuzi na azimio lako. Mambo mengine yatakuja yenyewe......

Haya basi, ebu kazana. Usikate tamaa kutokana na matatizo mbalimbali na mazingira ya maisha. Hayo yote ni hatua za kupitia tunapozidi kupanda kwenda juu zaidi katika Utashi wa Mungu. Na kwa namna ya pekee, katika mazingira ya mateso, Mpenzi wetu Yesu huwa anakuja kutusaidia ili tupande juu zaidi, na ili kutuwezesha tujipatie ushindi mzuri zaidi ambao siyo wa kibinadamu, bali ni ushindi wa kimungu ulio na thamani isiyo na mipaka. Oh, ningependa jinsi gani kusikia kuwa unadumu daima katika Utashi wa Mungu!

(.......) Nimekuwa ninasali daima kwa ajili ya nia na shida zako, kama vile kwa ajili ya Carmella mwema. Kwani tunajua ni mabusu na makumbatio mangapi atakayoyatoa Bwana kwa yeye mgonjwa anayeteseka na kwako wewe unayemwangalia mgonjwa akiteseka. Unajua mara nyingi ni afadhali mtu kuteseka mwenyewe kuliko kumwangalia mtu mwingine akiteswa. Kwa hiyo basi hebu badilishaneni kupeana hayo makumbatio na mabusu ya Yesu na yale ya kwenu na mwambieni Yesu hivi: “Yesu, ebu chukua utashi wetu na wewe utupatie Utashi wa kwako”. Yeye anapenda kuutoa Uhai wake na anapenda uwe unatafutwa na kutamaniwa (.......)

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu

Corato, 3 Decemba, 1937
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n 20.
Kwa Wakuu Wa Mashirika Mapadre Rogazionisti Na Masista Figlie del Divino Zelo
24 Februari, 1932

Fiat

Waheshimiwa Baba Mkuu na Mama Mkuu,

Mfariji wa kimungu, Yesu, awatulizeni na awapake mafuta ya uponyaji juu ya jeraha kubwa na la kina lililotoboka katika mioyo yenu kutokana na kifo cha mpendwa wetu M. Gesuina. Lakini, si kweli kwamba mmempoteza. Yeye ameaga akienda mbinguni. Ninyi mmejipatia sasa yule atakayekuwa mlinzi na mpatanishi wenu mbele ya Mungu kama alivyokuwa hapa duniani. Kule mbele ya safari ataendelea kutenda ile kazi ya upatanishi, hasa kwa vile ameondoka katika kipindi ambapo ninyi wapendwa viongozi pamoja na jamii nzima ya watawa mpo katika majonzi, kwani mnapenda kupata ile amani mnayoitamani sana. Roho yake nzuri, yenye utulivu, upole na amani, baada ya kuwa imekamilisha safari yake, haikuwa tena na kitu cha kufanya kwa ajili ya dunia. Mbingu ikawa inamwita kurudi kwake ilipotambua kuwa safari yake kama kiumbe imekamilika na kwa hiyo haikuwa na muda tena wa kumwacha asubiri mbali.

Kwa sababu hiyo, kwa upande wetu hakuna neno lingine la kusema isipokuwa “Asante kwa Mungu” kwa ajili ya M. Gesuina ambaye amebahatika na kusema FIAT kwa ajili yetu sisi wenyewe ambao tumempoteza. Na hiyo FIAT ndiyo itaturudishia kila kitu. Basi, uchungu na pengo tulilopata visitukatishe tamaa. Hivyo vyote ni pepo zinazoashira ujio wa neema mbalimbali, ujio wa mwanga, ujio wa misaada itakayotushangaza zaidi. Hapa pamoja nasi, tunao Utashi wa Mungu wenye maweza yote. Kwa hiyo, hamna kitu cha kuogopa hapa. Huo Utashi wa Mungu ndio utabadili mioyo na kutengeneza watu wanaotupenda. Yesu Mbarikiwa na Mama yetu wa mbinguni watakuwa pamoja nanyi ili kuwaongozeni na kuwasaidieni mambo yote yaende kadiri ya Utashi Wao mwabudiwa.

Mama yangu mpendwa na Mheshimiwa Padre, mimi nawaoneeni huruma sana. Najua kuwa msiba huu umeleta ufa katika moyo wenu wa kimama na wa kibaba. Kwa hiyo, ninamwomba Yesu awajalieni nguvu, Yeye aje na ajiweke Yeye badala ya moyo wenu, ili uchungu wenu upunguke kabisa na Yeye asimamie na kuongoza mambo yenu yote.

Nawaombeni sala zenu. Na sasa ninapowaageni katika amani ya Utashi Mkuu napenda kubusu mkono wako Mama. Nabusu na mkono wako Padre huku nikikuomba na Baraka yako ya kibaba.

Ni mimi mtumishi wenu,

Luisa Piccarreta

Corato, 24 Februari, 1932
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 77
Kwa Mkuu Wa Ngome (Duchess) Bi. M. Pignatelli, wa Pisa
25 Aprili, 1939

In Voluntate Dei!

Mheshimiwa sana katika Utashi wa Mungu,

Asante sana kwa barua yako iliyo muhimu sana na asante kwa makala ya Mama Mkubwa Sr. Landa ambayo umenitumia. Mbingu ikulipe katika Utashi wa Mungu, ili maisha yako yote yasiwe kitu tofauti sipokuwa yawe ni tendo moja endelevu la Utashi wa Mungu. Mpendwa Mama Mtawala Ngome, moyoni mwetu sisi, ni neno muhimu sana kuweza kuishi Utashi wa Mungu. Mambo mengine yote, hata yakiwa ni makubwa jinsi gani, yanabaki kuwa ni mithili ya vitone vingi vya maji mbele ya bahari. Zaidi zaidi ni kuwa, sisi tunapoishi katika Utashi Wake, Yesu mpenzi wetu ataweza kuziona hatua zake za kimungu ndani yetu, ataona ujimudu wake, ataona Pendo lake na ataona nafsi yetu yote imeongoka na kugeuka kuwa ni kitu cha kimungu, ambacho Yeye Yesu Mtamu, anaweza akakitumia kwa ajili ya kutengenezea Uhai Wake na pia akakitumia kwa ajili ya kukuzia na kuulisha huo Uhai Wake ndani yetu.

Vitu vingine vyote, hata vikiwa ni vizuri na vya kupendeza kiasi gani, huweza vikatumika kwa ajili ya kutengenezea kazi zake, lakini ni peke yake tu maisha ndani ya Utashi wa Mungu, ndiyo yanaweza kutengeneza Uhai Wake. Ona tofauti iliyopo kati ya kazi zake na Uhai Wake! Mara tu tunapoamua kutekeleza kitendo chetu katika Utashi Wake, Mbingu huteremkia juu ya kichwa chetu, Pendo la kimungu huchukua na kushika mara kiti chake cha kwanza ndani yetu. Na hapo sisi hatuwi tena ni sisi wenye kupenda au wenye kutenda kitu, bali sasa huwa ni Pendo tu la kimungu ndilo linalopenda na linalotenda chochote ndani yetu.

Kwa minajili hiyo, sisi tunakuwa sasa ni wabeba-FIAT, ambayo ndiyo inaanza kutenda mambo yake makuu ndani yetu, mambo ambayo yanawastaajabisha hata wenyewe Malaika. Kwa hiyo, hata wewe uitolee hiyo ngome yako na kuiweka katika Utashi wa Mungu, ili huo Utashi wa Mungu uweze kuingia na kutawala ndani ya watu wote watakaojitokeza na kuingia hapo.

Mpendwa wangu Mama Mtawala wa Ngome, kwa bahati mbaya, ni ukweli kwamba tumeadhibiwa kutokana na kitendo chetu cha kuwafahamisha watu, ili angalau wapate vitone tu vya ufahamu juu ya kuishi katika Utashi wa Mungu. Tumeadhibiwa na kupigwa bila kusamehewa, tumeadhibiwa kwa maumivu na mateso makali mno kiasi kwamba, isingekuwa ni kwa msaada wa FIAT, ingetakiwa tuwe tayari tumekufa kutokana na maumivu hayo makubwa yanayotutesa sana. Kitulizo pekee tunachopata ni hiki kwamba, hawawezi wakafikia kutuondolea Utashi wa Mungu. Basi nawe usali ili angalau watuache katika amani, na ili mateso hayo yote yajae na kufurika kwa ajili ya kuleta ushindi wa Utashi wa Mungu. Utashi wa Mungu peke yake uwe ndilo kimbilio letu, uwe ndiyo mafuta ya kuponyesha maumivu yetu, uwe ndiyo maficho yetu wakati wanapotudhulumu, ili wasiweze kutuona.

Padre Benedetto anakubariki, na mimi ninakukabidhi ndani na katikati ya Utashi wa Mungu nikisema, ni mimi,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu

Corato, 25 Aprili, 1939
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 132
Kwa Federico Abresch
15 Januari, 1945


Mwanangu katika Utashi Wa Mungu,

Napenda leo kujibu barua yako ya upendo sana, na ninamwomba Yesu azidi kukujalia neema zaidi na nuru zaidi ili uwasaidie watu wote waelewe namna ya kuishi katika Utashi wa Mungu. Oh, ni jinsi gani Yesu anavyotamani, hata kufikia kutoa machozi, kwa vile anapenda sana sisi tuufahamu Utashi Mtakatifu wa Mungu na kwa vile anataka Utashi huo wa Mungu utawale na utamalaki duniani pote! Ni kwa vile ni kauli ya Utatu Mtakatifu Mtukufu kwamba Utashi wa Mungu ufanyike duniani kama vile mbinguni. Kama vile kauli ya Mungu ilivyotolewa juu ya uumbwa na juu ya ukombozi, kadhalika kauli imetolewa juu ya Ufalme wa Utashi wa Mungu juu ya dunia. Na kwa hiyo Utatu utatumia mbinu zote, utamchukua mwanadamu toka pande zote za dunia: Kwa kutumia mapigo makali na hata kwa kutumia miujiza ya kutisha, hadi hilo lipate kutimia. Hilo litafikia ile hatua kwamba atakayekuwa ni sadaka ya kwanza atakuwa ni Yesu: Yeye atajiweka kuwa kichwa na utangulizi wa matendo yetu yote ili kusudi watu wote wakimbilie katika bahari ya Utashi wa Mungu..........

Na kama Yesu anatuadhibu, ni tu kwa hoja hii kwamba wanadamu, mathalan watu wa maisha ya wakfu, badala ya kumsikiliza na kumfuata Yesu kwa kuvutwa na upendo kama Yeye alivyotamani, wao lakini wameamua kumjia na kumfuata kwa njia ya adhabu...... Masikini Yesu! Ni jinsi gani anavyoteseka! Ni kwa jinsi gani anavyotamani na anavyolia! Ni vile wanadamu hawamwombi wala hawamsihii kamwe awapatie zawadi ile ya kuishi katika Utashi wa Mungu. Na pale anapofanikiwa, anamchukua mkononi mwake, anasherehekea na anajiona kuwa ni mfalme mshindi ambaye, baada ya miaka zaidi ya elfu sita ya kupambana, kupata majeraha na kufanikiwa kupata ushindi wa kwanza, na anaufurahia ushindi huo kwa kualika Mbingu yote ije kusherehekea huo ushindi wake wa kwanza. Pindi anaposherehekea anatoa na kumwachia mwanadamu Utakatifu wake, Pendo lake, Mwanga wake, na neema zake na anampatia pia na haki juu ya Makao yake ya mbinguni........ Kwa hoja hiyo, mwanadamu huyo, hata pindi yupo bado duniani yeye atakuwa tayari ni mmiliki wa Makao ya mbinguni na ataweza kujisemea hivi moyoni mwake: “Kile kinachotendeka mbinguni, ndicho na mimi nakitenda hapa duniani. Yaani, Utatu unafurahia na kujiburudisha, na mimi hapa duniani naendelea kuvuna watu zaidi na kupata ushindi mpya unaozidi kuleta furaha zaidi kule mbinguni.

Basi, uwaeleze wote kwamba, hakuna jambo kuu zaidi na hakuna tukio la kushangiliwa kwa shamrashamra zaidi, kuliko hili la kuishi katika Utashi wa Mungu: Sisi tunajitoa na tunajiweka kabisa mikononi mwa Mungu na Mungu anajiweka kuwa tayari kwa ajili yetu kiasi kwamba anatuwezesha kuwatengeneza ma-Yesu wengi kulingana na idadi ya vitendo tunavyotekeleza katika Utashi Wake Mtakatifu. Mabahari ya Utashi wa kimungu hayajafahamika bado. Kama wanadamu wangefikia kuyafahamu mabahari hayo, hakika wangejitosa na kujitumbukiza katika bahari ya Utashi wa Mungu ili tokea hapo wajipatie uhai usioweza kukoma. Kwa hiyo tuombe na tusubiri: Yesu anashikilia karne zote katika mamlaka yake. Kile ambacho hatekelezi leo hii, atakuja kukitekeleza kesho, kwa vile kwa leo hii akili za watu zimepofuka bado. Kesho kutapatikana macho yatakayokuwa na uwezo na nguvu ya kuweza kuhimili ule mwanga wa Utashi wa Mungu na Yesu atatekeleza kile ambacho hajafaulu kutekeleza bado leo hii.

Ninawasalimuni na ninawakabidhi ninyi nyote katika bahari kuu ya Utashi wa Mungu.

Binti mdogo wa Utashi wa Mungu.

Corato, 15 Januari, 1945
Luisa akiwa pamoja na Masista wa Shirika la Figlie del Divino Zelo
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 92
Kwa Bi Maria De Regibus, wa Torino

Fiat

Binti yangu Mpenzi katika Utashi wa Mungu,

Asante sana kwa matashi yako mema katika Utashi wa Mungu. Ukimya wako wa muda mrefu haukunishangaza kwa lolote kwani tunajua kuwa tunapokuwa tumekabiliwa na hali ngumu ya kunyanyaswa, kuhinishwa na kunyenyekeshwa, watu wote wanatutoroka na wengine hata wanajutia kwa nini walifahamiana na sisi. Hilo lilikwisha kutokea hata kwa Yesu. Hata hivyo, Mapenzi ya Mungu yafanyike daima. Ni Utashi wa Mungu tu ndio ulio mwaminifu, yaani unatufungulia na kutupanulia mikono yake ili kutupatia mahali hakika na salama pa kukimbilia, na ili ukatulishe kwa Pendo lake na ili Mungu Baba atuambie kila mmoja wetu: “Binti yangu, usiogope. Ebu unipe matendo yako yote kwa ajili ya kuweza kukuzia na kulishia Uhai Wangu ndani yako. Na sasa ujue kwamba, kwa mshangao na fadhaa ya wale ambao walichukia kuujua Utashi Wangu, huo Utashi wa Mungu utatawala na utajenga Ufalme wake hapa duniani. Mimi ni Mungu Mwenye enzi na nitatumia kila njia ili kumpata binadamu na kumwezesha afufuke ndani ya Utashi Wangu”.

Binti mpendwa, mimi ninasikitika juu ya Padre Beda. Ni kwa nini makala nilizoandika hazikuweza kufika kule Roma? Ni nani aliyezizuia? Wakati mimi ninapofahamu kutokana na taarifa za kuaminika kwamba kule katika Ofisi Takatifu ya Kitume kuliwafikia maombi ya watu wa sehemu zote kutaka makala hizo nilizoandika zitolewe hadharani kwa umma........Mwishowe lakini unaona kwamba Bwana anataka atende kila kitu Yeye, kama siyo leo hii, basi atatenda hivyo kesho. Kwa hiyo basi, nakushauri sana wewe usitoke kamwe nje ya FIAT kama unapenda kuwa mmoja wa wale watu walioitwa kuishi ndani ya Utashi wa Mungu na kama unataka kuendelea kushikilia kile kiti chako cha heshima. Sasa ninakuagiza ushauri wangu wa kujitahidi kumfanya Mtoto Yesu aliye Kichanga rohoni mwako, aendelee kukua, nakutakia uishi pamoja Naye, uwe unamtunza daima na kumlinda ndani yako, ukimwangalia daima ili uweze kutekeleza kile anachotaka Yeye. Uwe ukimwambia: “Nataka kuwa nakala yako Wewe”.

Nakuletea salamu na matashi mema toka kwa dada. Nikikuaga, napenda kusema ni mimi,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu.
💌Kutoka Barua za Luisa Piccarreta💌
Barua n. 31
Kwa Bi. Mazari, wa Bari

In Voluntate Dei !

Binti yangu mwema katika Utashi wa Mungu,

Mbingu ikulipe wewe kwa sadaka unazotoa katika kueneza na kuelezea kile kitabu cha Malkia wa Mbingu. Nafikiri kuwa Mama wa Mbinguni hatakoma kukuambia ‘asante, asante, binti yangu’, na anaendelea kukuandalia neema nyingine nyingi kama vile ile neema kubwa ya kukuwezesha wewe uwe daima mbadala wa Mwanae Mpenzi ili kusudi wewe uwe ni mchukuaji na mpelekaji wa neema mbalimbali, uwe mleta umoja katika familia na uwe mletaji wa misaada ya mahitaji mbalimbali.

Binti yangu, tunapotekeleza Utashi wa Mungu sisi tunapata kuwa ni watoto wa kweli wa Mama Mkuu na tunageuzwa kuwa tabernakuli ambamo Yesu hujenga makao yake. Na kwa hiyo kila kitu tunachotenda hugeuka kuwa kitakatifu, kila tufanyacho hugeuka kuwa ni sala; hata mambo yale ambayo kwa yenyewe hayana lengo hilo kabisa. Hata mambo yale ya kawaida kabisa na ya kimaumbile tu, ambayo ni mahitaji ya maisha; pale tunapotekeleza Utashi wa Mungu hayo hugeuka kuwa sala, hugeuka kuwa ni uabudu, na ni upendo kwa Yesu wetu Mtamu. Ni kwa hoja kwamba, tunapotekeleza Utashi Wake, kila kitu tutendacho kinakuwa ni kitakatifu, na kila kitu ni pendo, hata nafsi yetu nzima huwa ni takatifu.

Sasa, kuhusu yale yote mnayonieleza juu ya mtoto wenu, nionavyo mimi katika akili yangu dhaifu, inaelekea kuwa yupo bado mdogo mno. Mwacheni akomae kwanza ili ajipatie mang’amuzi zaidi ya maisha. Ndoa ni msalaba, na kumwingiza katika msalaba wakati ni mdogo vile, nionavyo mimi, siyo jambo jema. Mnajua fika kuwa kila kitu kimeandikwa kule mbinguni. Kwa hiyo, endapo jambo hilo limepangwa na Mungu, Bwana Wetu kwa kipindi kifaacho na anachoona Yeye, atamtunza na kumhifadhi huyo msichana kwa ajili ya mtoto wenu mvulana. Halafu, jambo la kuzingatia zaidi ni kuwa familia ziwe tulivu na zenye amani, kwani ni amani ndiyo iletayo furaha katika familia na wala siyo fedha. Kuna matajiri wangapi ambao wanakosa furaha kwa sababu amani haitawali katika familia zao. Basi na ninyi zingatieni sana hilo. Tena, kama mwanamke anatukuka zaidi ya mume wake, atakuwa anapenda kumtawala huyo mume na kumfanya mtumwa wake duni..........Na mambo mengine jaribuni kuyapangilia vizuri.

Napenda kukuhakikishia kuwa namwombea mama yako mpenzi ambaye ni shahidi wa kweli. Huenda Bwana atamsaidia atimize siku zake za tohorani pindi yupo bado katika maisha yake haya. Oh, je isingewezekana wewe mwenyewe kumchukua akae nawe? Ni baraka kubwa ilioje ungeipata? Ebu uwafahamishe na kuwaonyesha hao kuwa kuna mikosi anayoleta Bwana juu ya wale wasiowaheshimu na wasiowapenda wazazi wao.

Mimi ninaomba sana sala zako; nami kwa upande wangu nitakuwa nakuombea kwa moyo wote. Sitasahau kamwe juu ya mambo yale yote unayofanya kwa ajili ya Mama mpendwa wa mbinguni. Na sasa ninakukabidhi katika Utashi wa Mungu ili Mungu akulinde, akusaidie na kukutegemeza.

Ninakusalimu sana, ni mimi,

Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu